Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinanishangaza sana kwa watu kwenye kuwapa elimu ya fedha ni kukosa subira. Unamwelimisha mtu kuhusu manufaa ya uwekezaji, anakuwa mbishi kuelewa, lakini kwa msisitizo, anaelewa na kuwekeza.
Lakini sasa, anapowekeza, anakuwa anaangalia mwenendo wa uwekezaji huo kila siku. Anapoona hakuna ukuaji wa siku hadi siku, au mbaya zaidi akiona baadhi ya siku uwekezaji huo umeshuka, anapata taharuki na kuona anapoteza.
Kukosa huko subira kumewakwamisha sana watu wengi, siyo tu kwenye uwekezaji, bali kwenye kila eneo la maisha. Fikiria mtu anayepanga kupunguza uzito wa mwili wake, anajifunza kuhusu ulaji sahihi na mazoezi. Anafanya hivyo na mwanzo anaona akipungua, lakini baada ya muda haoni tena akipungua, licha ya kufuata ulaji na mazoezi, hapo anakosa subira na kuacha.
Kadhalika kwenye biashara, mtu anaona fursa ya kuuza kitu ambacho anaona kina uhitaji. Lakini anapokuwa na kitu hicho na kuwashawishi watu kununua, wanakuwa hawapo tayari. Kwa kukosa subira mtu anaona kitu hicho hakina soko na kuacha kukiuza.
Pamoja na kila mtu kujua kwamba mafanikio yanahitaji muda ndiyo yaweze kutokea, bado watu wengi sana wamekuwa wanashindwa kuweka muda huo. Wengi wanakata tamaa na kuacha kwa sababu moja, wanakutana na kushindwa na kushindwa kunauma.
Ni lazima tuwe wa kweli, sisi binadamu hatupendi hali ya kushindwa. Kushindwa ni kitu tunachokiona ni kibaya na cha hatari. Hivyo inapotokea tumeshindwa, inakuwa vigumu sana kwetu kuendelea na kitu hicho.
Kwa bahati mbaya, hakuna mafanikio makubwa yanayopatikana bila kupitia kushindwa. Hivyo kama hatutakuwa na mkakati madhubuti wa kuvuka hali hiyo ya kushindwa, hatutaweza kupata mafanikio makubwa tunayoyataka.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unaenda kujifunza namna bora ya kuchukulia kushindwa ili kusikukwamishe kufanikiwa. Badala ya kuangalia tukio moja la kushindwa, unaenda kujifunza kuangalia wastani wa hatua zote unazokuwa umechukua.

1. Kushindwa Ni Kwingi Kuliko Kushinda.
Ukiangalia hatua nyingi ambazo tunachukua kwenye maisha, zinazofanikiwa na kuleta matokeo ni chache kuliko zisizoleta matokeo. Ukiangalia mambo mengi ambayo miili yetu inafanya, yanayochangia kwenye uhai ni machache mno.
Hicho ni kitu kikubwa na muhimu sana ambacho watu wengi wamekuwa hawajui kuhusu asili. Asili imeweka uwezo mkubwa kwenye kila kitu, kuliko unavyohitajika, kwa sababu kushindwa ni kwingi kuliko kushinda.
Simba, pamoja na ukali na nguvu zake, ana wastani wa asilimia 25 kwenye kukamata wanyama anaowawinda. Yaani kwa kila wanyama 4 ambao anawakimbiza, anafanikiwa kumkamata mmoja tu. Lakini simba huwa hawafi njaa, wanapata chakula chao na maisha yanaendelea.
Fikiria kama simba angemkimbiza swala wa kwanza akamkosa, akajaribu wa pili pia akamkosa na akaamua kwamba hana tena uwezo wa kukamata swala. Simba anayechukulia mambo hivyo atakufa njaa. Lakini simba wanajua, kushindwa kumkamata swala siyo mwisho wa kuwinda. Kuwinda kunaendelea mpaka pale swala anapokamatwa.
Sitaki kuamini kama simba wana akili ya kujua hilo la msingi kuhusu maisha kuliko sisi binadamu. Nadhani akili nyingi tulizonazo kuna wakati zinatufanya tusahau kabisa mambo haya ya msingi.
2. Acha Kuchukulia Kila Hali Kama Ya Kufa Na Kupona.
Kwa kipindi kirefu sana binadamu waliishi kwenye mazingira hatari sana hapa duniani. Usalama ulikuwa mdogo na hatari za kupoteza uhai zilikuwa nyingi. Hali hiyo ilifanya kushindwa kukachukuliwa kama hali ya kufa na kupona. Katika kipindi ambacho binadamu waliishi karibu na wanyama wakali, kukataliwa kwenye kundi ilimaanisha kifo. Kushindwa kuchukua hatua kwenye hatari ilimaanisha mwisho wa maisha.
Hali hiyo ya kuchukulia kushindwa kama hali ya kufa na kupona bado tumebaki nayo, licha ya kuwa kwenye mazingira ambayo ni salama. Kwa mazingira ya sasa, hata mtu akikataliwa, bado anaweza kuendesha maisha yake. Hata mtu akishindwa kuchukua hatua kwenye mambo yanayoonekana ni hatari, bado anakuwa na nafasi ya kufanya vizuri zaidi.
Kuna mambo machache sana ambayo yana hali ya kufa na kupona kweli. Lakini kwa mazoea yetu binadamu, bado tumekuwa tunachukulia kila kushindwa na kila kikwazo kama ndiyo mwisho kabisa wa safari au maisha. Na hilo ndiyo limefanya watu wengi kuacha kuchukua hatua baada ya kushindwa.
Unapaswa kujipa wajibu wa kuendelea kuchukua hatua bila ukomo. Kwa kila unachofanya, unapaswa kuendelea kufanya, bila kujali umepata matokeo gani. Matokeo yoyote yasikufanye uone umefika mwisho wa safari. Kila matokeo ni mwanzo wa safari nyingine.
Endeles kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK134; Kuepuka Kukata Tamaa, Angalia Wastani Badala Ya Tukio Moja Moja