Sikiliza hapa;

Rafiki yangu Mpendwa,

Kipindi cha nyuma nimewahi kuangalia filamu moja ya vichekesho. Kwenye filamu hiyo, mtu alikuwa amenunua TV mpya na kuamua kuitoa TV ya zamani na kuiweka nje ili mtu mwenye uhitaji aichukue. TV ilimaliza siku nzima na hakuna mtu aliyeichukua. Alifikiria sana nini afanye ili TV hiyo iweze kuchukuliwa na akapata wazo.

Siku iliyofuata alibandika karatasi kwenye TV hiyo, ikiwa na maandishi, ‘Inauzwa’ na akaweka bei ya kuuzia. Alipoingia ndani na kutoka nje muda mfupi baadaye, TV ilikuwa imeshachukuliwa na haipo tena.

Japo ni igizo la kuchekesha, lakini kuna somo kubwa sana hapo kuhusu saikolojia yetu sisi binadamu. Kitu kikiwa cha bure au cha thamani ya chini hatukithamini. Ni mpaka kitu kiwe na gharama au thamani kubwa ndiyo tunakithamini.

Na hilo linaenda kwenye kila eneo la maisha yetu, tafiti zinaonyesha hata dawa ya bei kubwa inaponyesha zaidi kuliko ya bei ndogo. Na vitu rahisi kupatikana huwa vinapotea haraka kuliko vinavyopatikana kwa ugumu.

Kwenye mafanikio, hili lipo na limekuwa na athari kubwa. Kanuni na misingi ya mafanikio ipo wazi kabisa kwa kila mtu. Lakini wengi huwa hawatumii kanuni na misingi hiyo inayopatikana bure kabisa. Ila watu hao hao utawakuta wakihangaika kutafuta siri za mafanikio na kuwa tayari kulipa gharama ili kupata siri hizo.

Nimekuwa nakueleza mara nyingi jinsi ambavyo mafanikio hayana siri, ambapo kila kitu kuhusu mafanikio kiko wazi kwa kila mtu. Lakini bado kuna hali ya kibinadamu inaweza kukufanya ushawishike labda kuna vitu bado hujajua kuhusu mafanikio.

Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kukumbushana kuhusu siri isiyo siri ya mafanikio. Tutaangalia msingi mmoja muhimu sana wa mafanikio, ambao tukiusimamia, hakuna kitakachoshindikana kwetu.

1. Siri Isiyo Siri Ya Mafanikio.

Kama kuna msingi mmoja unaoweza kumpa mtu yeyote mafanikio makubwa basi ni huu; “Fanya kwa juhudi kubwa sana sana sana, kwa kipindi kirefu sana sana sana.” Neno la ufunguo hapo ni SANA. Hapo ndipo msisitizo mkubwa unapopaswa kuwekwa.

Kwa nini hii siyo siri? Kwa sababu ndivyo asili inavyofanya mambo yake. Ukiangalia kila kitu kwenye ulimwengu, kinahitaji kazi kubwa na muda mrefu. Hata ukipanda mmea, unahitaji kazi na muda ndiyo uweze kuzalisha kile kinachohitajika. Kadiri kitu kinavyokuwa kikubwa, ndivyo kinavyohitaji kazi kubwa na muda mrefu.

Kwa nini ni siri? Kwa sababu ndivyo watu wanavyopenda kusikia. Ukiwaambia watu una kitu wanachokijua, hawana msukumo wa kukisikia. Lakini ukiwaambia una siri, ghafla wanasukumwa kutaka kujua siri hiyo. Kufanya jambo lililo bayana kuonekana siri ni kuwafanya watu walipe uzito unaostahili.

Kwa kutafakari kwa kina msingi huu wa mafanikio, unaweza kuona ni wapi umekuwa unajikwamisha wewe mwenyewe kufanikiwa. Unachopaswa kufanya ni kujiuliza na kujitafakari kama umeweka juhudi kubwa sana na kwa muda mrefu sana.

Na najua kwa kila mtu mzima aliye hai, ameshaweka juhudi kubwa na muda mrefu, lakini ni kwenye vitu vingi ambavyo havina mchango kwenye mafanikio makubwa anayoyataka.

Juhudi kubwa na muda mrefu unaohitajika ni kwenye kitu kimoja, ambacho mtu umekichagua kujenga mafanikio yako makubwa. Na hapo ndipo msingi huu unapotoa siri yake.

Wakati wengi wanahangaika na mambo mengi, wanaofanikiwa wanahangaika na jambo moja au mambo machache na kuyapa juhudi kubwa na muda mrefu. Kwa mkusanyiko huo wa juhudi na muda, matokeo makubwa na mazuri lazima yapatikane.

2. Weka Juhudi Kubwa Sana, Ambazo Hazijazoeleka.

Ukifanya yale ambayo umekuwa unafanya, utapata matokeo ambayo umekuwa unayapata.

Ukifanya yale ambayo wengine wamekuwa wanafanya, utapata matokeo ambayo wamekuwa wanapata.

Wewe unataka mafanikio makubwa, ambayo hujawahi kuyapata wala wengine hawajawahi kuyapata.

Ni lazima uwe tayari kufanya mambo ya tofauti kabisa na ambavyo umekuwa unafanya na wengine wamekuwa wanafanya.

Mafanikio makubwa yanataka mtu ujue kile hasa unachotaka kupata, kisha kuwa tayari kufanya kila kinachohitajika ili kupata hicho unachotaka.

Siyo kufanya kilicho ndani ya uwezo wako.

Siyo kufanya unachojisikia kufanya.

Ni kufanya kila kinachopaswa kufanywa.

Ukubwa na ugumu wa kinachopaswa kufanya kunategemea ukubwa wa mafanikio ambayo mtu anayataka.

Ni muhimu sana kukumbushana hili kwa sababu kumekuwa na hali ya watu kudanganyika kwamba kuna njia ya mkato ya kupata mafanikio bila kuweka juhudi kubwa.

Teknolojia mpya zinazovumbuliwa kila siku zimekuwa zinaonekana kama njia ya kuondoa hitaji la kuweka juhudi kubwa. Lakini hakuna chochote kinachoweza kuondoa juhudi zinazohitajika kwenye mafanikio makubwa.

Ni lazima mtu aweke juhudi kubwa sana sana sana ndiyo mafanikio makubwa yaweze kupatikana.

Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK130; Siri Isiyo Siri Ya Mafanikio Makubwa