Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Watu wengi wamekuwa hawaelewi pale wanaposikia kwamba mafanikio makubwa yanahitaji juhudi kubwa sana. Wengi wanashindwa kuelewa hilo pale wanapowaangalia watu ambao hawajafanikiwa wakiwa ndiyo wanaoweka juhudi kubwa zaidi.
Ukienda kwenye eneo lolote, utawakuta watu wa chini wakiwa ndiyo wanafanya kazi sana kuliko watu wa juu. Wale wanaofanya kazi ngumu, kwa kutumia nguvu kubwa na muda mwingi, ndiyo pia wanaokuwa wanalipwa kidogo.
Wale wanaolipwa sana, huwa wanaonekana kama hakuna kazi kubwa na ngumu wanayofanya. Wanaonekana kufanya mambo machache na kupata mafanikio makubwa.
Ni kutokuoana huku kwa juhudi na matokeo ndiyo kumepelekea watu wengi kuamini kuna siri za mafanikio ambazo zimefichwa kwa wengi na zinazojulikana na wachache waliofanikiwa. Ni vigumu sana watu kuamini kwamba juhudi ndiyo zinazoleta mafanikio.
Lakini huo ndiyo ukweli, juhudi ndiyo zinazoleta mafanikio. Lakini pia ni kweli kwamba siyo kila aina ya juhudi inaweza kukupa mafanikio makubwa unayoyataka. Unapokuwa unataka mafanikio makubwa, lazima ujue aina ya juhudi zitakazoleta mafanikio hayo.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia aina hiyo ya juhudi ambazo zikiwekwa zitaweza kukufikisha kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Juhudi Kubwa Zinaleta Matokeo Ya Kawaida
Kama kuna kitu ambacho kimewapoteza watu wengi kwenye mafanikio ni kuiga yale ambayo yanafanywa na watu waliofanikiwa. Kwa sababu maisha ya watu waliofanikiwa yanaandikwa sana, utaratibu wao wote wa maisha ukielezwa, watu wamekuwa wanaiga yale wanayofanya ili na wao wafanikiwe.
Watu wanakazana sana kuweka juhudi kubwa kama ambavyo waliofanikiwa wanaonekana kuweka. Lakini bado hao wanaoiga juhudi hizo kubwa hawapati matokeo makubwa, badala yake wanaishia kupata matokeo ya kawaida. Hilo linatokea kwa sababu kinachoonekana kwa nje siyo hasa kilicho ndani.
Unapoiga moja kwa moja yale ambayo watu wanafanya, hutaweza kupata matokeo makubwa na ya kipekee kama ambayo wao wanapata. Badala yake unaishia kupata matokeo ya kawaida, ambayo kila anayeiga anayapata.
Matokeo makubwa na ya kipekee yanatokana na ufanyaji wa kipekee pia. Yanatokana na juhudi ambazo ni za kipekee sana, ambazo ni kubwa, na kwenye kitu cha kipekee ambacho mtu anacho.
Kingine kinachowapoteza watu kwenye kuweka juhudi ni kushindwa kuchagua maeneo ya kupuuza na ya kuwekea mkazo. Unapowasikiliza waliofanikiwa, utaona maeneo mengi yakiwa muhimu kufanyiwa kazi. Lakini mtu akifanyia kazi maeneo mengi, hawezi kupata matokeo makubwa.
Unapowaangalia watu wote waliofanikiwa, kuna maeneo machache sana ambayo wanayafanya kwa ukubwa na upekee. Na wana maeneo mengi ambayo wameyapuuza. Matokeo makubwa wanayoyapata kwenye maeneo machache wanayoyapa uzito yanafukia udhaifu unaotokana na maeneo ambayo wameyapuuza.
Mafanikio makubwa hayatokani na juhudi kubwa tu, bali yanatokana na juhudi za kipekee, ambazo ni juhudi kubwa zinazowekwa kwenye maeneo machache ya msingi na yanayoleta matokeo ya kipekee.
Usikimbilie tu kuiga juhudi kubwa ambazo watu wanaweka, jua maeneo yako ya kipekee ambayo ndiyo utayapa juhudi hizo kubwa na kuwa tayari kupuuza mengine ambayo yataonekana ni udhaifu. Lakini uzuri ni ukishafanikiwa kwenye maeneo machache ya kipekee, utayafunika maeneo ambayo umekuwa na udhaifu.
2. Kazana Kwa Moyo Wako Wote
Watu ambao wanaiga juhudi kubwa za wengine, na ambao wanajisifia kwa juhudi kubwa wanazoweka, huwa wanafanya kama maonyesho tu. Yaani ni kama wanafanya ili waonekane wamefanya, kama kuondoa lawama, wasionekane ni wavivu na wazembe.
Wengi wanafanya kama sehemu ya kukamilisha ratiba au majukumu waliyopanga. Wanachokazana nacho zaidi ni kukamilisha kufanya na siyo namna wanavyofanya au matokeo wanayopata. Hilo limepelekea matokeo kuwa ya kawaida licha ya juhudi kubwa ambazo watu wanaonekana kuweka.
Juhudi za kipekee, ambazo zinachangia mafanikio makubwa ni ambazo mtu ameziweka kwa moyo wake wote. Mtu anafanya kweli kutoka ndani ya moyo wake, anaweka kila kilicho ndani yake.
Kwa njia hii, mtu hafanyi ili kukamilisha au kuonekana amefanya, bali anafanya ili kuleta matokeo ya tofauti. Anafanya kile kinachohitajika kufanyika ili matokeo yapatikane na siyo kufanya kile anachojisikia kufanya.
Watu wanapopata matokeo ya kawaida huwa tayari kulalamika kwamba wanajitahidi sana ila hawapati matokeo. Na ni watu hao wanaolalamika hawapati matokeo ndiyo ambao hawafanyi kwa moyo wao wote.
Wale wanaofanya kwa moyo wao wote huwezi kuwakuta wakilalamika kutokupata matokeo. Badala yake unawakuta wakiwa wametingwa na kufanya kile kinachopaswa kufanyika ili matokeo yapatikane.
Ni rahisi kuwaonea huruma wale wanaopiga kelele za malalamiko ya kutokupata matokeo. Lakini ni hizo kelele ndiyo zinapaswa kukuambia kwa nini watu hao hawapati matokeo.
Watu waliojitoa kweli kufanikiwa, walio tayari kufanya kila kinachopaswa kufanyika ili wafanikiwe, hawawezi kuwa na muda wa kupiga kelele za kwamba wameweka juhudi ila hawajapata matokeo. Jitafakari sana pale unapokuwa unalalamika au kulaumu kutokupata matokeo, ni kiashiria cha kwamba hujajitoa kweli kuyapata matokeo hayo.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK135; Juhudi Kubwa Pekee Hazitoshi Kukupa Mafanikio Makubwa