Sikiliza hapa;
Rafiki yangu Mpendwa,
Kwenye tasnia ya mafanikio huwa kuna kauli mbiu maarufu ya ‘fake it, until you make it,’ ikimaanisha; ‘igiza mafanikio mpaka ufanikiwe.’ Kauli hiyo imekuwa na lengo la kuwapa watu hamasa ya kujisukuma kuchukua hatua ili wapate mafanikio.
Japokuwa kisaikolojia kauli hiyo inaweza kutetewa, kwa uwezo wake wa kuifanya akili iyavutie mafanikio, madhara yake kwenye mafanikio ni makubwa kuliko faida.
Kauli hiyo ilichochewa na saikolojia chanya, kwamba mtu anakuwa kile anachohisi, anachofikiri na anachofanya. Hivyo ikaonekana kama mtu atayaigiza mafanikio, basi ataweza kuyavutia mafanikio hayo kwenye uhalisia.
Wapo waliotumia kauli hiyo na wakafanikiwa kweli, lakini kilichowafanya wafanikiwe siyo kauli hiyo, bali namna walivyoyafanya mambo yao.
Na wapo wengi sana ambao wametumia kauli hiyo, wameingia gharama kubwa na hawajapata mafanikio.
Mimi rafiki yako nataka wewe upate mafanikio makubwa na kwa uhakika. Ndiyo maana nimekuwa nakupa njia ambazo najua ukizifanyia kazi, lazima utapata matokeo.
Katika msingi huo huo, nimekuwa nakuepusha na njia ambazo zitakupoteza kimafanikio. Njia ambazo zinatumiwa na wengi, lakini hazina mchango kabisa kwenye mafanikio.
Tatizo kubwa la mafanikio ni hili, kile ambacho kinaonekana kwa nje, mara nyingi sana siyo kilichopo ndani na kinacholeta mafanikio. Mafanikio yanahitaji kitu kikubwa sana kuliko kinachoonekana kwa nje.
Kwenye hii #BaruaYaKocha tunaenda kuangalia madhara ya kauli mbiu ya kuigiza mpaka iwe ili usishawishike kuitumia kwa namna yoyote ile. Na kwa kuwa tunahitaji kauli mbiu, naenda kukupa mbadala wake ambao utakupa mafanikio kwa uhakika.

1. Kila Mtu Anaigiza.
Tatizo kubwa kwenye maisha ni hili, kitu kikishakuwa rahisi, kila mtu anakifanya. Na kitu kikishakuwa kinafanywa na kila mtu, kinakuwa hakina thamani tena.
Kwa zama tulizopo sasa, kila mtu anaigiza. Ndiyo, namaanisha kila mtu, hata mimi na wewe kuna maeneo mengi ambayo tunaigiza.
Maigizo hayawezi kuleta mafanikio makubwa kamwe, kwa sababu hayana uhalisia. Ingia kwenye mitandao ya kijamii na utaona watu wote wana furaha na maisha bora kuliko wewe. Rudi kwenye uhalisia na watu wana maisha magumu, msongo wa mawazo na sonona.
Pale kila mtu anapoigiza, uhalisia unakuwa kitu adimu na chenye thamani kubwa. Hivyo kwa sisi ambao tunapambana kupata mafanikio makubwa na kudumu kwenye mafanikio hayo, hatuna kabisa haja ya kuigiza chochote.
2. Maigizo Yanachosha.
Mafanikio yangekuwa ni kitu chenye uhakika wa wakati wa kuyapata na kudumu kwake, kuigiza mafanikio ingekuwa njia ya uhakika kabisa. Kwa sababu unajua unaigiza kwa muda fulani na ukishafikia mafanikio basi umemaliza.
Lakini uhalisia wa mafanikio ni tofauti kabisa na hilo. Hujui mafanikio yatakuja lini na hata yakija kazi inakuwa haijaisha, bali ndiyo inakuwa imeanza. Kwa kuigiza ili upate mafanikio, utachoka na kushindwa kuendelea.
Utachoka pale mafanikio yanapochukua muda mrefu kuliko unavyotarajia. Na hata ukivumilia mpaka mafanikio yakaja, bado kuyatunza kunahitaji kazi endelevu. Hivyo kama ni kuigiza, inakulazimu mtu uigize kwa maisha yako yote.
Kwa binadamu wa kawaida, ni vigumu sana kuigiza kwa kipindi kirefu. Huwa inafika hatua ya kuchoshwa na maigizo na uhalisia wa mtu kujitokeza wenyewe.
Hakuna haja ya kuigiza kitu ambacho unapaswa kwenda nacho kwa kipindi chote cha maisha yako. Utachoka na uhalisia utajidhihirisha wenyewe. Nguvu unazokuwa umetumia kwenye maigizo hayo zinakuwa zimepotea.
Endelea kusoma #BaruaYaKocha hapa; #BZK129; Kwa Nini ‘Kufeki’ Mafanikio Ni Hatari Kwa Mafanikio Yako Makubwa