Habari za siku ya leo mpenzi msomaji wa mtandao huu wa AMKA MTANZANIA, naamini umzima wa afya na unaendelea vyema na majukumu ya kuboresha maisha yako. Nami kwa moyo mkunjufu napenda kukukaribisha katika siku nyingine tena ambapo tunapata nafasi ya kujifunza na kuongeza maarifa yakutusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika maisha.
Katika mada yetu ya leo, tutajadili mambo ya lazima ambayo unatakiwa uyajue katika safari yako ya mafanikio. Ukumbuke kuwa, katika safari yoyote ya mafanikio huwa ipo misingi na mambo ya lazima ambayo ni lazima uyajue ili kufanikiwa. Kwa kuyajua mambo hayo yatakupa dira na mwelekeo mzuri wa kufikia mafanikio makubwa.
Ni kweli unaweza ukawa una malengo mazuri uliyojiwekea, lakini bila kuyajua mambo hayo na kuyafanyia kazi itakuwa ni ngumu sana kufikia mafanikio yako. Watu wengi wenye mafanikio wanayajua mambo haya na kuyafanyia kazi mara kwa mara. Je, unajua ni mambo gani ambayo ni ya lazima sana katika safari yako ya mafanikio?
 1. Hamasa.
Ili uweze kufanikiwa ni lazima kwanza uwe na hamasa kubwa ya kufikia mafanikio hayo. Wengi huwa wanashindwa kufanikiwa kwa sababu ya kukosa hamasa. Unapokuwa unashindwa kuwa na hamasa inakuwa ni ngumu kufikia mafanikio yoyote kwa sababu karibu kila kitu utakifanya kizembe au kivivu ilimradi ukikamilishe.
Kitu kinachokufanya uongeze juhudi kwa kile unachokifanya sasa ni kwa sababu una hamasa ya kutaka kufanikiwa. Kushindwa kwako kutaanza mara moja ikiwa utaanza kukosa hamasa hiyo. Huu ni ukweli ambao ni lazima uujue ili kuweza kufanikiwa, vinginevyo hakuna utakachoweza kukifanikisha. Kila kitu kitakuwa kigumu kwako.
LAZIMA UJIAMINI ILI UFANIKIWE
2. Uzingativu.
Haijalishi una hamasa kubwa kiasi gani lakini ikiwa ndani yako utakosa uzingativu, kuyafikia mafanikio hayo itabaki kuwa ndoto za mchana. Watu wote ambao huwa wanafanikiwa katika mambo yao ni watu wa kuzingatia sana. Huwa ni watu ambao hawana papara, wakianzisha jambo hulifatilia mpaka kulifanikisha.
Mara nyingi unapoweka nguvu ya uzingativu katika jambo moja, huwa zinaleta matokeo makubwa na kuyashangaza. Hakuna kinachoshindikana katika nguvu hizi za uzingativu zinapotumika. Hiki ni kitu ambacho unatakiwa kukiweka kwenye akili yako na kukifanyia kazi. Na hili ni jambo la lazima sana katika safari yako ya mafanikio, bila hivyo huwezi kufanikiwa.

3. Kujiamini.
Msingi mkubwa wa mafanikio upo kwenye kujiamini. Ikiwa wewe utakuwa mtu ambaye unajitilia shaka na hujiamini katika mambo yako ukweli wa mambo uko wazi hata ufanyaje huwezi kufanikiwa. Kama unabisha hebu angalia mambo ambayo hukuwahi kufanikiwa, utagundua mengi hukuweza kujiamini sana.
Kwa hiyo mpaka hapo utagundua kwamba kujiamini ni jambo la lazima sana katika safari ya mafanikio yako. Mafanikio yoyote yale yanahitaji kwanza wewe uanze kujiamini binafsi kuwa utafanikiwa. Kwa kadri unavyozidi kujiamini sana katika maisha yako, ndivyo ambavyo utajikuta ukifanikisha mengi.
4. Kufanya kazi kwa bidii.
Ni kweli unaweza ukawa una hamasa kubwa, una nguvu ya uzingativu na unajiamini vya kutosha, lakini kama hufanyi kazi kwa bidii huwezi kufanikiwa. Kazi ni msingi mkubwa sana wa mafanikio yoyote unayoyahitaji. Ili uweze kufanikiwa ni lazima kujituma na kufanya kazi kwa bidii zote. Hapo ndipo utaanza kuyaona mafanikio yako.
Watu wote wenye mafanikio makubwa ni watu wa kujituma sana. Bila kufanya kazi kwa bidii, elewa kabisa mipango na malengo yako mengi yataishia njiani. Kwa hiyo kama ni kazi weka juhudi zako zote mpaka ikuletee mafanikio. Kwa sababu unakuwa umeweka nguvu zako nyingi, hata ikitokea umeshindwa hutajilaumu sana. 
Kwa mambo hayo manne ni silaha kubwa sana ya mafanikio kwa mtu yeyote mwenye nia ya kufikia mafanikio makubwa. Kitu kikubwa naomba ufanyie kazi mambo hayo ili yaweze kubadili maisha yako na ya wengine wanaokuzunguka. Kila kitu kinawezekana ukiamua, hivyo amua sasa upate kufanikiwa.
Nikutakie kila la kheri katika safari yako ya mafanikio  na tukutane tena wakati mwingine, kwa makala nyingine nzuri ya kubadilisha maisha yetu. Kumbuka TUPO PAMOJA.
Kwa makala nyingine nzuri pia tembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku.
Ni wako rafiki katika mafanikio,                      
Imani ngwangwalu,
Simu; 0713 048 035,

E-mail; dirayamafanikio@gmail.com
Blog; www.dirayamafanikio.blogspot.com