Rafiki yangu mpendwa,

Changamoto zipo kwenye maisha yetu kwa lengo moja tu, kutufanya kuwa imara ili pale tunapopata mafanikio makubwa, tusianguke kirahisi. Hivyo hatupaswi kuzichukia wala kuzikimbia changamoto, badala yake tunapaswa kuzipokea na kuzitatua ili tuwe imara na tayari kuyapokea mafanikio makubwa.

Karibu kwenye makala yetu ya ushauri ambapo tunakwenda kushirikishana hatua za kuchukua pale unaposhindwa kwenye kila unachofanya kwenye maisha yako.

Kabla hatujaangalia kwa kina hatua hizo za kuchukua, tusome maoni ya mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili;

Kila kitu chochote ninachofanya hakikuwi sio ndoa, biashari. Kila kitu. – Irene M. K.

Rafiki, ipo kauli kwamba; mtu mmoja akisema una matatizo, ana kisa na wewe, watu watatu wakisema una matatizo wanajaribu kukuhujumu, lakini watu kumi wakisema una matatizo, basi huenda ni kweli una matatizo.

KURASA ZA MAISHA YA MAFANIKIO

Tukitumia kauli hiyo kwenye ushauri wa leo; ukishindwa kwenye kitu kimoja, kitu hicho hakikuwa sawa, ukishindwa kwenye vitu vitatu unajifunza kuwa bora, ukishindwa kwenye kila unachofanya, kwa hakika una matatizo, na unahitaji kuchukua hatua ya kubadilika wewe kwanza kabla ya kufanya kingine chochote.

Ndiyo rafiki, kama kila unachofanya kinashindwa kuanzia kazi, biashara, mahusiano, ndoa na kila kitu, basi wewe ndiyo tatizo kubwa. Kwa sababu haiwezekani vitu vyote hivyo ambavyo havihusiani vikawa vina matatizo kila vikikutana na wewe.

Hivyo zifuatazo ni hatua muhimu za kuchukua ili kuondoka kwenye hali hiyo ya kushindwa kwenye kila unachofanya.

Hatua ya kwanza; kubali kwamba wewe ni tatizo.

Hatua ya kwanza na ya muhimu kabisa ni wewe kukubali kwamba una tatizo, yaani wewe ndiyo tatizo kuu. Kama hutaweza kukubali hili, ni bora uishie hapa kusoma, maana hatua za mbele hazitakusaidia kama hutakubali wewe ni tatizo.

Inahitaji ujasiri kukubali kwamba wewe ni tatizo, kukubali kwambe wewe ndiye unayekosea, na ndiyo maana wengi huwa wanaendelea kushindwa.

Kubali wewe ndiye tatizo kwenye mambo yote yaliyoshindwa.

Hatua ya pili; yajue makosa ambayo umekuwa unayarudia mara kwa mara.

Kwa kuangalia maeneo yote ambayo umeshindwa, utagundua kuna makosa fulani ambayo unayarudia rudia kila wakati. Yajue makosa hayo kwa sababu hapo ndipo unapokwenda kuanza kutatua tatizo ambalo ni wewe.

Angalia kama umekuwa unaweka umakini wa kutosha kwenye kila unachofanya, angalia kama umekuwa na nidhamu na kujituma kwenye yote unayofanya, angalia kama umekuwa mwadilifu, angalia kama hakuna uvivu na uzembe ambao umekuwa unaruhusu uingie kwenye yale unayofanya na ikapelekea wewe kushindwa.

Wanasema kujua tatizo ni nusu ya kulitatua, jijue wewe mwenyewe jinsi ambavyo umekuwa tatizo kwako mwenyewe ili uweze kuchukua hatua sahihi za kuzuia kushindwa tena.

SOMA; Maeneo Manne (4) Ya Kufanyia Kazi Kila Siku Ili Uwe Imara Na Uweze Kutengeneza Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako.

Hatua ya tatu; chagua tabia utakazojijengea kwa ajili ya mafanikio.

Baada ya kujua makosa yako yapo wapi, chagua tabia utakazojijengea na kuziishi kila siku ambazo zitakuwezesha kuepuka makosa yako na kukuwezesha wewe kufanikiwa.

Kuwa na msingi unaoongoza maisha yako na ambao utajikumbusha na kuuishi kila siku.

Msingi rahisi sana ambao nimekuwa nashauri kila mtu auishi kwa ajili ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA.

Kuwa na nidhamu kwako wewe binafsi, kwa kufanya yale uliyopanga kufanya, kuwa na nidhamu ya muda kwa kutokupoteza muda wako kwa mambo yasiyo sahihi. Kuwa na nidhamu ya fedha kwa kuwa na matumizi ambayo ni chini ya kipato chako. Pia kuwa na nidhamu ya kazi kwa kuheshimu na kufanya kazi au biashara yako kwa ubora wa hali ya juu.

Kuwa na uadilifu kwako mwenyewe na kwa wengine pia. Ishi kile unachohubiri, timiza kile unachoahidi, heshimu mahusiano yako na wengine na usiwafanyie wengine kile ambacho usingependa wao wakufanyie. Na muhimu zaidi, wafanyie wengine vile ambavyo wangependa kufanyiwa.

Pia kuwa mtu wa kujituma, nenda hatua ya ziada kwa kila unachofanya, weka juhudi zaidi, toa thamani zaidi, fanya zaidi ya unavyolipwa na washangaze wale wote unaowahudumia, iwe ni kwenye kazi au biashara, mfanye kila anayekutana na wewe aondoke akiwa bora kuliko alivyokuwa kabla hajakutana na wewe.

Kwa msingi huu wa NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA, utaweza kuyabadili kabisa maisha yako.

Hatua ya nne; jifunze kila siku.

Hatua ya nne ya kuchukua ni kujifunza kila siku, jifunze kupitia mafunzo mbalimbali yaliyoandaliwa kuhusu kila unachofanya, jifunze kupitia maisha ya wengine na pia jifunze kwenye kila unachofanya.

Usikubali kufanya kitu chochote kwa mazoea, badala yale jifunze njia bora zaidi za kufanya chochote unachofanya, na kila siku piga hatua zaidi.

Hatua ya tano; kuwa na mtu wa kukusimamia na kukufuatilia kwa karibu.

Mazoea ni mabaya, tabia mbaya ni ngumu kuvunja. Unaweza kuanza na hamasa kwamba utabadilika, baada ya muda mfupi ukarudi nyuma. Ndiyo maana unahitaji kuwa na mtu anayekusimamia na kukufuatilia kwa karibu.

Mtu huyu anaweza kuwa mtu wa karibu kwako anayejali kuhusu wewe, anaweza kuwa menta wako au kuwa kocha wako ambaye atakusaidia usirudi nyuma.

Kwa vyovyote vile, hakikisha yupo mtu nyuma yako ambaye hatakuruhusu kabisa urudi tena nyuma, na atakufuatilia kwa karibu kiasi kwamba itakubidi uendelee kufanya hata kama mambo yamekuwa magumu kiasi gani.

Rafiki, fuata hatua hizo tano na utaweza kuyabadili kabisa maisha yako, utaondoka kwenye kushindwa kwenye kila kitu mpaka kufanikiwa kwenye kila kitu.

Kama utahitaji huduma za ukocha, tembelea www.amkamtanzania.com/kocha

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog

Usomaji