Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Unapoenda kwenye eneo lolote, unakuta katika watu wengi wanaofanya kitu, ni wachache sana wanaokuwa wamepata mafanikio makubwa. Wengi wanakuwa kwenye hali ya chini na ya kawaida sana.
Wachache pekee kufanikiwa haimaanishi kwamba mafanikio yanawezekana kwa wachache tu. Mafanikio yanawezekana kwa kila mtu ambaye anakuwa amedhamiria kweli kufanikiwa.
Kinachowakwamisha wengi kupata mafanikio makubwa wanayoyataka ni kushindwa kudumu kwenye mchakato unaowapeleka kwenye mafanikio. Kwa kuwa mafanikio huwa yanachelewa, na watu wanataka mambo ya haraka, wengi wamekuwa wanaacha mchakato wakati ambao wameshakaribia kabisa kupata ushindi.
Kazi yangu mimi ni ushindi wako. Nimejitoa kuhakikisha unafanikiwa. Ninaamini, bila ya shaka yoyote kwamba wewe unaweza kupata mafanikio makubwa zaidi ya hapo ulipo sasa. Na pia najua kuna maeneo ambayo umekuwa unajikwamisha, kwa kuacha kufanya unayojua unapaswa kufanya kwa sababu matokeo unayokuwa unatarajia yanachelewa.
Ndiyo maana kwenye hii #BaruaYaKocha naenda kukushirikisha mambo unayopaswa kufanya ili uweze kudumu kwenye mchakato wako wa mafanikio, hata kama matokeo yanachelewa. Karibu ujifunze ili uache kupishana na mafanikio unayostahili kupata.

1. Usife.
Unaweza kurekebisha makosa yote unayofanya kwenye maisha yako, kasoro kufa. Na hapa kufa sizungumzii tu kufa kimaisha, bali pia kufa kimchakato.
Kutokufa kimaisha ni kuhakikisha unaendelea kuwa hai ili uendelee kuweka juhudi kwenye mchakato wako wa mafanikio. Kwa sababu kadiri unavyoweka juhudi kwa muda mrefu, ndivyo unavyokusanya nguvu ya kupata mafanikio makubwa.
Kutokufa kimchakato ni kuhakikisha unaendelea kubaki kwenye mchakato wako kwa muda mrefu zaidi. Hiyo ni kuhakikisha hufanyi jambo lolote ambalo linakuondoa kabisa kwenye kile unachofanya.
Kama ni biashara, unahakikisha hufanyi mambo ambayo yanapelekea biashara hiyo kufa. Kwa sababu, hata kama hupati matokeo, kuendelea kuwepo kwenye biashara kunakupa nafasi ya kupata matokeo. Ukifanya maamuzi ambayo yatapelekea biashara kufa, unaua kabisa nafasi zote za kuweza kupata mafanikio baadaye.
Charlie Munger alikuwa na mwongozo wake unaosema; Nachotaka kujua ni wapi nikienda nitakufa na nisiende hapo. Unachopaswa kujua ni mambo gani ukiyafanya yatakuondoa kabisa kwenye mchakato na kuepuka kuyafanya hayo.
Wajibu wako mkubwa ni kuhakikisha unaendelea kubaki kwenye mchakato na kupambania ushindi wako. Kusiwepo na kitu chochote ambacho kinakuondoa kwenye mchakato huo.
2. Usikate Tamaa
Tofauti na picha inayoonyeshwa kwenye mitandao ya kijamii na habari mbalimbali za mafanikio, mafanikio makubwa huwa yanahitaji muda mrefu mpaka yatokee. Mitandao ya kijamii na vyombo vya habari huwa vinapenda kuonyesha mafanikio yanayotokea haraka.
Lakini mara nyingi kitu kinakuwa kimefanyika kwa muda mrefu bila kujulikana mpaka kinapokuja kuleta mafanikio. Na hata kwa vile ambavyo kweli vimepata mafanikio makubwa na kwa haraka, huwa vinaishia kupata anguko kubwa pia.
Hivyo basi, pamoja na kutokufa, hupaswi kukata tamaa kwa sababu yoyote ile. Unapochagua mafanikio unayotaka kuyapata na kujua unachopaswa kufanya ili kuyapata, wajibu wako ni kufanya bila kukata tamaa.
Hata kama unaweka juhudi kubwa na huoni matokeo, endelea bila kukata tamaa. Hata kama unaona kwa wengine mambo ni rahisi zaidi, usiache kufanya kile ambacho umechagua kikupeleke kwenye mafanikio unayoyataka.
Hata kama ni kweli kwamba unaweza kupata mafanikio kwa urahisi zaidi kwenye kitu kingine, bado hutaridhika na mafanikio hayo kama siyo kitu ulichokuwa unakitaka hasa.
Kaa kwenye kile ulichochagua bila kukata tamaa na kuacha. Endelea kufanya na kujifunza kuboresha maeneo yanayohitaji maboresho ili uweze kupata mafanikio.
Mara nyingi watu huwa wanakata tamaa wakiwa wameshafika karibu sana na mafanikio makubwa wanayoyataka. Halafu wanaenda kuanza vitu vingine ambavyo pia vinahitaji muda mrefu mpaka vilete mafanikio.
Unaweza kuona kama kwenda kwenye kitu kingine ni kuharakisha mafanikio, lakini matokeo yake huwa ni kuyachelewesha mafanikio zaidi. Kwa sababu unaenda kuanza kitu kipya, ambapo utahitaji muda wa kujifunza kitu hicho kabla hakijaweza kukupa matokeo.
Pamoja na kutokukata tamaa, hupaswi kuendelea kufanya mambo yale yale, kwa namna ile ile na kutegemea matokeo ya tofauti. Ni lazima uendelee kujitathmini na kuboresha kadiri unavyoendelea ili uweze kupata matokeo unayoyataka.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK133; Fanya Haya Uweze Kudumu Kwenye Mchakato Hata Kama Mafanikio Yanachelewa