Kuna vitu viwili ambavyo ni lazima vitokee kwenye maisha ya binadamu yeyote. Vitu hivyo ni vikwazo kwenye maisha na maisha kutokuwa sawa. Vitu hivi vinaweza kuharibu maisha yako kama hujavijua vizuri. Tuliona vitu hivi kwa undani sana kwenye makala MAMBO MAWILI MUHIMU UNAYOTAKIWA KUJUA KUHUSU MAISHA. Kama hukuisoma makala hiyo bonyeza hayo maandishi kuisoma.

  Kwa kuwa sasa tunajua vikwazo ni lazima tutakutana navyo na kuna wakati tunafanya kila jitihada lakini tunaishia kuumizwa, tunafanyaje tunapokuwa kwenye hali hizo? Kujua tu hizo hali haikusaidii kuweza kupambana nazo kama hujui njia bora ya kupambana nazo.

  Hapa tutazungumzia njia bora ya kuvuka nyakati hizi ngumu kwenye maisha yako.

  Kabla hatujazungumzia njia hiyo, nitatoa mfano mmoja ambao nimeusoma na umenigusa sana. Kuna mifano mingi ya watu waliofanikiwa baada ya kutokata tamaa waliposhindwa mara kwa mara. Kwa mfano Thomas Edison aligundua taa ya umeme baada ya kushindwa mara elfu moja. Ila mfano ninaokwenda kutoa naona umekaa tofauti kidogo maana umegusa vitu viwili tulivyozungumzia, vikwazo na dunia kutokuwa sawa/kutokuwa na huruma.

  Soichiro Honda mwanzilishi wa kampuni ya HONDA, alianzia kwenye karakana ndogo ya kutengeneza vifaa vya magari. Lengo lake kuu ilikuwa ni kuuzia kampuni ya TOYOTA vipuri vya injini za magari(piston). Hivyo alifanya kazi usiku na mchana na alipokamilisha piston hizo toyota walizikataa na kumwambia hazijafikia viwango vyao. Walimrudisha shule kwa miaka miwili akajifunze zaidi. Akiwa shuleni wanafunzi wenzake na hata walimu walimcheka kwa jinsi muundo wake wa piston ulivyokuwa wa ajabu. Baada ya miaka miwili Toyota walimpa Honda mkataba wa kuwatengenezea piston kwa kuwa hakukata tamaa na alijifunza kutengeneza piston nzuri zaidi.

  Baadae alipanga kuanzisha kiwanda kikubwa cha kuzalisha piston hizo. Ila alikosa msaada kutoka serikali ya Japan kwa sababu wakati huo serikali ilikuwa inajiandaa kwa vita kuu ya pili ya dunia. Hakukata tamaa wala kulalamika bali alitafuta njia nyingine ya kujenga kiwanda hicho. Wakati wa vita ya pili ya dunia kiwanda chake kililipuliwa na mabomu mara mbili. Hakukata tamaa bali alikusanya wafanyakazi wake na kuwaambia wakusanye mabaki ya silaha za vita na kuyatumia kwenye uzalishaji.

  Baada ya vita kuisha kiwanda chake kiliharibiwa kabisa na tetemeko la ardhi, hakulalamika wala kukata tamaa, bali aliuza masalia ya kiwanda chake kwa toyota na kupanga kuanzisha kingine. Baada ya vita Japani ilikumbwa na uhaba mkubwa wa mafuta ya magari, hivyo Honda alikosa hata mafuta ya kuweka kwenye gari ili kwenda kwenye shughuli zake. Hivyo ilimlazimu kutengeneza injini ndogo na kuiweka kwenye baiskel ili aweze kutumia kwenda mjini.

honda2 

  Alifanikiwa kujitengenezea usafiri huo rahisi na kila alikopita kila mtu alitaka nae atengenezewe usafiri huo. Alianza kuwatengenezea watu mpaka alipoishiwa na vifaa kabisa. Bado uhitaji ulikuwa mkubwa, hivyo ilimlazimu kuongea na wauzaji wa baiskel washirikiane ili aweze kutengeneza aina hiyo ya usafiri kwa kiwango kikubwa.

  Baada ya muda mfupi na baada ya marekebisho machache kwenye usafiri huo honda alikuwa mzalishaji mkubwa wa PIKIPIKI duniani. Baadae alikuwa mazalishaji wa magari na vyombo vingine vya moto na kuna wakati aliipiku hata TOYOTA.

 honda3

  Tunajifunza nini kwenye hadithi hiyo ya mafanikio ya Bwana Honda?

  Hakukatishwa tamaa na vikwazo vingi alivyokutana navyo, hakulalamika kwa dunia kutokuwa sawa na kutomuonea huruma. Yeye aliendelea kutafuta kile alichokuwa anakitaka. Kwa kifupi alifanya MAAMUZI.

  Pamoja na uvumilivu na kujihamasisha, maamuzi ni kitu cha msingi sana kwenye maisha. Pale unapofanya maamuzi ya kitu unachotaka na kufanya kila unachoweza kukipata kunakupatia nguvu kubwa ya kuendelea hata unapokutana na vikwazo.(soma; tatizo hujafanya maamuzi)

  Amua sasa kuwa kiongozi wa maisha yako. Amua kufanikiwa kwenye shughuli yoyote unayofanya na amua kuyasimamia na kuheshimu maamuzi yako.

  Bila ya kuwa na maamuzi thabiti ni rahisi sana kukata tamaa na kuona mambo hayawezekani. Hakuna linaloshindikana kama kweli utafanya maamuzi na kisha kuwa na malengo na mipango ya maisha yako.

 

Fanya maamuzi ya kubadili maisha yako sasa kwa kuungana na watanzania wenzako waliochukua hatua dhidi ya maisha yao kwa kujiunga na kundi hili SAA KUMI NA MOJA ALFAJIRI TANZANIA(bonyeza hayo maandishi kujiunga)