Rafiki yangu mpendwa,

Wote tunajua ya kwamba chanzo cha furaha kwenye maisha, chanzo cha mafanikio makubwa kwenye maisha yetu kipo ndani yetu wenyewe. Kipo kwenye fikra zinazotawala akili zetu, hisia tunazokuwa nazo na hata hatua tunazochukua.

Katika kujifunza kuhusu mafanikio, tumekuwa tunaambia kila tunachopaswa kufanya, kila tabia tunayopaswa kujijengea ili kufanikiwa. Hivyo tunaweza kusema bila ya wasiwasi wowote kwamba kila mtu anajua anapaswa kufanya nini ili afanikiwe. Hata wale ambao hawajafanikiwa, na ambao hawajisumbui na mafanikio, wakimwona mtu aliyefanikiwa, wanajua amefanya nini mpaka kufika pale.

Mwandishi na mwanasaikolojia Amy Morin kupitia kazi yake ya kuwashauri watu wengi wanaopitia magumu kwenye maisha yake, aligundua kwamba watu wengi wanajua nini wanapaswa kufanya ili wawe na maisha ya furaha na mafanikio.

Lakini licha ya kujua hayo muhimu na kuyafanya, bado walikuwa wanarudi nyuma, hawapati furaha na mafanikio waliyopata. Na katika kuchunguza hilo, aligundua licha ya watu kufanya yale waliyopaswa ili kufanikiwa, pia walifanya mambo mengine ambayo yaliwarudisha nyuma.

Kwenye kitabu chake cha 13 THINGS MENTALLY STRONG PEOPLE DON’T DO, Amy anatushirikisha vitu 13 ambavyo tunapaswa kuacha kuvifanya mara moja kama tunataka kuwa na maisha yenye furaha na mafanikio makubwa. Ukiangalia vitu hivi kumi na tatu, utaona jinsi ambavyo vingi vinaonekana ni vya kawaida kwa sababu kila mtu anafanya. Lakini kwa hakika, vitu hivyo kumi na tatu vinawarudisha wengi nyuma.

13 things mentally strong dont do

Karibu kwenye uchambuzi huu wa kitabu, tujifunze vitu 13 ambavyo unapaswa kuacha kufanya mara moja, na uache kuvifanya kweli ili uweze kufanikiwa.

Kwenye uchambuzi huu nikakushirikisha vitu hivyo 13, na jinsi kila kimoja kinakurudisha nyuma na hatua za kufanya ili usiendelee kurudishwa nyuma na vitu hivyo.

Kwenye kitabu hichi, Amy ameanza kwa kutushirikisha mfano halisi wa maisha yake, ambao ulimfanya atetereke sana na kuhitaji kuwa imara kifikra. Alipata msiba wa ghafla wa mama yake mzazi na haikuchukua muda mume wake kipenzi pia akafariki. Ni katika kipindi hicho kigumu cha maisha yake alijifunza jinsi ya kuwa imara kifikra ili changamoto yoyote anayokutana nayo isimtetereshe.

Kila mmoja wetu anakutana na changamoto mbalimbali kwenye maisha, kuanzia misiba ya watu wa karibu kwetu, kupoteza kazi au biashara, kupoteza fedha nyingi na kadhalika. Matukio haya kama yatakukuta hujajiimarisha kifikra, yanatosha kuharibu kabisa maisha yako.

Karibu tujifunze vitu 13 vya kuacha kufanya ili tuwe imara kifikra na tuweze kukabiliana na changamoto yoyote, tuweze kuwa na maisha ya furaha na mafanikio makubwa.

MOJA; USIPOTEZE MUDA KUJIONEA HURUMA.

Watu wengi wamekuwa wanapoteza muda wao kujionea huruma kwa mambo ambayo yametokea kwenye maisha yao. Wanajiona ni wanyonge na hawana cha kufanya. Amy anatuambia watu walio imara kifikra huwa hawajionei huruma kwa lolote. Chochote kinachotokea, wanakipokea kama kinavyokuja na kuchagua kuchukua hatua ili maisha yaendelee.

Amy anatuambia kwamba watu wengine amekuwa wanatumia matukio mabaya yanayotokea kwao kama njia ya kuonewa huruma na wengine, au kutaka kupata msaada kwa wengine. Kwa njia hii wengi wamekuwa wanakaribisha matukio mabaya, au yakiwatokea huwa hawataki yaondoke ili wapate kitu cha kujitetea kwa wengine. Chukulia mfano wa watu ambao kila ukikutana nao wana kitu kibaya cha kukuambia kinachoendelea kwenye maisha yao.

Kuondokana na tabia ya kujionea huruma na kujiona mnyonge usiye na cha kufanya, Amy anakuambia ukubali kila linalotokea kwenye maisha yako, na usione ni wewe tu mabaya yanatokea kwako. Jua ni sehemu ya maisha na chukua hatua ili kuwa bora zaidi. Pia unahitaji kuwa mtu wa shukrani, kwa chochote kinachotokea kwenye maisha yako, shukuru kwamba upo hai, na jua kuna kitu unaweza kufanya maisha yako yakawa bora zaidi.

MBILI; USIPOTEZE NGUVU ZAKO KWA WENGINE.

Kosa kubwa ambalo watu wamekuwa wanafanya kwenye maisha yao na linawagharimu sana ni kupoteza nguvu zao kwa wengine. Pale wanapowaruhusu watu wengine kuwa na mamlaka makubwa kwenye maisha yao kuliko wao wenyewe.

Hawa ni watu ambao wanapenda kuwafurahisha wengine na wanaopenda kumridhisha kila mtu. Watu ambao wanaogopa kusema hapana hata kama hawataki kufanya kitu. Kama umewahi kusema ndiyo kwenye kitu ambacho moyoni unataka kusema hapana, na umesema ndiyo ili tu kumridhisha mtu mwingine, basi jua umeshapoteza nguvu zako kwa mtu huyo.

Huwezi kufanikiwa kwenye maisha yako na hutakuwa na furaha kama huwezi kujiwekea mipaka kwenye maisha yako, kama huwezi kusema hapana kwa jambo usilohitaji kufanya au lisilo muhimu, utaishia kuwa mtumwa wa wengine, utasema ndiyo ambazo zitayafanya maisha yako kuwa magumu na yasiyo na maana.

Amy anatuambia kuweza kurudisha nguvu zetu kutoka kwa wengine, kwanza lazima mtu ujiamini na ujue huwezi kumridhisha kila mtu. Pia lazima ujue huhitaji kufanya kila ambacho unafikiri ni lazima kufanya. Chagua vitu muhimu kwako ambavyo uko tayari kufanya na upo tayari kusema ndiyo, na vile vingine visivyo muhimu sema hapana. Na usiogope kusema hapana kwa yeyote, na wakati mwingine huhitaji hata kutoa sababu za kusema hapana. Sema hapana na weka juhudi kwenye yale muhimu kwako.

TATU; USIOGOPE MABADILIKO.

Mabadiliko ni kitu ambacho hakikwepeki kwenye maisha, kama wewe utagoma kubadilika, basi mazingira yanayokuzunguka yatabadilika. Na pale unapostuka na kugundua mazingira yamebadilika, basi jua umeshaachwa nyuma.

Watu wengi wamekuwa wanaogopa kufanya mabadiliko kwenye maisha yao kwa sababu mabadiliko ni magumu. Pia mabadiliko yanamaanisha kuachana na kitu ambacho mtu umezoea na kwenda kwenye kitu ambacho mtu huna uhakika nao. Unafikiri kwa nini watu wengi hung’ang’ana kwenye ajira ambazo zinawalipa kidogo kwa miaka mingi na wasithubutu kuondoka na kuingia kwenye biashara ambazo zinaweza kuwalipa zaidi? Wengi wanapenda kipato kidogo cha uhakika, kuliko kipato kikubwa kisicho cha uhakika.

Ili kuondokana na hali ya kuogopa mabadiliko, Amy anatuambia tunahitaji kujua mabadiliko gani tunataka kufanya kwenye maisha yetu, kisha kuchukua hatua ndogo ndogo. Unapochukua hatua ndogo ndogo, unaipunguza hofu ya mabadiliko uliyonayo. Kwa hatua ndogo kwanza unaweka lengo unalotaka kutimiza miaka 30 ijayo, kisha jua tabia unazohitaji kujijengea ili kufikia lengo hilo, jua hatua unazohitaji kuchukua kila siku ili kufikia lengo lako. Kila siku chukua hatua ulizopanga kuchukua na hakikisha unakua na njia ya kujipima kwa hatua unazochukua.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; FACTFULNESS (Maeneo Kumi Tunayokosea Kuhusu Dunia Na Kwa Nini Mambo Ni Mazuri Kuliko Unavyofikiri).

NNE; USIPOTEZE MUDA WAKO KWENYE VITU AMBAVYO HUWEZI KUVIDHIBITI.

Kila kitu kinachotokea kwenye maisha yako, kinaweza kuwa kwenye moja ya makundi haya mawili, kundi la kwanza ni vitu ambavyo viko ndani ya uwezo wako, hivi unaweza kuvidhibiti na kubadili kitu. Kundi la pili ni vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako, hivi huwezi kuvidhibiti wala kubadili chochote. Sasa kwa akili ya kawaida, unapaswa kuhangaika na vile unavyoweza kudhibiti tu, huku ukiacha na usivyoweza kudhibiti.

Lakini huwezi kuamini ni muda kiasi gani umekuwa unapoteza ukihangaika na vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako, vitu ambavyo huwezi kuvidhibiti wala kuvibadili.

Watu wengi wamekuwa wanapenda kudhibiti kila kinachoendelea kwenye maisha yao, bila kujiuliza kama kipo ndani ya uwezo wao. Amy anatuambia watu ambao wanapenda kudhibiti kila kitu ni watu ambao wana wasiwasi na maisha yao, hivyo kupunguza wasiwasi wao, hupenda kujihakikishia kila kitu kipo chini ya udhibiti wao, jambo ambalo hawawezi kulikamilisha maana vitu vingi hawawezi kudhibiti.

Kuondokana na tabia hii ya udhibiti, jua ni vitu gani vipo ndani ya uwezo wako na vilivyo nje ya uwezo wako. Na usijisumbue na vilivyo nje ya uwezo wako. Mfano usipoteze muda wako kukazana kuwabadili watu, hutaweza na watakusumbua sana. Badala yake chagua kujihusisha na watu unaoweza kuendana nao kwa jinsi walivyo. Pia pale inapohitajika, badilika wewe na itakuwa rahisi kwa wengine kubadilika, kwa kutaka wao wenyewe.

TANO; USITAKE KUMRIDHISHA KILA MTU.

Watu wengi hufikiri kwamba ili wafanikiwe kwenye maisha basi lazima wapendwe na kila mtu, hivyo hujaribu kufanya mambo ambayo yanawafurahisha wengine, hata kama siyo mambo wanayojali kufanya. Hili limekuwa linawafanya watu waonekane siyo halisi na wanaigiza na pia wasiaminike.

Chukua mfano wa mtu ambaye anataka kuonekana wa aina fulani ili kupewa nafasi fulani, iwe ni kwenye kazi, biashara na hata kwenye mafanikio. Watu hao wanapofanikiwa kupata nafasi hizo, huwa hawezi kuendelea kuigiza maisha waliyoigiza ili kupata nafasi walizopata, na hapo ndipo matatizo mengi kwenye maisha yanapoanzia.

Ili kuwa na maisha ya furaha na hata kufanikiwa, Amy anatuambia lazima tujijue sisi wenyewe, tujua tunathamini nini kisha kuishi maisha ya uhalisia kwetu. Tukijua kwamba kwa kuishi maisha ya uhalisia kwetu, kuna watu hawatakubaliana na sisi wala kutupenda, lakini wapo ambao watakubaliana na sisi na kutupenda, na hawa ndiyo muhimu zaidi.

Hakuna chochote utakachofanya kwenye maisha na ukamfurahisha kila mtu au kupendwa na kila mtu. Na pale unapoigiza maisha fulani ili kuwafurahisha watu fulani, unavutia watu ambao siyo halisi kwako. Ishi maisha ya uhalisia kwako, hapo utawavutia watu sahihi ambao utaweza kwenda nao vizuri.

SITA; USIOGOPE KUCHUKUA HATUA ZA HATARI.

Hakuna mafanikio yanayopatikana kwenye maisha bila ya kuchukua hatua ambazo ni hatari. Kutoka tu nyumbani kwako ni hatari, unaweza kugongwa na gari, unaweza kushambuliwa na watu na kadhalika.

Lakini watu wengi wamekuwa wanaogopa kuchukua hatua ambazo zinaonekana ni za hatari ili kupata wanachotaka kwenye maisha yao. Na hatari nyingi ambazo watu wanaogopa, huwa hawaogopi kutokana na uhalisia wa hatari hizo, bali wanaogopa kutokana na hisia ambazo mtu anakuwa nazo kwenye hatari husika.

Amy anasema, kipimo tunachotumia kwenye kupima hatari kwa wengi siyo kipimo sahihi. Kwa mfano, watu wakiwa wanapenda kitu fulani, watakifanya hata kama kina hatari kubwa, wakati wataogopa kufanya kitu chenye hatari ndogo kama hawakipendi.

Kuondokana na hali hii ya kuogopa kuchukua hatua za hatari, lazima mtu ujue nini unataka, kisha ujue hatari unayohitaji kuingia ili kupata unachotaka, baada ya hapo kuchukua hatua sahihi ili kupata unachotaka, huku ukiwa na mbadala unaozuia hatari yoyote unayokutana nayo isikupoteze kabisa.

13 things mentally strong dont do 2

SABA; USIZAME KWENYE YALIYOPITA.

Kuna mambo makubwa, mabaya na magumu sana umewahi kukutana nayo kwenye maisha yako. Kuna watu walikunyanyasa, kukutesa, kukudhulumu na kukuumiza sana kwenye maisha yako. Lakini sasa upo hapo ulipo sasa, unachagua nini? Kuendelea kuzama kwenye yaliyopita au kuangalia wapi unakokwenda?

Watu wengi wamekuwa wanazama kwenye yaliyopita, kujikumbusha mabaya yote waliyopitia na hilo linawazuia kupiga hatua. Wengi wanaoangalia nyuma ni wale ambao wameshakata tamaa na maisha yao, au wanatumia matukio ya nyuma kama sababu kwa nini wapo pale walipo sasa au hawawezi kufanya zaidi.

Ili kuwa na maisha ya furaha, ili kufanikiwa, unahitaji kuachana na ya nyuma na kuangalia mbele. Unapoachana na ya nyuma haimaanishi unayafuta kabisa, hapana, unajifunza kupitia hayo ya nyuma, lakini huyatumii kama sababu kwa nini hupigi hatua zaidi. Badala yake unaweza nguvu na muda wako kwa wapi unaenda kuliko ulikotoka.

Na wale ambao huwa wanajiambia enzi zangu nilikuwa hivi au vile, jua umekata tamaa na maisha yanakuacha. Acha mara moja kujisifia kwa vitu vya nyuma, na tengeneza sifa mpya za leo na kesho.

SOMA; Mambo 6 Unayalazimika Kuyaacha Mara Moja Ili Kufanikiwa.

NANE; USIRUDIE KOSA MOJA MARA KWA MARA.

Kila mtu huwa anafanya makosa kwenye maisha yake, lakini watu wa hovyo kabisa, ni wale wanaorudia makosa yale yale mara kwa mara. Hawa ni watu wa hovyo kwa sababu hawataki kujifunza na wanajirudisha wao wenyewe nyuma. Hivi kwa mfano ukashika kitu halafu ukaugua, ukatoa mkono haraka. Halafu hapo hapo ukajiambia labda nilishika vibaya, unashika tena, unaungua, unaondoa mkono, unajiambia tena labda sikuwa na bahati, acha nibahatishe tena, unashika unaungua!

Hivi ndivyo wengi wanafanya kwenye maisha, kazi na hata biashara. Angalia mtu yeyote ambaye anateseka na maisha yake, ambaye kazi haimpeleki popote na ambaye biashara inakufa, utakuta kuna makosa anayarukia mara kwa mara kwenye maisha yake.

Ili kuondokana na hali hii ya kurudia makosa yale yale, jipe muda wa kutafakari kila kosa unalofanya na jiulize yafuatayo; nini hakikuenda sawa? Ni nini ningeweza kufanya kwa ubora zaidi? Na ni kipi nitafanya tofauti wakati mwingine? Jiulize na jipe majibu ya maswali hayo kisha chukua hatua sahihi.

TISA; USICHUKIE MAFANIKIO YA WENGINE.

Hakuna kitu kinawazuia watu kufanikiwa kama kuchukia mafanikio ya wengine. Hivi unajua kwa nini masikini wengi huwa hawawi matajiri, kwa sababu wanawachukia matajiri, kwa sababu wameaminishwa matajiri ni watu wabaya, watu wasiojali, watu wasio na huruma na wanaowadhulumu au kuwatesa wengine.

Hutaweza kuwa na furaha kwenye maisha yako kama unachukia pale unapoona wengine wana furaha kuliko wewe. Na hutafanikiwa kama kila aliyefanikiwa unamwona ni mbaya kwako.

Ili kuondokana na chuki hii ya mafanikio ya wengine, kwanza jua mafanikio kwako yana maana gani, kwa sababu mafanikio yanatofautiana kwa kila mtu. Unachoona wengine wamefanikiwa, ukipewa wewe kinaweza hata kisikufurahishe. Pili jua kila mtu anapambana na magumu yake, unaweza kuona watu kwa nje ukasema wamefanikiwa sana, ila ukapewa maisha yao na ukatamani maisha yako mara mia. Tatu, jua chochote ambacho wengine wamepata na wewe pia unaweza kupata. Hivyo unapoona wenzako wamepiga hatua, furahi, maana ni kiashiria kwamba na wewe unaweza kupiga hatua na kufanikiwa zaidi.

KUMI; USIKATE TAMAA BAADA YA KUSHINDWA MARA MOJA.

Ni mambo machache sana utayapata kwenye maisha yako kwa kujaribu mara moja, na hayatakuwa makubwa. Mambo mengi kwenye maisha yako, na hasa yale makubwa, utayapata baada ya kushindwa mara nyingi na kurudia tena na tena na tena. Kushindwa mara moja haimaanishi kwamba wewe huwezi, bali ina maanisha hujajua njia sahihi ya kufanya ili kupata.

Hivyo unaposhindwa kwenye chochote unachofanya, kaa chini na kuona wapi unakosea, kisha panga mkakati wa hatua sahihi za kuchukua na rudi tena. Ukishindwa tena kaa chini na tafakari wapi unakosea kisha fanya tena.

Thomas Edison aliposhindwa mara elfu kumi kutengeneza taa ya umeme, watu walimwambia ameshindwa mara elfu kumi, lakini yeye alikataa, alisema hajashindwa mara elfu kumi, badala yake amejifunza njia elfu kumi zisizo sahihi za kutengeneza taa ya umeme. Je wewe umeshajifunza njia zisizo sahihi ngapi mpaka uwaambie watu umeshindwa na hufanyi tena?

KUMI NA MOJA; USIOGOPE MUDA WA PEKE YAKO.

Kama kuna kitu watu wanakiogopa zama hizi, basi ni kuwa wao peke yao, kwenye hali ya utulivu. Naweza kusema hili ni jambo linalowatisha watu zama hizi kuliko wakati mwingine wowote. Na wala huhitaji kwenda mbali kudhibitisha hili, wewe panda tu kwenye gari na angalia watu wanafanya nini, nenda eneo ambalo watu wanasubiri huduma fulani na angalia watu wanafanya nini. Kila mtu utamkuta anajisumbua na kitu fulani. Asilimia tisini utawakuta wameinama kwenye simu zao, waliobaki utawakuta wanasoma magazeti, au wanashangaa shangaa tu.

Zama hizi watu wako bize kiasi kwamba wakipata muda mfupi wa kukaa wao wenyewe wanautumia kwa usumbufu, hawa wa simu na mitandao ya kijamii. Haya siyo aina ya maisha yanayoweza kuwa ya furaha na mafanikio.

Amy anatuambia tunapaswa kupenda na kutenga muda wa kuwa sisi peke yetu katika siku zetu. Huu ni muda ambao haturuhusu usumbufu wa yeyote au chochote uingie kwenye fikra zetu. Na huu ndiyo muda tunaoutumia kuyatafakari maisha yetu kwa pale tulipo sasa na hata tunapokwenda.

Amy anatuambia kuna vitu viwili muhimu tunapaswa kufanya kila siku ili kujiondoa kwenye usumbufu na kurudisha utawala wetu kwenye muda wetu. Vitu hivyo ni kufanya tahajudi (meditation) na kuwa na uwepo (mindfulness) kwenye kila tunachofanya.

SOMA; Mambo Mawili Muhimu Unayotakiwa Kujua Kuhusu Maisha

KUMI NA MBILI; USIFIKIRIE UNAIDAI DUNIA CHOCHOTE.

Kizazi cha zama hizi ni kizazi cha ajabu tangu kumekuwepo kwa wanadamu hapa duniani. Katika vizazi vya nyuma, watu walijua kabisa maisha yao ni jukumu lao, na kama hawakuchukua hatua basi maisha yao yalipotea mara moja. Kama mtu hakulima, au kwenda kuwinda, au kuweka juhudi ili maisha yaweze kwenda, mambo yalikuwa magumu kwake.

Lakini zama hizi watu wanapenda kulalamika kwa kila kitu, watu wanategemea kupewa kila kitu, watu wanalalamikia serikali, wazazi, ndugu, uchumi na hata mazingira na hali ya hewa kama sababu ya wao kutokufanikiwa.

Amy anatuambia ili tuwe na maisha ya furaha, ili tufanikiwe, lazima tujue kwamba hatuidai dunia chochote, hatustahili kupewa chochote na tuache kuwa na mategemeo makubwa kutoka kwa wengine na dunia kwa ujumla. Badala yake tuweke juhudi kwa chochote tunachotaka, na tuwe tayari kukosa licha ya kufanya kila tunachopaswa kufanya. Tusiwe watu wa kulalamika, badala yake tuwe watu wa kuchukua hatua.

KIMI NA TATU; USITEGEMEE MATOKEO YA HARAKA.

Watu wengi wapo tayari kuweka mipango mikubwa, na wapo tayari kuchukua hatua ili kufikia mipango yao, ila wengi wanakosa uvumilivu, na hilo ndiyo linawazuia kufanikiwa.

Hakuna mafanikio ya haraka, hakuna njia ya mkato ya kufika kwenye mafanikio makubwa. Na hata ikiwepo njia ya aina hiyo, matokeo yake huwa siyo mazuri mwishoni.

Kama unataka mafanikio ya kweli na yanayodumu, kama unataka kuwa na maisha bora na yenye furaha, Amy anatuambia tunapaswa kuwa wavumilivu na wenye subira. Licha ya kuweka juhudi kubwa, tunapaswa kuweka subira, tukijua mambo mazuri hayataki haraka. Na kadiri tunavyotegemea matokeo makubwa, ndivyo tunavyopaswa kuwa na subira zaidi.

Amy anatuambia pia tunapaswa kuwa tayari kupoteza raha ya muda mfupi kwa ajili ya kutengeneza furaha ya muda mrefu. Kwa sababu kinachowazuia wengi wasifanikiwe, ni kutaka raha za muda mfupi. Na chochote kinachokupa raha ya haraka, jua kinakuzia kupata furaha kubwa baadaye. Mfano kama una changamoto fulani, unaweza kuweka muda kuitatua, au ukatumia kilevi na kuisahau kwa muda. Njia bora siyo kujisahaulisha kwa kilevi, bali kutatua.

HITIMISHO; ISHI MISINGI HII NA USIOGOPE UNAPOANGUKA.

Ili kuimarisha uimara wako kifikra na kuweza kuwa na maisha ya furaha na mafanikio makubwa, haitoshi tu kujifunza na kufurahia. Bali unahitaji kuchukua hatua na kuishi misingi hii kwenye maisha yako. Jikumbushe kila siku na acha kufanya mambo haya kumi na tatu. Katika safari yako ya maisha kuna wakati utajisahau na kufanya mambo haya, usikate tamaa na kuona huwezi, bali jikumbushe siyo mambo sahihi kwako kufanya na usirudie tena.

Kuwa kocha wako mwenyewe, kwa kusimamia fikra zako, kudhibiti hisia zako na kutafakari hatua unazochukua ili kuweza kuwa na maisha bora, yenye furaha na mafanikio makubwa kwa kuepuka mambo hayo 13 yanayowaangusha wengi.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji