Rafiki yangu mpendwa,

Mafanikio kwenye maisha yako siyo matokeo bali ni mchakato, siyo mwisho wa safari, bali ni safari yenyewe.

Wengi wanaofanikiwa halafu wanakuwa na maisha ya hovyo ni kwa sababu hawakuelewa vizuri mafanikio. Walikazana kufikia kitu fulani kwa sababu walijua wakishakipata basi watakuwa hawana haja ya kuhangaika tena.

Lakini maisha yetu ni kwa ajili ya kuhangaika, kuanzia siku unazaliwa mpaka siku unakufa. Ndiyo maana wale wanaofanikiwa kisha wanapumzika au kujiambia wanastaafu, huwa maisha yao yanakuwa magumu sana kwenye kustaafu kwao.

Mafanikio ni yale maisha unayoyaishi kila siku, zile hatua unazokazana kupiga kila siku. Na ndiyo maana wanafalsafa na hata waandishi wengi, wanakazana sana kufundisha umuhimu wa kila siku ambayo tunaiishi.

Yaani hata kama hutakuwa na mpango mkubwa wa maisha yako, kukazana kuishi kila siku kwa ubora wa hali ya juu kutayafanya maisha yako yawe bora sana.

MASAA MAWILI YA ZIADA

Mwanafalsafa Socrates, ni mmoja wa mabaa wa falsafa, mmoja wa watu ambao wametujenga misingi muhimu sana ya kifalsafa na kimaisha. Kupitia yeye tunakwenda kujifunza maeneo manne muhimu ya kufanyia kazi kila siku ili tuweze kutengeneza maisha ya mafanikio kwetu.

Eneo la kwanza; kujidhibiti.

Eneo la kwanza kabisa unalohitaji kulifanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni kwenye udhibiti. Unahitaji kujidhibiti wewe mwenyewe, la sivyo utawapa wengine nafasi ya kukudhibiti wewe. Unahitaji kujipangia nini utafanya na kipi hutafanya na kufuata mpango huo.

Muda ulionao kila siku ni mfupi sana, ni muda ambao kama ukiweza kujidhibiti utaweza kufanya makubwa. Lakini ukishindwa kujidhibiti, utashangaa muda unaisha na hakuna ulichofanya. Lazima uweze kujiambia HAPANA wewe mwenyewe, pale unapojiona unakosa udhibiti. Pia lazima uweze kujiadhibu wewe mwenyewe pale unapokwenda kinyume na mipango uliyojiwekea wewe mwenyewe.

Jidhibiti wewe mwenyewe na kila siku yako itakuwa siku ya ushindi, kwa sababu utafanya yale ambayo ni muhimu zaidi kwako.

SOMA; Maeneo Matatu Muhimu Ya Kudhibiti Kinachoingia Kwenye Maisha Yako Ili Kuweza Kuwa Na Maisha Bora Na Ya Mafanikio Makubwa.

Eneo la pili; uhalisi.

Kitu kimoja ambacho dunia inakazana sana kufanya kwako ni wewe uwe kama wengine. Kwa sababu dunia inajua ukiwa wewe, utakuwa msumbufu, hutafaa kutawaliwa na hivyo inakazana sana uwe kama wengine, uwe ndani ya kundi ili uweze kutawaliwa na kutumiwa vizuri na wengine.

Hivyo eneo la pili la kufanyia kazi kila siku ili kuwa na maisha bora ni uhalisi. Unapaswa kukazana kuwa halisi kila siku, kuishi maisha yako kwa uhalisia, kuacha kuigiza na kuacha kufanya vitu ili kuwaridhisha wengine au uonekane na wewe unafanya.

Hutaweza kufanikiwa kama huishi maisha halisi kwako, hata kama utapata vitu vingi kiasi gani, kama maisha unayoishi siyo halisi kwako, kila mara utasikia sauti inakuambia wewe bado sana. Na hapa ndipo wengi husema wamefanikiwa lakini hawana furaha.

Shida yao ni moja tu, maisha wanayoishi siyo halisi kwao, ni maisha feki na hivyo mafanikio yoyote wanayopata yanakuwa yanaonekana na wengine lakini siyo ndani yao binafsi.

Kuwa halisi kwako, jua uimara wako, jua madhaifu yako, jua yapi yenye maana kwako na jua kusudi la maisha yako ni lipi. Kisha tumia kila dakika ya siku yako kuishi maisha ambayo ni halisi kwako. Utafanikiwa kariri unavyoishi maisha halisi kwako.

Eneo la tatu; kujitambua.

Kujitambua ni eneo muhimu sana la kufanyia kazi, na linatangulia uhalisia. Kwa sababu bila ya kujitambua, hutaweza kuishi uhalisia wako. Na changamoto ya kujitambua ni kwamba ni zoezi endelevu.

Watu wengi wamekuwa wakifikiri wakishajua wanataka nini kwenye maisha yao, wakishaweka malengo makubwa basi wamemaliza. Hiyo siyo sahihi, unachojua leo kuhusu wewe, kinaweza kuwa tofauti kabisa na utakachotambua kesho kuhusu wewe.

Kubadili mazingira, kukutana na changamoto, kote huko kutakufunulia kwa undani kuhusu wewe. Mara nyingi huwezi kujua una uwezo wa kufanya makubwa kiasi gani mpaka pale unapokutana na changamoto kubwa kwenye maisha yako.

Hivyo zoezi la kujitambua ni endelevu, kila siku, kwa kila unachopitia, jiulize ni kipi kipya umejua kuhusu wewe. Na wakati mzuri wa kujipima ni pale unapopitia mambo magumu. Utaweza kupima uwezo wako wa kudhibiti hasira pale unapokasirishwa hasa. Unaweza kujua unaweza kuvumilia ugumu kiasi gani pale unapokutana na ugumu zaidi.

Kila siku mpya ya maisha yako ni siku ya kujitambua zaidi, ishi kila siku kwa kutaka kujitambua na maisha yako yatakuwa bora sana.

SOMA; Kama Huwezi Kutoa Fedha Yako Na Kununua Kitu Hichi Kimoja, Unajizuia Wewe Mwenyewe Kufanikiwa.

Eneo la nne; kujiendeleza.

Eneo la nne ambalo unapaswa kulifanyia kazi kila siku ni kujiendeleza wewe binafsi. Kila siku lazima ukazane kuwa bora zaidi kuliko siku iliyopita. Kila siku unapaswa kujifunza kitu kipya. Usikubali siku iishe ukiwa kama siku ya jana ilivyoisha.

Weka kipaumbele kwenye kujifunza. Jifunze kupitia kusoma, kusikiliza, kuangalia na hata kufanya. Soma vitabu, sikiliza mafundisho mbalimbali, waangalie wengine kwa namna wanavyofanya na jaribu vitu vipya kwa ajili ya kujifunza kwa kufanya.

Jinsi unavyojifunza kila siku, unazidi kuwa bora na kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.

Rafiki yangu mpendwa, maeneo haya manne ni muhimu sana kwako kuyafanyia kazi kila siku. Ninaposema kila siku, namaanisha kila siku ya maisha yako. Na usiache hata siku moja, mpaka siku unaondoka hapa duniani.

Kama unajiambia huwezi kila siku, kama unajiambia utajisahau au kupitiwa na maisha mengine, ninayo nafasi ya kukumbusha hili kila siku, na kukushirikisha fursa za kujifunza na kujitambua kila siku. Karibu kwenye KISIMA CHA MAARIFA, ambapo utapata nafasi ya kuingia kwenye kundi la wasap, na kila siku utajifunza kwenye maeneo hayo manne na mengine mengi.

Nakutakia kila la kheri katika kufanyia kazi maeneo haya manne kila siku, maeneo haya ni muhimu sana kwako rafiki yangu, weka nguvu na muda wako kwenye maeneo hayo, na hutabaki pale ulipo sasa.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; http://eepurl.com/dDZHvL

Usomaji