Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Watu wengi hudhani kama hawajaajiriwa basi wapo huru. Kwa sababu wao ndiyo wanaamua kipato chao, iwe ni kwa kujiajiri au biashara, wanaona hakuna kinachoweza kuwazuia kujenga utajiri wanaotaka.
Lakini pamoja na matamanio hayo makubwa ya watu kujenga utajiri kwa kujitegemea wao wenyewe, bado wengi wameshindwa kutimiza hilo. Wengi wamejikuta wakikwama kujenga utajiri mkubwa kama walivyotaka, licha ya kutokuwa na yeyote anayewapangia kipato.
Hii ni hali ambayo wengi wanashindwa kuelewa kwa nini inatokea. Pamoja na juhudi kubwa sana wanazokuwa wanaweka, bado kipato wanachoingiza na hata utajiri wanaojenga unakuwa umekwama kwenye kiwango fulani.
Wengi wanapofikia kwenye huo mkwamo, wanadhani ni njia wanayotumia ndiyo yenye shida. Hilo linawapelekea kubadili njia, ambapo wanabadili shughuli wanayofanya, lakini bado matokeo hayabadiliki.
Tatizo haliwi kwamba watu hawawezi kuingiza kipato kikubwa na kujenga utajiri, bali tatizo linakuwa ni ukomo ambao watu wanakuwa wamejiwekea wao wenyewe.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujua ukomo huo na jinsi ya kuuvunja kwa kujijengea rasilimali zitakazokupa utajiri mkubwa unaoutaka.

1. Tenganisha Muda Wako Na Pesa Zako.
Tangu nimejifunza nukuu ya Naval Ravikant, ambayo inasema; ‘Huwezi kutajirika kwa kukodisha muda wako,’ nimekuwa najitafakari sana kwenye eneo la muda na pesa. Kila njia ya kuingiza kipato ninayokuwa nayo, kitu cha kwanza kuangalia ni kama muda wangu ni lazima utumike ndiyo fedha iingie.
Nikishaona tu kwamba muda wangu ndiyo hitaji kuu kwenye njia ya kipato, naanza kufikiri kwa namna ya tofauti. Kwa wengo hawajui hili na wamekuwa wanajikwamisha wao wenyewe kupata matokeo makubwa.
Iko hivi, tuna masaa 24 tu kwa siku, hakuna anayeweza kupata hata sekunde moja ya ziada. Pale kipato kinapotegemea muda moja kwa moja, tayari kina ukomo wa masaa yanayopatikana.
Hatua ya kwanza ya kuwa huru ili uweze kujenga utajiri mkubwa ni kutenganisha muda wako na pesa zako. Ni lazima uhakikishe unao uwezo wa kuendelea kuingiza kipato bila kulazimika kutumia muda wako moja kwa moja.
Najua wengi hatuwezi kuanzia hapo, lazima tunaanzia mahali ambapo kipato chetu kinategemea muda wetu moja kwa moja. Lakini hakuna kinachotuzuia kuanza kutenganisha kipato na muda kadiri muda unavyokwenda.
Unaweza kwenda hata kwa asilimia na vipindi fulani. Kila baada ya muda unapunguza asilimia kadhaa za kipato chako kutegemea muda wako. Hata kama itakuwa ni asilimia 10 kila mwaka, ndani ya miaka 10 unakuwa umefika hatua ambayo kipato chako hakitegemei kabisa muda wako.
Huwezi kutenganisha muda wako na pesa zako kwa kutaka tu, unapaswa kujenga rasilimali ambazo ndiyo zitakuwa nyenzo kwako kufanya hilo litokee. Hapo chini unakwenda kujifunza rasilimali hizo na jinsi ya kuzitumia ili upate mafanikio na utajiri unaotaka.
2. Rasilimali Pesa.
Unapoanzia chini, unaweza kuingiza kipato kwa nguvu na muda wako. Hapo unakuwa huhitaji pesa ili kupata pesa. Lakini hilo litaenda mpaka kufika hatua fulani na huwezi tena kuvuka hapo hata uweke muda na nguvu kiasi gani.
Watu wengi wanaoanzia chini na kutumia nguvu na muda kuingiza kipato, huwa wanabweteka na kile wanachopata. Wanakizoea na kujikuta wamebaki hapo kwa kipindi kirefu. Kwa sababu huwa kuna mfumuko wa bei na fedha kupungua thamani, watu wanajikuta kila wakati wanapambana sana lakini hawapigi hatua.
Hakuna ubaya wowote kwenye kuanzia hatua ya kutumia nguvu na muda kupata pesa. Lakini ni kujizuia kupata utajiri kama hutaenda zaidi ya hapo.
Utajiri mkubwa huwa hautengenezwi kwa nguvu na muda wako, bali unatengenezwa kwa nguvu ya pesa na muda ambao pesa hiyo imewekwa kwenye kujenga utajiri huo.
Ili kujenga utajiri mkubwa, ni lazima pesa itumike kuzalisha pesa. Pesa inapaswa kuwekezwa kwenye maeneo ambayo yanazalisha thamani, faida na kuongezeka. Hapo ndipo ukomo wa nguvu na muda wa mtu unapoondoka.
Wengi wanaposikia pesa inahitajika ili kupata pesa zaidi, wanajiona wao wameshindwa kwa sababu hawana pesa. Lakini ukweli ni kinachohitajika ni pesa, bila kujali pesa ni ya nani.
Unaweza kutumia pesa zako na ukajenga utajiri bila kutegemea muda na nguvu zako. Lakini lazima uelewe pesa inapokuwa kidogo ndivyo utajiri nao unakuwa mdogo.
Lakini habari njema ni unaweza kutumia pesa za watu wengine kujenga utajiri mkubwa kwako. Na hapa hata siyo kwamba unawaibia, bali unatengeneza mazingira ambayo unaweza kutumia pesa za wengine na kujenga utajiri wako.
Chukua mfano wa kukopa fedha benki na kujenga nyumba ya wapangaji, ambapo kodi wanayolipa ndiyo marejesho ya mkopo huo. Baada ya muda unakuwa umekamilisha kulipa mkopo na nyumba ikiwa mali yako inayoendelea kukuingizia kipato na yenye thamani pia. Huu ni mfano, kuna mengi ya kuzingatia mpaka hilo litokee.
Kitu muhimu cha kutoka nacho hapa ni usitegemee tu pesa zako mwenyewe, badala yake tafuta fursa za kutumia pesa za wengine kujijengea utajiri mkubwa.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK137; Tumia Rasilimali Hizi Kutenganisha Muda Wako Na Pesa Zako Ili Kujenga Utajiri Usio Na Ukomo