Rafiki yangu mpendwa,
Hongera kwa kuweza kufika ukingoni mwa juma hili la 39 kwa mwaka huu 2018. Na pia hongera kwa namna ambavyo mwaka huu unakwenda kwako.
Kama tumekuwa pamoja tangu mwaka huu unaanza, hasa kama umekuwepo kwenye KISIMA CHA MAARIFA tangu tunafanya semina ya kuuanza mwaka huu, utakuwa umepiga hatua kubwa sana mwaka huu kuliko miaka mingine iliyopita.
Na hata kama umekutana na changamoto, basi umeweza kuzitatua kwa ubora zaidi na hujakubali changamoto yoyote uliyokutana nayo ikurudishe nyuma.
Karibu kwenye TANO ZA JUMA, ambapo nakushirikisha mambo matano muhimu niliyojifunza na kukutana nayo kwenye juma husika, ambayo pia wewe rafiki yangu unaweza kujifunza na kuchukua hatua kisha maisha yako yakawa bora zaidi.
#1 KITABU NILICHOSOMA; HII ITAKUUMIZA.
Katika vitabu nilivyosoma juma hili, kipo kitabu cha Daktari aliyeamua kuachana na udaktari ambaye ametushirikisha safari yake yangu anaanza udaktari mpaka anafikia maamuzi ya kuachana na udaktari.
Kitabu kinaitwa THIS IS GOING TO HURT; SECRET DIARIES OF A JUNIOUR DOCTOR ambacho kimeandikwa na Adam Kay.
Adam Kay alihitimu mafunzo ya udaktari nchini Uingereza na kuanza rasmi safari ya kazi ya udaktari mwaka 2004. Alifanya kazi hiyo, huku akipanda ngazi kulingana na mfumo wa udaktari nchini humo, mpaka kufikia mwaka 2010 akiwa amefika ngazi ya mwisho kabla ya kuwa daktari bingwa, alipoamua kuachana kabisa na udaktari na kuingia kwenye uandishi wa vichekesho.
Kupitia kitabu chake cha THIS IS GOING TO HURT, Adam ametushirikisha kumbukumbu zake alizokuwa anaandika kwenye kijitabu chake kwenye siku zake za maisha ya udaktari.
Ni kitabu ambacho ukianza kukisoma huwezi kukiweka chini, kwa sababu tangu mwanzo mpaka unakaribia mwisho, ameandika kwa mfumo wa kuchekesha na furahia. Lakini sura ya mwisho ya kitabu ndipo unapopata huzuni kubwa na huenda ukatokwa na machozi, pale anaposhirikisha kisa kilichomfanya aamue kuachana kabisa na udaktari.
Ni kitabu ambacho kila mtu anaweza kujifunza kuhusu kazi na maisha na siyo kwa udaktari tu, bali kwa chochote ambacho mtu unaamua kufanya na maisha yako.
Nishirikishe kwa kifupi yale ambayo Adam ametushirikisha kwenye kitabu chake.
Wazo la yeye kuandika kitabu lilikuja miaka mitano tangu alipoamua kuachana na udaktari, ambapo alitumiwa ujumbe kutoka taasisi ya usajili wa madaktari nchini huko, ujumbe ukimwambia kwama ataondolewa kwenye orodha ya madaktari kwa sababu kwa miaka mitano hajafanya kazi ya udaktari. Na hapo ndipo alipokumbuka maisha ya udaktari, tangu alipoanza mpaka alipoishia, akakumbuka kijitabu chake alichokuwa anaandika matukio ya kila siku.
Hivyo alichukua matukio yale na kuyafanya kuwa kitabu. Ni matukio yenye kufundisha, kufurahisha na kuhuzunisha pia.
Adam anaelezea jinsi kazi ya udaktari ilivyokuwa inachukua muda wake mwingi, alikuwa na shifti nyingi za kufanya kazi na hakuwa kabisa na muda wa kupumzika. Anaeleza kuna kipindi alikuwa anapata masaa mawili pekee ya kulala kwa siku.
Kwenye kitabu hiki anatushirikisha changamoto za kazi, hasa ule ugeni kwenye kazi mpaka kuzoea kazi na kuweza kufanya maamuzi sahihi. Anatushirikisha changamoto ya wasimamizi wake, yaani wale madaktari bingwa aliokuwa anafanya kazi chini yao. Na pia anatushirikisha changamoto za wagonjwa, ambazo zinatofautiana kuanzia wagonjwa kuwa na mahitaji yasiyo ya msingi, mpaka wagonjwa kuja kama wana dharura na usiku wa manane kumbe hawana chochote wanachoumwa bali tu wasiwasi.
Kwa miaka 6 ambayo Adam alifanya kazi ya udaktari, alikuwa amehamishwa hospitali mbalimbali, zote kwa lengo la kujifunza. Baada ya kufanya kazi kama daktari wa kawaida kwa mwaka, alichagua kufanya kazi kama daktari wa wanawake, eneo ambalo lilimfanya kama akose maisha yake yote.
Mara nyingi yeye ndiye aliyekuwa kazini kwa sababu alikuwa hajawa daktari bingwa, na hivyo dharura zote alizifanyia kazi yeye. Anatushirikisha jinsi ambavyo alikuwa anaitwa kuhudumia dharura nyingine wakati yupo katikati ya dharura. Na dharura za wagonjwa wa wanawake ni dharura kweli, kama mtu anajifungua na mtoto amekwama hatoki, au kama mtu amesukuma na mtoto amechoka na mama naye kachoka, ni dharura ya kuchukua hatua ndani ya dakika chache la sivyo unaweza kumpoteza mtoto na hata mama pia.
Kupitia kazi yake Adam alikutana na madaktari waliojali na wasiojali, alikutana na wagonjwa wanaojali na wasiojali.
Kazi ilimfanya akose kabisa maisha ya kijamii, maana hakuna siku ambayo aliweza kusema angeondoka kazini mapema au kutokwenda kabisa kazini. Anatuelezea kisa kimoja ambapo aliumwa na alishauriwa asifanye kazi, lakini bado alihitajika awepo eneo lake la kazi.
Adam alikuwa akijituma sana na kujali kazi yake, alikuwa tayari kujifunza na aliweza kufanya mengi na makubwa kwa muda ambao alikuwa anafanya kazi kama daktari wa magonjwa ya wanawake.
Mara kwa mara alikuwa akiyatafakari maisha yake, akijilinganisha na wengine aliosoma nao lakini walichagua taaluma nyingine, walikuwa wamepiga hatua kuliko yeye. Lakini alijipa moyo kwa sababu aliona jinsi juhudi zake zinavyoleta matunda mazuri, na kuyafanya maisha ya wengine kuwa bora. Mfano kuokoa maisha ya mama na mtoto, kuwasaidia wanandoa waliokosa watoto mpaka kuweza kupata watoto na kadhalika.
Akiwa anakaribia kabisa kufikia kuwa daktari bingwa, kilitokea kisa ambacho kilimkatisha tamaa na kupelekea yeye kuamua kuachana na udaktari. Anaeleza wakiwa kazini, kulikuwa na mama mjamzito ambaye vipimo vilionesha mtoto ameanza kuchoka hivyo asingeweza kujifungua kwa njia ya kawaida bali kwa operesheni. Hivyo alimwambia msaidizi wake amwandae kwa ajili ya operesheni ya kumtoa mtoto. Msaidizi wake alimwomba afanye operesheni hiyo huku yeye akimsimamia kwa karibu. Kwa sababu alikuwa ameshasaidia operesheni nyingi, Adam alimkubalia.
Operesheni ilianza vizuri katika kufungua tumbo la mama, na walipofikia tumbo la uzazi, alipokata, badala ya kutoka maji ya kawaida ambayo yanamzunguka mtoto, zilitoka damu nyingi. Msaidizi yule alitahamaki lakini Adam alimpa moyo aendelee kumtoa mtoto, alipojaribu alishindwa. Ndipo adam alipojaribu naye na kugundua kondo (plasenta) la mtoto lilikuwa limekaa sehemu mbaya, hivyo kizazi kilipofunguliwa, kondo lilikatwa damu nyingi zikapotea. Hili lingeweza kuonekana mapema kama kipimo cha ultrasound kingefanywa kwa umakini. Hivyo mama alipoteza damu nyingi, mtoto akafa na ilibidi mama aongezewe damu nyingi sana na hata baada ya operesheni kuisha, ambapo ilipelekea mama kuondolewa kabisa kizazi chake, ilibidi apelekwe chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa sababu alikuwa na hali mbaya sana.
Katika operesheni hiyo ilibidi amwite daktari bingwa, ambaye naye hakufanikiwa, ikabidi aitwe daktari mwingine bingwa zaidi na mwisho wakafikia kuondoa kizazi. Lengo la kwanza ilikuwa kuzuia damu isiendelee kutoka na kukiacha kizazi, maana ule ulikuwa uzazi wa kwanza wa mama yule, lakini hilo halikuwezekana na lilipelekea kizazi kuondolewa kabisa na mama kuwa kwenye hali mbaya sana.
Baada ya tukio hili, Adam aliona jinsi ambavyo kukosa kwake umakini kabla ya operesheni kulivyoleta madhara makubwa. Japo madaktari bingwa walimweleza kwamba hicho ni kitu cha kawaida na hakuna daktari ambaye hajawahi kupitia, yeye hakuweza kujisamehe. Alikosa kabisa morali wa kazi, akawa mtu wa mawazo muda wote na hatimaye kufikia maamuzi ya kuachana kabisa na kazi ya udaktari.
Yafuatayo ni mambo ambayo Adam anatufundisha kupitia kitabu hiki cha sehemu ya maisha yake ya udaktari;
- Maamuzi ya mtu unakua nani kwenye maisha yanafanyika mtu akiwa bado ni mdogo sana na hajajua nini kipo mbele yake. Adam anasema alifanya maamuzi ya kuwa daktari akiwa na miaka 16, anasema kama kipindi hicho angepewa ukweli kwamba maisha ya udaktari yapoje, asingekimbilia.
- Kinachowasukuma wengi kuingia kwenye taaluma fulani, huwa siyo wanachokwenda kukutana nacho. Na hapa watu wengi sana wameangushwa na uchaguzi wao wa taaluma. Mtu anachagua kusomea kitu fulani akitegemea anapohitimu atapata vitu fulani au ataweza kufanya vitu fulani, lakini anapohitimu, anakutana na uhalisia ambao hakuutegemea.
- Unapoanza kazi yoyote ile, mwanzo huwa mgumu sana, unakuwa huelewi namna ya kuweka vipaumbele vyako na wengi wanatumia upya wako kama sehemu ya kupunguza majukumu yao. Hili Adam aliliona sana kwenye majukumu aliyokuwa anaachiwa afanye maamuzi mwenyewe, ambapo angepaswa kuwa na mtu wa juu yake wa kumsaidia.
- Kuchagua kazi yoyote ila kwa kigezo cha kipato ni kujiandaa kuumia, kwa sababu kazi nyingi hazitakupa kipato kinachoendana na juhudi unazopaswa kuweka kwenye kazi hiyo. Hivyo kitu cha kwanza unachopaswa kutumia kufanya maamuzi ya kazi ni mapenzi na kujali. Ikiwa unafanya kile unachopenda, na unakijali kwa sababu kina maana kwako, hata kama hutapata fedha nyingi kwa haraka, utakuwa na maisha bora na baadaye kipato chako kitakuwa kizuri.
- Asante ya yule unayemhudumia ni nguvu kubwa ya kukufanya uendelee kupiga hatua kuliko malipo unayopata au vyeo unavyopewa.
- Tunapaswa kuyajali maisha yetu binafsi hata kama kazi zinatuhitaji kiasi gani. Tukiangalia maisha ya Adam kwa kipindi chote cha udaktari, aliweka mbele maisha ya wagonjwa wake na kusahau maisha yake binafsi, kitu ambacho kilipelekea mwishoni ashindwe kabisa kuendelea na kazi yake.
- Tunapaswa kujua kwamba kufanya makosa ni sehemu ya ubinadamu, na tunachopaswa kufanya ni kujifunza kupitia makosa hayo ili tusiyarudie tena. Kosa moja kubwa alilofanya Adam alishindwa kujisamehe kwa sababu alikuwa ameijali sana kazi yake kuliko maisha yake binafsi.
- Jitoe kufanya kitu, na kama huwezi kujitoa, ni bora ukaachana nacho, bila ya kujali umewekeza muda na nguvu kiasi gani. Watu wengi huwa wanakuja kugundua kwamba uchaguzi waliofanya siku za nyuma, kwenye masomo au kazi ulikuwa wa makosa. Lakini wanaendelea na kazi hizo kwa sababu wanaona hawana cha kufanya. Wanafanya kazi za hovyo na chini ya kiwango na hilo haliwaridhishi, kinachotokea ni maisha yao yanakuwa hovyo. Kilichopelekea Adam kushindwa kujisamehe na kuamua kuachana na udaktari siyo tukio hilo moja, bali alishagundua tangu awali kwamba maisha ya udaktari siyo aliyotegemea, lakini hakuweza kufanya maamuzi ya haraka ya kuondoka, mpaka lilipotokea tukio lililomlazimisha kufanya maamuzi.
- Kufanya kazi kwenye sekta za umma ni kufanya kazi kwenye mazingira magumu sana, unajikuta unatumia akili yako ya ziada na nguvu za ziada kuwahudumia wale wanaotegemea huduma lakini wale wanaokusimamia hawajali hilo. Adam ameeleza kwenye kitabu chake jinsi wanasiasa walivyo rahisi kusema madaktari wanalipwa sana au wana tamaa, lakini wasijue kwamba kazi wanayoifanya ni kubwa sana ukilinganisha na wanacholipwa.
- Huwezi kuacha kuwa daktari. Pamoja na kuachana na udaktari, Adam anatuambia kwamba ukishakuwa daktari, utaendelea kuwa daktari. Hata kama hutibu moja kwa moja, bado utasaidia kutoa huduma ya kwanza pale unapokuwa na ikatokea uhitaji huo, utaweza kutosha ushauri wa kiafya kwa wale wanaouhitaji na pia utaweza kukutana na madaktari wengine pale inapohusu maslahi ya udaktari. Hivi ni vitu ambavyo Adam anaendelea kufanya licha ya kuwa ameachana na udaktari.
Kupitia kitabu chake cha THIS IS GOING TO HURT, Adam ametushirikisha jinsi maisha ya udaktari yalivyoumiza maisha yake na maisha ya wale wa karibu kwake, lakini mwishoni aliamua kuchukua maamuzi ambayo angepaswa kuyafanya muda mrefu.
Yapo mengi sana ya kujifunza kwenye kitabu hiki, na pia yapo mengi ya kuchekesha ambayo Adam ametushirikisha, usiache kupata na kusoma kitabu hiki.
#2 MAKALA YA JUMA; USHAURI MUHIMU KWA WENYE MIAKA 20 MPAKA 50.
Kuna watu wengi sana ambao wamekuwa wanajiambia hawawezi kuanza safari ya maisha ya mafanikio kwa sababu umri umeshawaacha. Wanaona umri umeenda na hakuna wanachoweza kufanya.
Ninachotaka kukuambia rafiki yangu ni hiki, popote ulipo sasa, bila ya kujali umri wako, unaweza kuanza safari yako ya mafanikio.
Tunaishi zama ambazo umri wa watu kuishi umeongezeka sana, sasa hivi watu wanaweza kuishi zaidi ya miaka 80 mpaka miaka 100. Hivyo popote ulipo sasa, hata kama una miaka zaidi ya 60, una zaidi ya miaka 20 mbele yako.
Na unachohitaji ili kutengeneza mafanikio makubwa sana kwenye maisha yako, ni kama miaka 10 ya kuweka kazi kisawasawa, kitu ambacho unakiweza kama unasoma hapa.
Na kwa wale wenye miaka 20, 30, mpaka 40 ndiyo kabisa wanapaswa kutokufikiria kuhusu dhana kwamba umri wao umeenda, maana kama upo kwenye kundi hilo, ni sawa na hata hujayaanza maisha kabisa. Maana unaweza kuamua kuwa kama unayaanza maisha yako leo na ukawa na miaka zaidi ya 40 ya kuishi kwa mafanikio zaidi.
Kwenye makala ya juma hili, nimelieleza hili kwa kina, isome hapa; USHAURI; Ujumbe Muhimu Sana Kwa Wenye Miaka 20, 30, 40 Mpaka 50. Kama Unajiona Muda Umekutupa Mkono, Soma Hapa.
Juma hili pia nilikushirikisha makala ya hatua sita za kuanzisha biashara na kuweza kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti. Unaweza kuisoma makala hiyo hapa; Hatua Sita Za Kufuata Ili Kuweza Kuanzisha Biashara Na Kutengeneza Kipato Kupitia Mtandao Wa Intaneti.
Makala zaidi zipo kwenye AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kila siku.
#3 TUONGEE PESA; KITU UNACHOPASWA KUFANYA NA NYONGEZA YAKO YA KIPATO.
Moja ya vitu vya kushangaza kuhusu fedha ni kwamba, wengi huwa wanaanza na kipato kidogo, kinakuwa hakiwatoshi, wakiongezewa wanafurahia kweli, baada ya muda kile kipato cha nyongeza kinakuwa hakiwatoshi tena, kinaongezwa tena na baada ya muda kinakuwa hakitoshi.
Kwa kifupi watu tumekuwa na tabia ya kukuza maisha yetu kila kipato chetu kinapoongezeka, kitu ambacho hakina ubaya wowote. Unapoanza kazi ukawa na kipato kidogo, unajibana kwa kipato hicho, lakini kinapoongezeka, na wewe unayabadili maisha yaendane na kipato chako.
Lakini nashauri mtu usilifanye hilo kwa haraka. Kwa mfano pale kipato chako kinapoongezeka, usikimbilie kuongeza maisha yako yaendane na kipato chako kipya. Badala yake ishi kwa kipato chako cha awali, halafu ile nyongeza ya kipato unayopata iweke kwenye akiba yako ambayo haigusiki (kama unakumbuka; GEREZA LA AKIBA YAKO). Fanya hivyo kwa muda wa miezi sita mpaka mwaka mmoja, halafu unaweza kukuza maisha yako yaendane na kipato kipya unachoingiza.
Ukifanya hivi, utajikuta baada ya miezi hiyo sita huhitaji hata kutumia kipato hicho cha ziada, badala yake utakuwa umeshatengeneza njia mbadala za kukupatia fedha unayohitaji.
Kila kipato chako kinapoongezeka, iwe ni kwenye ajira au biashara zako, chukua ongezeko hilo na liweke kwenye akiba ambayo huwezi kuitumia. Najua unajua matumizi ya akiba hiyo, ni kwa ajili ya uwekezaji unaozalisha fedha zaidi baadaye.
Kama umekuwa unaishi maisha uliyokuwa unaishi mwanzo mpaka hapo ulipofika, ina maana kwamba unaweza kuendelea kuyaishi kwa miezi sita mpaka mwaka mmoja ujao, na usiwe na tatizo kubwa. Jaribu hilo na utaona jinsi ambavyo unaweza kujitengenezea uhuru wako wa kifedha.
#4 HUDUMA NINAZOTOA; SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018.
Rafiki, kwa muda sasa nimekuwa nakukumbusha kuhusu SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018, ambayo itafanyika tarehe 03/11/2018. Ni semina ya kukutana ana kwa ana itakayofanyika jijini dar es salaam na inayofanyika mara moja pekee kwa mwaka.
Kwenye semina hii tutakwenda kujifunza mambo yote muhimu kuhusu mafanikio kwenye maisha, kazi, biashara, fedha na uwekezaji. Pia tutapata shuhuda za wanamafanikio wenzetu, ambao wanapambana na kuweka juhudi kufikia maono makubwa waliyonayo kwenye maisha yao.
Ni semina ya siku nzima, ambayo utaondoka ukiwa na mpango wa kufanyia kazi kwa mwaka mzima unaofuata. Semina ambayo utaondoka na msingi muhimu wa kuyaendesha maisha yako kwa mafanikio makubwa sana.
Ni semina ambayo kila mtu mwenye kiu ya mafanikio, kila anayetaka kuacha alama kwenye hii dunia, kila anayetaka maisha yake yawe na mchango kwa wengine, anapaswa kuhudhuria.
Ada ya kushiriki semina hii ni tsh 100,000/= (laki moja) na ada inalipwa kwa mpesa 0755 953 887 au tigo pesa/airtel money 0717 396 253 majina ya namba hizo ni Amani Makirita.
Mwisho wa kulipa ada ili kupata nafasi ya kushiriki semina hii ni tarehe 31/10/2018. Hivyo lipa ada yako mapema ili upate nafasi ya kushiriki semina hii.
Pia unaweza kulipa ada kidogo kidogo mpaka tarehe ya mwisho inapofikia uwe umeshakamilisha kulipa.
Muhimu zaidi, kama unapanga kushiriki semina hii, tuma jina lako na namba yako ya simu kwenda namba 0717396253 ili ujihakikishie nafasi ya kushiriki. Kama bado hujatuma jina lako tuma sasa, hata kama utafanya malipo baadaye.
Karibu sana kwenye SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA 2018 ambapo utapata nafasi ya kujifunza na kuhamasika kuchukua hatua kwa kipindi cha mwaka mzima.
#5 TAFAKARI YA KUFIKIRISHA; JINSI UNAVYOJITENGENEZEA KUKOSA FURAHA KWA MAISHA YAKO YOTE.
“If you deliberately plan on being less than you are capable of being, then I warn you that you’ll be unhappy for the rest of your life.” – Abraham H. Maslow
Kinachowafanya watu wengi wakose furaha kwenye maisha yao ni hiki; wanaishi maisha ambayo yako chini ya uwezo wao. Yaani mtu anajijua kwamba anaweza kuwa na maisha bora kuliko aliyonayo sasa, anaweza kufanya kazi yake kwa ubora kuliko anavyofanya sasa na pia anaweza kupata kipato kikubwa kuliko anachopata sasa, lakini hakuna hatua anazochukua kufikia ule uwezo uliopo ndani yake.
Kanuni ya kutengeneza maisha ya hovyo, maisha yasiyo ya furaha kwa kipindi chote cha maisha yako, ni kupanga kuishi chini ya uwezo ulio ndani yako.
Ni bora upange kuishi kuliko uwezo wako, upange kufanya makubwa zaidi ya unavyoweza, na hata ukishinda basi utakuwa umeshindiwa juu ya pale ulipo sasa.
Lakini kama utapanga vitu ambavyo vipo nje ya uwezo wako kabisa, kama utaendesha maisha ya mazoea, yasiyo na mpango, maisha ya kusubiri mambo yatokee na wewe ndiyo uone utafanya nini, utakuwa na maisha yasiyo na furaha, maisha ya hovyo na utakuwa umechagua kuyapoteza maisha yako wewe mwenyewe.
Sehemu nzuri ya kuanza kuishi kulingana na uwezo wako au hata juu ya uwezo wako, ni kuchukua chochote unachofikiria sasa hivi na kuzidisha mara kumi. Kwa mfano chukua kipato unachoingiza sasa, kizidishe mara kumi na hilo ndiyo linapaswa kuwa lengo lako la kipato unalofanyia kazi. Angalia mipango yote uliyojiwekea, zidisha mara kumi na weka juhudi kuhakikisha unafikia mara kumi hiyo.
Hizo ndiyo tano za juma hili namba 39 kwa mwaka huu 2018, jifunze na kisha chukua hatua ili maisha yako yawe bora zaidi. Kumbuka popote ulipo sasa, unaweza kupiga hatua na kuwa bora zaidi. Hivyo kabla hujalianza juma la 40, panga yale unayokwenda kukamilisha kwa juma hilo, na usisahau kuzidisha mara kumi ili uweze kuchukua hatua kulingana na uwezo wako.
Makala hii imeandikwa na Kocha Dr Makirita Amani.
Dr. Makirita ni Daktari wa binadamu, Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.
Dr. Makirita anaendesha mafunzo ya mafanikio kwa wale waliojitoa hasa kufanikiwa kupitia program ya KISIMA CHA MAARIFA.
Kama bado hujajiunga na KISIMA CHA MAARIFA, tuma sasa ujumbe wenye maneno KISIMA CHA MAARIFA kwa njia ya wasap namba 0717 396 253 (tumia wasap tu)
Kupata huduma nyingine za ukocha tembelea www.amkamtanzania.com/kocha
Kupata vitabu vizuri vya kusoma tembelea www.amkamtanzania.com/vitabu