Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Hatimaye tumefika hatua ambayo kila kitu sasa kinafanana.

Ujio wa Akili Unde (Artificial Intelligence – AI), umewapa watu wote nguvu sawa ya kuzalisha chochote wanachotaka.

Ugumu uliokuwepo kwenye kuzalisha vitu mbalimbali, na ambao ndiyo uliwatofautisha wenye uwezo na wasiokuwa nao sasa umeondolewa kabisa.

Kila mtu anaweza kuzalisha kitu chochote anachotaka kwa kuiambia tu Akili Unde imtengenezee kitu hicho.

Mtu asiye na utaalamu wowote wa kompyuta wala mifumo yake, anaweza kuiambia akili unde imtengenezee tovuti au programu za kompyuta. Na akili unde itafanya hivyo na kumpa kitu kama anavyotaka.

Pamoja na urahisi huo wa kuzalisha chochote ambacho mtu anataka, kumekuwa na mfanano usio wa kawaida kwenye vitu vinavyozalishwa kwenye zama hizi.

Ukiangalia vitu vingi vinavyozalishwa sasa, vina mfanano mkubwa. Ule upekee uliokuwa unaletwa na ubunifu wa tofauti walionao watu umeondoka kabisa.

Angalia picha na matangazo mengi yanayoandaliwa sasa, kuna mfanano mkubwa sana. Angalia tovuti na programu za kompyuta, utaona mfanano mkubwa.

Angalia hata uandishi na mawasiliano ya watu, kwa sasa yamekuwa yanafanana sana. Ilizoeleka kuwepo na makosa makosa kwenye maandishi ya watu, lakini pia maandishi hayo kuwa ya kipekee. Lakini kwa sasa maandishi hayana makosa kabisa, ila pia yanafanana sana.

Pamoja na watu kufurahia urahisi huu ambao umeletwa na akili unde, kuna hatari kubwa ya kuondoa ule utofauti na upekee ambao ndiyo unawapa watu mafanikio na kuwafanya wadumu nayo.

Hakuna ubaya wowote kwa watu wengi kufanikiwa kwa sababu mambo yamerahisishwa. Lakini, kwa bahati mbaya sana, kwa mambo kurahisishwa, yale manufaa yaliyokuwa yanaleta mafanikio yanaondoka.

Yaani kama kitu kilikuwa kinaleta mafanikio kwa watu, kwa sababu kulikuwa kigumu na cha kipekee kufanya, kinapokuwa rahisi hakiwezi tena kuleta mafanikio kwa wengi. Badala yake kinapoteza nguvu ya kuleta mafanikio. Na hiyo ndiyo hali tunayopitia sasa kwenye akili unde.

Kwa sababu watu wote sasa wanaweza kupata matokeo sawa, matokeo hayo yamekosa nguvu ya kuwapa watu mafanikio makubwa wanayoyataka. Hili limewafanya watu waamini hakuna tena namna ya kujitofautisha kwenye zama hizi za akili unde.

Mimi rafiki yako, ambaye nimejipa wajibu wa mafanikio yako, nakuambia bado nafasi kubwa ya wewe kujitifautisha ili uweze kujenga na kulinda mafanikio yako makubwa.

Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza njia pekee ya kujitofautisha ili uweze kujenga na kulinda mafanikio makubwa.

1. Ngome Imara, Yenye Mtaro Wa Kina Wenye Papa.

Bilionea mwekezaji Warren Buffett huwa ana kauli yake maarufu inayosema; “Biashara nzuri ni kama ngome imara, yenye mtaro mpana na wa kina unaoizunguka. Nataka kuwe na papa ndani ya mtaro huo. Nataka iwe kitu kisichoweza kuguswa na yeyote.”

Buffett amekuwa akitumia mwongozo huo kuchagua ni aina gani ya biashara anayoweza kununua na kuwekeza ili kupata faida kubwa. Biashara inayofanikiwa ni inayokuwa na sifa hizo tatu; ngome imara ambayo ni thamani inayotoa, mtaro wa kina ambao ni kitu kinachoitofautisha na papa ambao ni mikakati ya kipekee.

Kwa kuwa amekuwa kwenye tasnia ya uwekezaji kwenye biashara kwa zaidi ya miaka 70, na amepata mafanikio makubwa kwenye tasnia hiyo, anachosema kina usahihi mkubwa.

Lakini sasa, kwenye zama hizi za akili unde, inaonekana ni vigumu kwa biashara na hata watu kujitofautisha, kwa sababu watu wote wanaweza kupata majibu sawa kwenye mambo wanayofanya.

Ujio wa Akili Unde umefanya watu wengi kuamini kwamba hakuna tena njia ya watu na biashara kujitofautisha na kuwa na upekee. Kwa sababu kila mtu anaweza kupata majibu pale anapokutana na changamoto yoyote, inaonekana mambo ni rahisi kwa watu wote.

Ukweli ni kwamba, ujio wa akili unde na kurahisisha mambo umefanya kujitofautisha kuwe kugumu zaidi. Na kwa ugumu huo, kujitofautisha kumekuwa kwa thamani kubwa zaidi kwenye zama hizi.

Kwa msingi huo wa Buffett wa kuwa na ngome imara, yenye mtaro wa kina na papa, tunaenda kuangalia jinsi ya kutumia kwetu binafsi na kujitofautisha na wengine wanaoweza kufanya kila tunachofanya.

2. Ngome Yako; Mchezo Kwako, Kazi Kwa Wengine.

Kujitofautisha kunaanza na ngome yako imara, ambayo ni kile unachopenda sana kufanya kuliko wengine wote. Hiki ni ambacho kwako kinaonekana kama mchezo, lakini kwa wengine ni kazi ngumu. Kwa kuchagua kitu hicho unachopenda kufanya, utakifanya kwa kujali zaidi na hivyo kupata matokeo ya tofauti.

Unapochagua kufanya kile unachopenda, ambacho kwako ni kama mchezo, hutafuti njia za mkato za kukifanya. Hivyo hutahangaika sana na akili unde kwenye ufanyaji wa kitu hicho, kwa sababu hukimbilii kupata njia ya mkato ya kufanya. Wewe kinachokuwa kinakusukuma ni kufanya hicho unachopenda kufanya.

Akili unde imerahisisha kila mtu kuweza kufanya chochote na kupata matokeo, hata kama ni kitu ambacho hakipendi wala hana uzoefu nacho. Hilo unawaachia hao wasiopenda wala kuwa na uzoefu. Kwa mapenzi na uzoefu wako kwenye kitu unachopenda kufanya, tayari unakuwa na upekee wa tofauti kwako.

Ukishajua kile hasa unachopenda kufanya na kukipa kipaumbele kwenye kufanya kwa upekee na utofauti, unakuwa na ngome ambayo hakuna anayeweza kuingia na kukuvuruga. Ni vigumu sana kushindana na mtu ambaye anaona ni mchezo kile ambacho wengi wanachukulia ni kazi ngumu.

Huenda kazi au biashara unayofanya sasa ni kwa sababu tu inakuingizia kipato unachokihitaji sana. Hapo unakuwa huna cha kukutofautisha na wengine, ambao pia wanasukumwa na kipato. Lakini kwa kwenda kwenye kile unachopenda kufanya, mambo yanabadilika kabisa.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK138; Tofauti Kwenye Mfanano, Njia Pekee Ya Kupata Na Kulinda Mafanikio Makubwa Kwenye Zama Za Akili Unde (AI)