Rafiki yangu mpendwa,

Wazungu wanao msemo wanaouita GIGO yaani GARBAGE IN, GARBAGE OUT, wakimaanisha kwamba kinachoingia kwenye mfumo wowote, ndiyo kinachotoka. Ukiingiza uchafu unatoa uchafu, na ukiingiza usafi unatoa usafi. Msemo huu umekuwa unatumika sana kwenye mifumo ya programu za kompyuta, lakini unaweza kutusaidia sana kwenye maisha yetu.

Ili kuweza kuwa na maisha bora na yenye mafanikio makubwa, sehemu ya kwanza kabisa unayohitaji kuchukua hatua ni kudhibiti kile kinachoingia kwenye maisha yako. Kama hutakuwa na udhibiti, kama utaruhusu kila kinachokuja kwenye maisha yako kiingie bila ya ukaguzi wa ubora wake, utajikuta unahangaika sana na maisha na hakuna hatua kubwa unazopiga.

Maisha yako yanatengenezwa na maeneo matatu muhimu yanayofanya kazi kwa ushirikiano na kuyafanya maisha yako kuwa bora na hata kufanikiwa zaidi. Bila ya kufanyia kazi maeneo haya matatu, na bila ya kuyadhibiti kwa kuchagua kinachoingia kiwe bora, ni vigumu sana kwako kupiga hatua.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Karibu kwenye makala ya leo, tujifunze maeneo haya matatu tunayohitaji kuyadhibiti hasa kwa kile tunachoingiza ili kuweza kuwa na maisha bora yenye mafanikio makubwa.

ENEO LA KWANZA; MWILI.

Mwili ndiyo nyumba pekee tunayoishi hapa duniani. Nafikiri mpaka sasa unaelewa kwamba wewe siyo mwili, bali mwili ni sehemu yako. Lakini mwili wako ndiyo utakaokuwezesha kufanya chochote unachotaka kufanya.

Kama mwili utakuwa kwenye afya bora, utaweza kufanya makubwa na kupiga hatua. Kama mwili hautakuwa kwenye afya bora, ni vigumu kwako kufanya makubwa.

Unahitaji kudhibiti sana kila kinachoingia kwenye mwili wako. Chakula unachokula, vinywaji unavyokunywa na hata vitu vingine unavyoruhusu viingie kwenye mwili wako, lazima uwe umevikagua sana.

Usiruhusu sumu yoyote iingie kwenye mwili wako, maana mwili wako ndiyo hekalu linalokubeba wewe. Kama utalijaza na sumu, utakuwa unajizuia wewe mwenyewe usifanikiwe.

Kwa maana hiyo basi, unahitaji kula vyakula vya kiafya, siyo vyakula vya haraka ambavyo zinaharibu mwili wako. Pia unahitaji kutoruhusu kabisa ulevi wowote kuiungia kwenye mwili wako.

Kitu chochote ambacho hakiufanyi mwili wako kuwa bora, usiruhusu kiingie kwenye mwili wako.

SOMA; Njia Kumi (10) Za Kuyafanya Maisha Yako Kuwa Rahisi Bila Ya Kuyarahisisha.

ENEO LA PILI; AKILI.

Akili yako ndiyo inayokuwezesha kupanga na hata kufikiria kule ambapo unakwenda. Ni akili yako ndiyo inayokuonesha fursa mbalimbali, inayokufanya uweze kufikiri kipi cha kufanya kwa hali unayokutana nayo.

Ili kufanikiwa, lazima akili yako iwe safi na iweze kufikiri vizuri na kufikia maamuzi sahihi.

Hivyo unahitaji sana kulinda akili yako, kwa kudhibiti kila kinachoingia kwenye akili yako. Usiruhusu akili yako kupokea kila aina ya mawazo, taarifa au maarifa. Kagua sana usahihi wa kila kinachoingia kwenye akili yako.

Usiruhusu habari na taarifa hasi ziingie kwenye akili yako. Usiruhusu mawazo ya hofu na kukata tamaa yatawale akili yako. Chochote kinachotaka kuingia kwenye akili yako, kikague kwanza na ona umuhimu na madhara yake.

Pia usitumie chochote ambacho kinapumbaza akili yako, kama vilevi na hata madawa mbalimbali.

Bila akili imara na iliyo safi, mafanikio yatakuwa magumu sana kwako.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; THE HEALING POWER OF MIND (Nguvu Ya Tahajudi Kwenye Afya, Uzima Na Uamsho)

ENEO LA TATU; ROHO.

Roho au kama wengine wanavyopenda kuita imani, ndiyo sisi kwa uhalisia wetu. Sisi ni viumbe  wa kiroho ambao tumepata nafasi ya kukaa kwenye miili ambayo tupo. Hivyo mafanikio yako yanategemea sana na jinsi ulivyo kiroho, ile imani ambayo unayo, au kwa maneno mengine, jinsi ambavyo upo.

Unahitaji sana kujidhibiti kiroho, kukagua na kuhoji kila aina ya imani ambayo umekuwa unaishikilia kwenye maisha yako. Kwa sababu cha kushangaza, imani nyingi unazoshikilia ndiyo zinakurudisha nyuma, licha ya wewe kukazana kuweka juhudi kubwa.

Kagua sana zile imani ambazo wengine wanataka kupandikiza kwako. Usifanye tu kitu kwa sababu wengine wanafanya, au kwa sababu umezoea kufanya. Hoji kila unachofanya na ona kina mchango gani kwenye kuyafanya maisha yako kuwa bora.

Pia jitengeneze kuwa mtu bora kabisa kiimani, kwa kupata muda wa kujitafakari, kutahajudi, kusali na hata kukaa na wewe mwenyewe, kufanya mazungumzo na wewe mwenyewe kwa namna maisha yako yanavyokwenda.

Maisha ya mafanikio ni pale maeneo hayo matatu ya maisha yako yanapokwenda vizuri kwa ushirikiano. Unahitaji kudhibiti sana kila kinachoingia kwenye maisha yako kwenye maeneo hayo matatu. Kwa sababu chochote unachoruhusu kiingie, kina madhara fulani, sasa hakikisha madhara yanayopatikana ni chanya na siyo hasi.

Mwisho nikukumbushe maisha yako ni jukumu lako, na hulazimiki kufanya chochote ambacho hutaki kufanya. Kuwa huru na maisha yako, chagua kile unachotaka kufanya na kifanye kwa juhudi kubwa na kwa hakika utafanikiwa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha