Rafiki yangu Mpendwa,
Kujenga mafanikio makubwa kwenye maisha ni mapambano makubwa. Ni sawa na vita ambayo inakutaka wewe upambane sana ndiyo uweze kupata ushindi.
Hiyo ni kwa sababu mafanikio makubwa siyo kitu cha kawaida, siyo kitu kilichozoeleka au kinachoweza kupatikana kirahisi.
Pamoja na ugumu huo wa mafanikio makubwa, bado ni kitu kinachoweza kupatikana kwa yeyote anayetaka hasa na kujitoa. Yeyote anayekuwa tayari kuweka mapambano yanayohitajika, anaweza kuyapata mafanikio hayo makubwa.
Tatizo ambalo limekuwa linawakwamisha watu wasipate mafanikio hayo makubwa ni kuhangaika na mambo ambayo hayana mchango kwenye mafanikio wanayokuwa wanayataka.
Badala ya watu kuweka mapambano yanayohitajika, wanapoteza muda na nguvu kwenye mambo ambayo wangepaswa kuachana nayo kabisa. Ubaya wa mambo hayo yanayowahamisha watu kutoka kwenye mapambano nayo yanaonekana kama mapambano. Kumbe ni usumbufu tu unaowakwamisha watu kuweka mapambano halisi yanayohitajika.
Kwenye hii #BaruaYaKocha unakwenda kujifunza mambo unayopaswa kuachana nayo kabisa kwenye safari yako ya kujenga mafanikio makubwa. Mambo hayo yanaweza kukutamanisha sana kufanya, lakini hayana tija wala mchango kwenye mafanikio makubwa unayoyataka.

1. Usiingie Kwenye Kila Pambano
Mafanikio makubwa ni mapambano, lakini huwezi kuwa unapambania kila kitu. Mapambano ni makubwa na yanataka rasilimali nyingi ili kuweza kupata ushindi unaotaka. Hivyo unapaswa kuwa na pambano moja tu ambalo unalipa rasilimali zote ulizonazo. Pambano moja ambalo unaposhinda, unapata mafanikio makubwa unayoyataka.
Unapochagua pambano lako, siyo kwamba dunia itakuacha ubaki na hilo tu, badala yake itakuletea mapambano mengine unayoweza kuona ni muhimu uingie. Na huo ndiyo mtego ambao wengi wamenasa na kushindwa kupata mafanikio makubwa wanayokuwa wanayataka.
Ukishachagua pambano lako, huo ndiyo mlima unaochagua kufia ukiwa unayapambania mafanikio makubwa. Mengine yote unapaswa kuachana nayo, kuyapuuza ili yasihamishe rasilimali zako kutoka kwenye pambano kuu.
Kuna vitu vingi utaona havipo sawa na kuona unapaswa kuhakikisha vimekaa sawa, kitu ambacho kinakuondoa kwenye eneo lako kuu. Kuna watu watakushambulia na kuona unapaswa kujibu mapigo, lakini inakuwa haina mchango kwenye mafanikio unayotaka.
Pia kuna fursa nyingi nzuri zitakazojitokeza, ambazo hazipo kwenye eneo ulilochagua, ni lazima uwe tayari kupitwa na fursa hizo ambazo zinaonyesha kuwanufaisha wengi.
Inahitaji ujasiri wa kipekee sana uweze kupuuza watu wanaokusumbua kwenye maeneo ambayo ungeweza kuwajibu. Inahitaji umakini mkubwa kuacha fursa zinazoonekana kuwanufaisha wengi na kubaki kwenye kitu chako kikuu.
Ukishachagua mafanikio makubwa, tambua kila kitu ni mapambano, hata kile kinachoonekana ni kizuri, ni cha kupambania ili usitoke kwenye kitu kikuu ulichochagua.
Unapaswa kupigana vita moja kwa wakati, ili uweze kutumia vizuri rasilimali ulizonazo kupata ushindi mkubwa. Ukianza kutawanya rasilimali hizo kwenye vitu vingi, unapunguza uwezekano wako wa kupata mafanikio makubwa unayoyataka.
Chagua pambano lako kuu moja na achana na mengine yote. Pambana mpaka upate ushindi kwenye pambano lako kuu kisha unaweza kwenda kwenye mapambano mengine unayoyataka.
Kama hujapata mafanikio makubwa kwenye kile unachotaka, hupaswi kuhangaika na kitu chochote ambacho hakikupeleki kwenye mafanikio hayo.
2. Usipambane Na Mafanikio Yako Mwenyewe
Umeona watu ambao walianzia chini, wakapambana sana na kufanikiwa, lakini baadaye wakaanguka na kupoteza mafanikio waliyopata.
Hata kwako mwenyewe, ulipokuwa unaanzia chini na huna kitu kabisa, ulikuwa na msukumo mkubwa wa kupambana, lakini unapoanza kupiga hatua, hata kama ni ndogo, msukumo wako unapungua.
Hali hiyo imekuwa inasababishwa na kupambana na mafanikio yako mwenyewe. Unapokuwa unaanza unakuwa na kitu kilicho wazi ambacho unapambania. Unapoanza kupata matokeo, unajikuta ukiwa na vitu vingi vya kupambania, ikiwepo kulinda kile ambacho umeshapata.
Kulinda ambacho umepata, kunahamisha rasilimali nyingi kutoka kwenye kupambania matokeo makubwa zaidi na kupeleka kwenye kulinda matokeo madogo yaliyopatikana. Hilo linageuza mapambano, kutoka kupambana kupata mafanikio na kuwa kupambana na mafanikio unayokuwa umeyapata.
Ugumu unaoanza nao, na nyuma unakokuwa unaanzia kunakupa msukumo wa kupambana sana kupata mafanikio unayotaka. unapopata urahisi na kupiga hatua, kunapunguza msukumo huo na nguvu kupungua kwenye pambano kuu.
Njia ya kuondokana na hili la kupambana na mafanikio yako ni kila wakati kuwa na pambano kubwa kuliko matokeo unayopata. Pale unapopambana na kupata matokeo fulani, boresha kile unachopambania kiwe kikubwa zaidi.
Unapaswa kuhakikisha matokeo yoyote unayopata yanabaki kuwa madogo sana ukilinganisha na yale makubwa unayopambania kufikia. Hapo ndipo unapoweza kuondokana na usumbufu wa kukwamisha na matokeo yako na kupambania mambo ambayo ni makubwa zaidi.
Kadiri unavyopiga hatua, ndivyo unavyopaswa kuongeza mapambano yako ya kupiga hatua zaidi. Unaposhawishika kulinda ushindi ambao umeshaupata, jua njia pekee ya kuulinda ni kupambana kupata ushindi mkubwa zaidi. Kwa kila wakati kuwa kwenye mapambano makubwa, kunaondoa nafasi ya kujikuta ukipambana na mafanikio yako mwenyewe na kuanza kujiangusha.
Jifunze kwa wengine na hata wewe mwenyewe, kila matokeo mazuri yanayopatikana yana tabia ya kuleta kiburi na mazoea. Komesha hilo kwa kuwa na mapambano makubwa kila wakati ili usiwe na kiburi wala mazoea kwenye kitu chochote.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK131; Epuka Mambo Haya Kwenye Mapambano Yako Ya Kufanikiwa