Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Fanya unachopenda na utafanikiwa ni ushauri maarufu sana kwenye tasnia ya mafanikio. Licha ya ushauri huo kuwa rahisi kueleweka, wengi hawajaweza kuutumia kupata mafanikio makubwa wanayoyataka.

Wengi kutokufanikiwa kwa ushauri huu haimaanishi ni ushauri mbaya au usiofanya kazi. Bali inamaanisha kuna kitu ambacho watu wanakuwa hawajakielewa vizuri kwenye huo ushauri.

Watu wanaweza kukuambia ni nini wanapenda kufanya na wakawa wanafanya. Pamoja na kufanya, bado wakawa hawapati mafanikio makubwa. Wakikueleza jinsi wanavyofanya wanachopenda na hawafanikiwi, unaweza kuwaonea huruma na kudhani wana bahati mbaya.

Lakini ukipata muda wa kuwaangalia kwa umakini wakiwa wanafanya hicho wanachosema wanapenda kufanya, unapata majibu kwa wazi kabisa kwa nini hawafanikiwi. Jinsi watu wanavyokuwa wanafanya wanachosema wanapenda kufanya, inakuonyesha wazi kama watafanikiwa au la.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia zaidi ya kufanya unachopenda. Hapa tutaangalia namna ya kufanya unachopenda ili uweze kupata matokeo unayoyataka.

1. Una Motisha Sahihi?

Novak Djokovic ni mmoja wa wacheza tenisi bora kuwahi kuwepo hapa duniani. Kwa miaka mingi ameweza kuwa kwenye kilele cha ubora bila kushuka. Alipoulizwa nini kimekuwa kinamsukuma kuendelea kufanya kwa ubora na kubaki kileleni alijibu; “Nimeweza kubaki kwenye kilele cha mafanikio kwa sababu napenda kuupiga mpira wa tenisi.”

Alipoulizwa kama kuna wachezaji ambao hawapendi kupiga mpira, alijibu;

“Kuna watu wengi wako kwenye huu mchezo lakini hawana motisha sahihi. Naweza kuona. Lakini sihukumu.”

Hayo ni majibu mafupi, lakini yaliyobeba maana kubwa sana kwenye safari ya mafanikio makubwa.

Anachosema Novak kinahusika sana kwenye safari ya mafanikio makubwa. Ni kweli kwamba ili mtu ufanikiwe, lazima ufanye unachopenda (au upende unachofanya).

Lakini wengi wamekuwa hawana motisha sahihi kwenye kitu wanachofanya. Wanasema wanakipenda, lakini hawakipendi kitu hicho, bali wanayapenda matokeo wanayotegemea kupata.

Kwa sababu mapenzi yao yapo kwenye matokeo, ufanyaji wao unakuwa siyo kwa viwango ambavyo vinaweza kuwapa matokeo wanayokuwa wanayataka.

Na pia kwa sababu matokeo huwa yanachelewa, wengi hukosa uvumilivu na kuacha kufanya pale matokeo yanapochelewa.

Na hata kwa wanaoweza kuvumilia mpaka wakayapata matokeo, wanaacha kufanya na hilo kuwapelekea kushindwa kubaki kwenye kilele cha mafanikio.

Anachokisema Novak, ndiyo ambacho nimekuwa nakiona kwenye mafanikio. Watu wengi hawafanikiwi kwa sababu wanayapenda mafanikio na siyo kile cha msingi kinachowapa mafanikio.

Watu wengi hawapendi kupiga mpira wa mafanikio yao. Hawapendi kufanya kile cha msingi kabisa ambacho ndiyo kinawapa mafanikio. Watahangaika na mambo mengi, lakini lile la msingi ambalo linabeba mafanikio wanayotaka, hawatalipa umakini wa kutosha.

Kwenye barua hii unaenda kujifunza namna ya kuweka motisha wako kwa usahihi ili uweze kupata mafanikio makubwa unayoyataka.

2. Fanya Kwa Sababu Ya Mapenzi Na Siyo Matokeo.

Watu wamekuwa wanalalamika pale mahusiano yanapovunjika kwa sababu ya hali ya mmoja kubadilika. Labda mtu alikuwa na wadhifa fulani, ambao akiupoteza anapoteza na watu wake wa karibu. Au alikuwa na hali nzuri ya kifedha, na anapokuwa kwenye hali mbaya, anapoteza watu wake wa karibu.

Wengi huona kama hakuna marafiki au mahusiano ya kweli, kwamba watu wengi wapo kimaslahi, wakiangalia ni nini wanachopata. Hilo lina ukweli, kwa sehemu kubwa watu wanakaa mahali ambapo wanapata kile wanachotaka.

Na hivyo ndivyo watu wamekuwa wanajifanyia wao wenyewe. Watu wengi hawana mahusiano ya kweli na mafanikio yao. Wanayapenda mafanikio kwa kuangalia matokeo watakayopata baada ya kufanikiwa. Lakini hawaangalii yale wanayopaswa kufanya ndiyo waweze kupata hayo mafanikio wanayoyataka.

Watu wanasema wanataka mafanikio fulani, na kufanya mambo ambayo yatawapa mafanikio hayo. Lakini hawadumu kwenye kufanya mambo hayo, wanabadilika haraka sana pale matokeo wanayoyataka yanapochelewa.

Usikae kimaslahi kwenye mafanikio yako mwenyewe, kwa kufanya ukivizia matokeo na kuacha pale matokeo yanapochelewa. Ukishajua unachotaka na unachopaswa kufanya ili kukipata, kinachofuata ni kufanya bila kuyumbishwa na chochote.

Wanasema ukipenda boga, penda na ua lake. Ukipenda mafanikio, unapaswa kupenda na yote yanayoambatana na mafanikio. Ikiwepo kupenda unachopaswa kufanya ili ufanikiwe, kupenda muda wa kusubiri mpaka uyapate mafanikio yenyewe na mengine mengi yanayoambatana na hilo.

Ukipenda kile unachofanya na ukawa tayari kuendelea kukifanya licha ya matokeo unayokuwa unayapata, unakuwa kwenye njia nzuri ya kupata mafanikio makubwa unayoyataka. Hivyo ndivyo unavyopaswa kwenda na dhana ya kupenda unachofanya ili ufanikiwe, siyo kupenda mafanikio unayotarajia kupata pekee, bali kupenda kwa uhakika kile unachopaswa kufanya.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK132; Kupenda Unachofanya Haitoshi, Unapaswa Kukifanya Kwa Namna Hii