Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kwa zama hizi ambapo kumekuwa na changamoto kubwa ya ajira, kufanya biashara na ujasiriamali imeonekana kama ndiyo suluhisho. Watu waliokaa kwenye mfumo wa elimu kwa karibu miaka 20, wakifundishwa kuwa wataalamu kwenye maeneo mbalimbali, wanapohitimu wanaambiwa wakafanye biashara.

Hakuna ubaya wowote kwenye hilo, na kwa hakika ni jambo zuri sana. Lakini tatizo ni watu kudhani kwa sababu tu kila mtu anaweza kufanya biashara, basi pia kila mtu anaweza kufanikiwa kwenye biashara.

Watu hawataruhusu mtu ajiite mhasibu kama hajasomea, au daktari kama hajasomea, au mwanasheria. Taaluma hizo, na nyingine nyingi zinataka watu wakae darasani kwa miaka mingi ndiyo waweze kufuzu. Lakini mtu anaweza tu kuamka siku moja na kujiita mjasiriamali au mfanyabiashara na kila mtu akakubaliana na hilo.

Kuingia kwenye biashara na ujasiriamali kumerahisishwa sana, kiasi cha watu kutokuweka uzito kwenye kujifunza eneo hili kama wanavyojifunza kwenye maeneo mengine. Na hiyo ndiyo sababu kwa nini watu wengi wanaoingia kwenye biashara wanaishia kushindwa au kutokupata ukuaji na mafanikio makubwa.

Watu wengi wanapoangalia biashara, wanaona ni kama kitu kimoja, lakini kwa uhalisia, biashara ni mkusanyiko wa ujuzi wa aina mbalimbali, ambao kwa pamoja ndiyo unaleta matokeo yanayohitajika.

Mafanikio au kushindwa kwa biashara kunategemea jinsi ujuzi wote unaohitajika unavyokuwa umejengwa au kutokujengwa ndani ya biashara.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia ujuzi ambao umekuwa unakosekana kwenye biashara nyingi na kupelekea biashara hizo kushindwa au kutokupata ukuaji mkubwa.

1. Biashara Ni Chombo Cha Kutengeneza Fedha.

Matatizo mengi ya biashara yanaanzia pale mwanzilishi au mmiliki wa biashara anaposhindwa kujitofautisha yeye na biashara yake. Watu wengi hawajui mpaka kati yao na biashara zao uko wapi. Wao ndiyo wanakuwa biashara na biashara zinakuwa wao. Kwa kushindwa kuweka huu mpaka wa msingi kabisa, watu wamekuwa wanajikuta kwenye ajira ya kikatili wanayoiita biashara.

Ukiwa na gari, siyo lazima uliendeshe wewe ndiyo liweze kufanya kazi. Mtu yeyote anayejua kuendesha gari, anaweza kuendesha gari lako na matokeo yakawa sawa na wewe kuliendesha. Lakini wengi wakiwa na biashara, hakuna mtu mwingine anayeweza kuiendesha isipokuwa wao. Hata kama mtu ni mzoefu kwenye kuendesha biashara, akiingia kwenye biashara ya mtu mwingine hawezi kuleta matokeo kama ambayo aliyeianzisha amekuwa anayapata.

Kitu kikubwa na muhimu sana ambacho kila aliye kwenye biashara anapaswa kujua ni kwamba biashara ni chombo cha kuingiza fedha. Neno la msingi hapo ni chombo, na chombo kinaweza kutumiwa na mtu yeyote.

Hiki ni kitu ambacho watu wanatakiwa kukijua kabla hata hawajaingia kwenye biashara, ili kila wanachofanya kwenye biashara hizo kiweze kuendana na hiyo dhana ya chombo. Tangu awali wahakikishe wanafanya mambo kwa namna ambayo hawazifanyi biashara kuwategemea wao kwa kila kitu.

Uzuri ni kwamba, watu wanapokuwa wanasomea taaluma mbalimbali, wanafundishwa kabisa jinsi ya kutekeleza majukumu yao, bila ya majukumu hayo kuwategemea wao. Hakuna daktari anayefundishwa kwamba asipokuwepo wagonjwa hawawezi kutibiwa, hata kama ameanza kuwatibu yeye. Hakuna mwanasheria anayefundishwa kwamba asipokuwepo kesi alizoanza nazo haziwezi kuendelea. Au mwalimu akafundishwa akianza kumfundisha mtoto darasa la kwanza, lazima yeye ndiyo aende naye mpaka anamaliza darasa la saba.

Kila taaluma inawaandaa watu wake kuweza kutekeleza majukumu yao kwa namna ambayo hayawategemei wao ndiyo yaende. Kila mwanataaluma anajua mchakato wa kutekeleza majukumu yake, ambapo hata asipokuwepo, mtu mwingine akija anaendelea pale alipoishia.

Lakini inapokuja kwenye biashara, wengi wanafanya kinyume na hilo. Wanaendesha biashara zao kwa namna ambayo wasipokuwepo, hakuna kinachoweza kwenda. Na hapo ndipo anguko la biashara linapoanzia, na pia biashara kushindwa kupata ukuaji mkubwa ambao unawezekana.

2. Fedha Inapatikana Kwa Kutoa Thamani.

Namna watu wanavyoingia kwenye biashara nalo ni tatizo jingine kubwa. Wengi wamekuwa wanaangalia biashara zilizopo na wao kuiga hizo hizo. Wanapoona kuna biashara ambayo ni rahisi kufanya na yenye wateja wengi, wanaona hapo ndipo pa wao kuingia pia.

Hakuna ubaya wowote kwenye kuiga biashara zinazofanya vizuri, lakini kuiga kwa nje ndiyo tatizo kubwa. Kuiga kwa kuangalia tu nje ndiyo kumepelekea biashara nyingi kuwa na ushindani usio wa afya, ambapo watu wanashindana kwa kupunguza bei.

Msingi wa kwanza wa biashara unapaswa kuwa ni kutoa thamani. Biashara inapaswa kutoa thamani kwa watu ambao wanaihitaji, kisha watu hao kuwa tayari kutoa fedha walizonazo ili wapate thamani hiyo.

Wengi wanapoiga biashara kwa kuangalia kwa nje, wanaweza kuona ni bidhaa au huduma fulani inayouzwa, lakini kama hawaelewi ni thamani gani inayotolewa, hawawezi kujenga biashara imara.

Kuna watu wamekuwa wanaingia kwenye biashara, halafu wanaanza kuwalaumu watu wao wa karibu kwa nini hawanunui kwao. Wanawaona watu hao wa karibu kama wasaliti ambao hawataki maendeleo yao.

Kitu kimoja ambacho kila mtu anapaswa kujua ni kwamba, kwa asili, sisi binadamu ni wabinafsi. Tunafanya jambo pale ambapo tuna nafasi ya kunufaika. Kama haina manufaa au maslahi kwetu, hatufanyi.

Ukiona unauza kitu na watu wanaenda kukinunua kwa wengine, jua kuna thamani wanaipata kule na kwako hawaipati. Hata kama bei ni moja, au wewe unauza pungufu zaidi, kama hawanunui kuna thamani hawapati.

Kukimbilia kupunguza bei imekuwa ndiyo njia ya kivivu ya wengi kutaka kufanikiwa kwenye biashara. Lakini ni njia ya matatizo na kupotea, kwa sababu kila mtu anaweza kuitumia.

Kutoa thamani kubwa, ambayo inawavutia watu na kuwafanya wabaki kwa muda mrefu ndiyo mkakati sahihi wa kujenga biashara yenye ukuaji mkubwa. Hicho ni kitu ambacho kila mtu aliyepo kwenye biashara anapaswa kukijua vizuri.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK136; Kukosekana Kwa Huu Ujuzi Kumezuia Biashara Nyingi Kupata Ukuaji Mkubwa