Maisha ni mfululizo wa vitu viwili vinavyojitokeza kila wakati, utulivu na machafuko. Utulivu ni pale vitu vinavyokwenda kama ambavyo tumepanga, vile ambavyo unategemea viende. Machafuko au vurugu ni pale vitu vinavyokwenda tofauti na tulivyopanga, tofauti na mategemeo yetu.

Ili kuweza kuendesha maisha yetu katika hali hizi mbili, tunahitaji kuwa na mwongozo, kuwa na sheria ambazo siyo kwamba zitatuzuia tusiingie kwenye machafuko, bali zitatusaidia pale tunapokuwa kwenye machafuko, yasitupoteze kabisa na kufanya maisha kuwa magumu.

Hapa ndipo mwandishi na mwanasaikolojia Jordan Peterson anapokuja na kitabu chake 12 RULES FOR LIFE, ambacho anatupa mbadala wa machafuko, msingi utakaotuwezesha kuendesha maisha yetu vizuri kwenye hii dunia yenye kila aina ya changamoto.

12 RULES

Lakini Jordan anatambua kitu kimoja, sisi binadamu hatupendi Sheria, hata kwenye vitabu vya dini, Moses alipotoka mlimani na amri alizopewa na Mungu, hakupokelewa kwa shangwe na vigelegele. Sheria au Amri zinaonekana kama kitu kinachotunyima uhuru na kukandamiza haki zetu.

Japokuwa kuna ukweli kiasi kwenye kukosa uhuru, bado sheria zina manufaa makubwa sana. Kwa sababu sisi binadamu tusipokuwa na mipaka, basi tunaweza kufanya mambo mabaya mno. Mfano mzuri ni kwenye uongozi wowote wa kidikteta, pale mtu mmoja anapoamini anajua kuliko wengine wote na hana haja ya kufuata sheria, hata kama ana nia njema, huwa mambo yanaishia kuwa mabaya. Mifano ipo mingi ya tawala za kidikteta na jinsi zilivyoleta madhara kwenye maisha ya watu.

Hivyo tukubali sheria mbalimbali, na tuone jinsi gani tunaweza kuzitumia kuwa na maisha bora kabisa kwetu na kwa wale wanaotuzunguka.

Karibu kwenye uchambuzi huu, tujifunze sheria hizi 12 ambazo kwa kuzifuata, tutaweza kuepuka na kupambana na changamoto mbalimbali kwenye maisha yetu ya kila siku.

12 RULES 1

SHERIA YA KWANZA; SIMAMA WIMA, MABEGA NYUMA.

Jinsi unavyouweka mwili wako, kuna maana kubwa sana kisaikolojia na hata wengine wanavyokuchukulia. Unaposimama wima ni dalili ya kujiamini na kuwa na nguvu, ukiinama ni ishara ya kutokujiamini. Kusimama wima pia ina maana ya kuchukua majukumu ya maisha yako.

 1. Mwonekano wako unaeleza mengi kuhusu wewe.

Kwa jinsi mtu anavyoonekana, unaweza kujua mengi kuhusu yeye kwa jinsi tu alivyo. Hii ni kuanzia kwa wadudu, wanyama na mpaka binadamu. Miili yetu huwa inatuma ujumbe kwa wengine, na hivyo watu wanatuchukulia kwa namna wanavyotuona.

Mtu anayesimama wima, akiangalia mbele na mabega yakiwa juu na nyuma anatuma ujumbe kwamba ni mtu anayejiamini, na mtu mwenye kujua nini anataka. Mtu anapokutana na mtu wa aina hii anatanguliza heshima kabla hata hajamjua kwa undani.

Mtu anayeinama, mabega yameshuka na anaangalia chini anatuma ujumbe kwamba ni mtu asiyejiamini na asiyejua nini anataka, mtu anapokutana na mtu wa aina hii hakuna heshima anayotanguliza na anaweza hata kuamua kumwonea au kumdhulumu.

Hivyo tunapaswa kuiweka miili yetu kwenye mwonekano wa ushindi, maana hili ni muhimu sana kwa maisha yetu.

 1. Madaraja kwenye jamii na matokeo yake.

Kwenye kila jamii, huwa kuna madaraja, hii ni kuanzia kwenye wadudu, wanyama na hata binadamu. Kuna ambao wapo daraja la juu na ambao wapo daraja la chini. Hii inaonekana kwenye kila eneo la maisha. Ni rahisi kuona haya ni madaraja tu, lakini matokeo yake ni makubwa sana.

Wale waliopo daraja la juu, maisha yao yanakuwa mazuri, wanakuwa na uwezo wa kupata kile wanachotaka na wanakuwa na usalama kiafya, hivyo wanaishi muda mrefu na kuwa na familia imara.

Wale waliopo daraja la chini, maisha yao yanakuwa siyo mazuri, wanakuwa na maisha ya mateso, hawapati wanachotaka na hata usalama wao kiafya unakuwa mdogo, hivyo wanaishi muda mfupi pia.

Na madaraja haya siyo tu kifedha, bali yanaanzia kwa namna mtu anavyojiamini na kujichukulia. Kwa mfano mtu wa daraja la juu akipata fedha anajua jinsi ya kuitumia vizuri na hata kuizalisha pia. Lakini mtu wa daraja la chini akipata fedha, hajui hata aitumieje, mwishowe anaishia kuitumia kwa njia ambazo ni hatari kwake kama ulevi na vitu vingine.

Unahitaji kuwa daraja la juu, kwa kuanzia kwenye fikra zako na matendo yako, kama unataka kupiga hatua kwenye maisha yako.

 1. Kubali majukumu ya maisha yako, japo ni magumu.

Maisha ni magumu, maisha ni mateso, kama siyo wewe unayeteseka, basi kuna ndugu yako wa karibu ambaye anateseka kwa magonjwa au hata hali nyingine kimaisha. Kinachotokea kwa wengi, wanapokuwa kwenye hali hizi za mateso huwa wanajaribu kukwepa majukumu, kukataa au kutafuta wengine wa kulaumu.

Kusimama wima na mabega nyuma inamaanisha kukubali changamoto za maisha yako kama zilivyo na kuona hilo ni jukumu lako, inamanisha kukubali hali ya vurugu na kuchukua hatua kuifanya kuwa utulivu, ina maana kwamba umechagua kutokumlaumu yeyote kwa kile kinachotokea kwenye maisha yako.

SHERIA YA PILI; JICHUKULIE KAMA MTU AMBAYE UNA WAJIBU WA KUMSAIDIA.

Watu wengi hujitoa sana pale wanapowasaidia wengine, lakini inapokuja kwao binafsi, wanapuuza. Mifugo yako ikiumwa haraka utaitafutia matibabu na kuhakikisha inapata matibabu, lakini wewe ukiumwa huhangaiki sana, na hata ukipewa dawa hutumii kwa umakini kama unavyoelekezwa.

 1. Kuku anapokuwa muhimu kuliko wewe.

Kitu kimoja ambacho kimekuwa kinawashangaza madaktari ni kwamba watu wanaopumwa, wakiandikiwa dawa za kutumia, huwa hawamalizi kutumia dawa hizo. Watatumia kidogo wakishapata nafuu hawaendelei tena kutumia. Lakini mtu huyo huyo, akiwa na mifugo na ikaumwa, akaenda kwa daktari wa mifugo na akapewa dawa, atahakikisha mifugo hiyo inapata dawa na kukamilisha bila kuacha.

Hapa ndipo utajiuliza je mifugo ni muhimu kuliko mtu mwenyewe? Lakini tunapoangalia ndani tunaona ni tabia ya mwanadamu kujali wengine kuliko anavyojijali yeye mwenyewe. Mtu mwingine anapokuwa chini ya uangalizi wetu, basi huwa tunafanya kila juhudi kuhakikisha yupo vizuri, lakini kwetu wenyewe, tunajichukulia kwa mazoea.

 1. Utulivu na machafuko ni vitu vinavyofuatana.

Huwa tunafikiri kwamba maisha ni utulivu pekee au machafuko pekee. Lakini huwezi kuyarahisisha maisha kwenye hali hizo mbili pekee. Maisha ni mfululizo wa utulivu na machafuko.

Upo kwenye utulivu pale unapokuwa na rafiki mwaminifu, lakini rafiki huyo anapokusaliti, unaingia kwenye machafuko. Unapokuwa na kazi yenye uhakika wa kipato ni utulivu, kazi hiyo inapoondoka au kipato kinapoacha kuwa cha uhakika ni machafuko.

Maisha yetu ni utulivu uliozungukwa na machafuko, tupo kwenye eneo dogo tunalojua, tukiwa tumezungukwa na eneo kubwa tusilolijua. Ili kuweza kwenda vizuri na maisha, lazima mguu mmoja uwe kwenye utulivu na mguu mwingine uwe kwenye machafuko, kujiandaa kwa chochote kinachoweza kutokea, maana chochote kinaweza kutokea.

 1. Pamoja na madhaifu yako, bado wewe ni muhimu.

Moja ya mambo yanayopelekea tusijijali sana, ni kwa sababu tunajijua sisi wenyewe kuliko mtu mwingine anavyotujua, kuliko tunavyowajua watu wengine. Hivyo tukijikumbusha madhaifu yetu, mabaya ambayo tumewahi kufanya huko nyuma, tunajiona tunastahili mateso na hivyo kutokujijali kama tunavyowajali wengine.

Tunaona sisi tuna hatia na wengine hawana hatia, na ndiyo maana tunaweza kuwasaidia wengine kuliko tunavyoweza kujisaidia sisi wenyewe. Tunapaswa kujikumbusha kwamba pamoja na madhaifu yetu, pamoja na mabaya ambayo tumewahi kuyafanya, bado tunastahili kujijali kama tunavyowajali wengine.

 1. Nguvu kubwa ya kukuongoza kwenye machafuko.

Wakati wa machafuko ndiyo wakati ambao wengi hupotea kabisa, ndiyo wakati ambapo ndoto nyingi huvunjika kabisa. Ili uweze kuvuka kipindi cha machafuko na hata kufanya vizuri kipindi cha utulivu, unahitaji kuwa na nguvu inayokuongoza. Na nguvu nzuri ya kukuongoza ni kuwa na maono makubwa ya maisha yako, maono ambayo yanatoka ndani yako, kuna msukumo ndani yako wa kukupeleka kwenye maono hayo. Kwa maono unayokuwa nayo, jione pale unapotaka kufika na kila siku ishi picha hiyo unayoiona.

Maono yako ndiyo yanayokupa sababu ya kuishi, na kama ambavyo mwanafalsafa Friedrich Nietzsche alivyowahi kunukuliwa akisema, yeyote mwenye sababu ya kuishi, anaweza kupambana na chochote.

SOMA; NYEUSI NA NYEUPE; Kuhusu Kufanya Kazi Kwa Nguvu Na Kufanya Kazi Kwa Akili.

SHERIA YA TATU; TENGENEZA URAFIKI NA WALE WANAOTAKA UWE BORA ZAIDI.

Watu unaojihusisha nao, wana mchango mkubwa sana wa wapi unafika. Kama unajihusisha na watu waliokata tamaa na maisha yao, hutaweza kupiga hatua kwenye maisha yako.

 1. Unakuwa wale wanaokuzunguka.

Dhana kwamba tabia yako na hata mafanikio yako ni wastani wa watu wako wa karibu imekuwepo kwa muda mrefu. Ndiyo maana mama au mlezi wako alikuambia ulipokuwa mdogo usicheze na watoto fulani, kwa sababu walikuwa na tabia mbaya. Sasa hili haliishii kwenye utoto tu, hata kwa watu wazima, tabia zetu zinaathiriwa na wale wanaotuzunguka.

Jama watu wanaokuzunguka wamekata tamaa na maisha yao, utajikuta na wewe unakata tamaa na maisha yako. Kama watu wanaokuzunguka ni watu wa kulalamika wakati wote, na wewe utajikuta unalalamika.

Na wakati mwingine siyo kwamba watu hao wamekubadili tabia, bali wamekutana na wewe kwa sababu tayari ulikuwa na tabia hizo au unawavumilia kwenye tabia zao hizo.

 1. Siyo kila anayeanguka anataka kuokolewa.

Wakati mwingine watu wanajenga urafiki na watu kwa sababu wanaona watu wale wanaanguka na wanataka kuwaokoa. Kinachotokea badala ya wao kuwaokoa wanaoanguka, wanajikuta wao wakianguka. Siyo kila anayeanguka anahitaji kuokolewa, hivyo kukimbilia kuwaokoa wanaoanguka, ambao ndiyo maisha wameyachagua, kunaweza kukuingiza wewe kwenye matatizo ya aina hiyo pia.

 1. Kitu cha kwanza kuangalia kabla hujamsaidia mtu.

Ukiona moshi unatoka mahali na ukakimbilia kuondoa moshi huo, hutazuia moshi kuendelea kutoka, kwa sababu kwa akili za kawaida kabisa, penye moshi, chini kuna moto. Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye matatizo ya watu, unapomwona mtu yupo kwenye matatizo, jua kuna kitu kimesababisha. Sasa ukikimbilia kumsaidia kuondokana na matatizo, bila ya kujua kwa nini ameingia kwenye matatizo hayo, msaada wako hautakuwa na maana.

Kabla hujamsaidia mtu, jua kwanza nini kimemuingiza kwenye matatizo aliyonayo. Na usikubali yale maelezo ambayo watu wanakupa, kwamba hawana hatia, kwamba hakuna chochote kibaya wamefanya. Kila tatizo ambalo mtu anapotia, kuna namna amelisababisha au amelichochea.

 1. Kigezo cha kuchagua marafiki.

Ili kufanikiwa kwenye maisha, ili kuepuka vurugu na machafuko kwenye maisha yako, unahitaji kuwa makini kwa marafiki unaowachagua, chagua marafiki ambao wanataka uwe bora, marafiki wanaokusukuma ukue zaidi ya hapo ulipo. Na marafiki hawa ni wale ambao nao pia wamepiga hatua au wanapiga hatua.

Sasa inaweza isiwe rahisi kujua kama ni watu waliopiga hatua au wanaopiga hatua, hivyo cha kwanza kuangalia ni tabia zao. hivyo kama una urafiki na mtu ambaye huwezi kumshauri kaka yako, dada yako, mzazi wako au mtoto wako awe na urafiki naye, basi huyo siyo rafiki sahihi kwako.

SHERIA YA NNE; JILINGANISHE NA ULIVYOKUWA JANA, NA SIYO NA JINSI MWINGINE ALIVYO LEO.

Haijalishi unafanya nini kwenye maisha, kuna mtu ambaye ni bora kuliko wewe, ukikazana ukawa na baiskeli, kuna wenye pikipiki, ukiwa na pikipiki kuna wenye magari, ukiwa na gari kuna wenye ndege. Hivyo kujilinganisha na wengine ni kujiumiza, jilinganishe na ulivyokuwa jana, kama leo uko bora kuliko ulivyokuwa jana basi unapiga hatua, haijalishi wengine wapoje.

 1. Ukubwa wa jamii zetu umefanya mashindano kuwa magumu sana.

Chukulia maisha ya kijijini ya zamani, ambapo kwenye kijiji kuna watu wachache, ambao karibu wote mnajuana. Kila mtu anajulikana kwa sifa yake, hivyo kijiji kizima kunaweza kuwa na fundi mwashi mmoja, kunaweza kuwa na mfua chuma mmoja na kadhalika. Ni rahisi kuwa bora zaidi ya wengine pale jamii inapokuwa ndogo.

Lakini jamii inapokuwa kubwa, dhana ya mashindano au ubora kuliko wengine inakuwa ngumu zaidi. Fikiria kwa zama hizi za mitandao ya kijamii, ambapo karibu dunia nzima imeungana, ni vigumu sana wewe kuwa bora zaidi ya wengine kwenye kitu chochote. Kwa sababu watu wa kujilinganisha nao ni wengi, na hivyo wengi wanaweza kuwa bora kuliko wewe, kwenye chochote unachofanya.

 1. Viwango vinahitajika.

Kwa kuwa kujilinganisha na wengine ni kitu kigumu kufanya, haimaanishi unaweza kufanya chochote unachojisikia kufanya wewe mwenyewe. Kwa sababu kitu kisipokuwa bora, kuna madhara. Fundi asipojenga nyumba kwenye ubora, inaweza kubomoka na kuua watu. Msanii asipotoa wimbo mzuri, watu wanakereka, mwandishi asipoandika kitabu kizuri, anapoteza muda wa wasomaji wake.

Pamoja na kwamba huhitaji kujilinganisha na wengine, lazima uwe na viwango na mara zote ufanye kwa ubora zaidi katika viwango vilivyopo.

 1. Labda siyo mchezo sahihi kwako.

Huwezi kuwa bora kwenye kila kitu, lakini unaweza kuwa bora kwenye maeneo machache. Lakini kama kwenye kile unachofanya, kile unachotaka kuwa bora, huoni nafasi za wewe kuwa bora, basi huenda siyo eneo sahihi kwako kuwa bora. Kama unacheza mchezo ambao ni mgumu kwako kushinda na hufurahii mchezo huo, basi huenda siyo mchezo sahihi kwako.

Hivyo kupata kile ambacho unaweza kuwa bora zaidi unahitaji kujaribu vitu vingi, na kuweka kila unachoweza kuweka kisha kuangalia matokeo unayopata. Na unapaswa kujua kwamba hakuna mchezo mmoja tu wa kushinda, bali ipo michezo mingi, hivyo ni wewe kuchagua mchezo upi unakufaa na kuweka juhudi kuwa bora zaidi.

Usisahau pia kama kila mchezo unaojaribu unakuwa siyo sahihi kwako, unaweza kuanzisha mchezo mpya na ukashinda, kwa sababu wewe ndiye uliyeuanzisha. Kwa kifupi usiingie eneo ambalo utakuwa unashindana na wengine, utaishia kuanguka vibaya.

SHERIA YA TANO; USIWARUHUSU WATOTO WAKO WAFANYE KITU AMBACHO KITAKUFANYA UWACHUKIE.

Watoto wa zama hizi wanakua hovyo bila ya malezi bora, wazazi wanaogopa kuwaadhibu watoto kwa kuhofia kuchukiwa na watoto hao. Lakini kitu chema ambacho mzazi anaweza kufanya kwa mtoto ni kutoa adhabu sahihi kwa makosa ambayo mtoto amefanya. Na kama mzazi hatafanya hivyo, kwa kufikiri anampenda mtoto wake, anamwandaa kuja kuadhibiwa na dunia, na dunia haina huruma, inaadhibu kikatili sana.

 1. Tatizo la wazazi wa sasa.

Wazazi wa zama hizi wana tatizo moja kubwa kwenye malezi ya watoto wao, wanawaogopa watoto wao. Wazazi wanawaogopa watoto kutokana na jinsi jamii zetu zilivyobadilika, na kuonekana kwamba malezi bora ni pale mzazi anapompa mtoto kila anachotaka, na asipompa basi hampendi au amemtelekeza. Pia kama mzazi atatoa adhabu kwa mtoto, basi anachukuliwa ni katili na asiyejali.

Hali hii imepelekea kuwepo kwa wimbi la vijana ambao wanakua bila ya msingi, ambao hawajaandaliwa kupambana na changamoto za maisha. Ambao wanafikiri dunia itakuwa inawapa kila wanachotaka, kama ambavyo wazazi wao walikuwa wanawapa.

Ni mpaka pale wanapoingia kwenye dunia halisi, ndiyo wanajifunza ukweli wa maisha, na wengi wanaishia kushindwa vibaya.

 1. Watoto wanaharibiwa kwa kukosa adhabu kuliko kuharibiwa na adhabu.

Kumekuwa na harakati nyingi za kufuta adhabu kwa watoto, kuanzia majumbani mpaka mashuleni. Ni harakati ambazo ukiziangalia kwa haraka zina maana kubwa, kwamba adhabu nyingi zinazotolewa kwa watoto haziwasaidii bali zinawaharibu, zinawadumaza, zinawafanya wakose kujiamini na kuua vipaji vyao, pale wanapoadhibiwa kwa kuwa tofauti.

Lakini unapokuja kuangalia kwa undani, unaona jinsi ambavyo adhabu zinawasaidia watoto kuelewa uhalisia wa dunia. Kwa sababu bila ya adhabu, wanakua wakijua kwamba dunia inapaswa kuwasikiliza wao, inapaswa kuwapa kila wanachotaka. Wanakua wakiwa na mtazamo mbovu, na wakiwa na mazoea mabaya, hivyo vinawafanya washindwe kufanikiwa kwenye maisha yao.

Adhabu, licha ya mapungufu yake, zinawafanya watoto wajenge tabia nzuri na wajiandae kukabiliana na dunia, ambayo adhabu zake ni kali kuliko zile zinazotolewa na wazazi. Hivyo wanajua wakija kukosea kwenye dunia, dunia inawaadhibu kwa ukatili kuliko wazazi walivyokuwa wanawaadhibu.

 1. Kumwadhibu mtoto ni wajibu, na isiwe hasira.

Kama mzazi, mtoto anapokosea anapaswa kuadhibiwa, kwa kadiri inavyoweza kumsaidia, lakini usifanye hivyo kwa hasira. Kwanza kabisa mzazi hapaswi kutoa adhabu kwa mtoto kwa hasira, kwa sababu hiyo itapelekea atoe adhabu ambayo siyo sahihi. Mzazi anapaswa kutoa adhabu kama sehemu ya upendo, kama sehemu ya kumfundisha mtoto awe na tabia njema.

Na adhabu siyo lazima iwe ya viboko au maumivu, inaweza kuwa ya kukosa kile ambacho mtoto anapenda, akijua kwa nini anakikosa, au hata kutengwa kwa muda ili ajifunze.

 1. Watoto wana tabia ya kujaribu ukomo wa tabia zao.

Watoto wadogo huwa wana tabia ya kujaribu ukomo wa tabia zao, wakitaka kujua ni kwa kiasi gani wanaweza kufanya kitu bila ya kufanya chochote. Hivyo huwa wanaanza na tabia mbaya ndogo, wasipoadhibiwa wanaongeza zaidi. Hivyo kama mtoto ataachwa kwa sababu amefanya kosa dogo, jua amejifunza kosa hilo halina adhabu, hivyo ataenda kwenye kosa kubwa zaidi.

Hivyo adhabu inapaswa kutolewa kwenye makosa madogo, ili mtoto ajifunze mapema. Pia adhabu inapaswa kutolewa wakati wa kosa, ili mtoto ajifunze.

 1. Sheria tano za kutoa adhabu kwa watoto.

Utoaji wa adhabu kwa watoto siyo jambo rahisi, linahitaji muda na uangalifu mkubwa ili mtoto ajifunze na kuwa na tabia bora. katika kusaidia hilo, unaweza kutumia sheria hizi tano;

Moja; sheria ziwe chache na zinazoeleka. Mtoto anapaswa kujua vitu gani anapaswa na hapaswi kufanya.

Mbili; tumia nguvu kidogo katika utoaji wa adhabu kabla ya kwenda kwenye nguvu kubwa zaidi, mfano kuanza na onyo, kisha adhabu ndogo na baadaye adhabu kubwa.

Tatu; wazazi wanapaswa kuwa wawili, kazi ya malezi ni kubwa, hivyo ni vigumu mzazi mmoja kuiweza vizuri. Watoto wanaolelewa na mzazi mmoja wanakuwa na changamoto nyingi kuliko wanaoelelewa na wazazi wawili.

Nne; wazazi wanapaswa kujua uwezo wao wa kuwa wakatili na wenye hasira na kujizuia kufikia hatua hiyo wanapotoa adhabu kwa watoto wao.

Tano; ni jukumu la wazazi kutengeneza jamii inayokuja, hivyo wanavyoadhibu watoto wao, siyo kwa sababu ya watoto wao tu, bali kwa sababu ya kujenga jamii bora. Maana mtoto anapokuwa na tabia mbaya, siyo tatizo kwa mzazi pekee, bali kwa jamii nzima.

SOMA; Mambo 20 Niliyojifunza Kutoka Kwenye Kitabu Cha The Truth About Innovation (Ukweli Kuhusu Uvumbuzi)

SHERIA YA SITA; WEKA NYUMBA YAKO SAWA KABLA HUJAKOSOA DUNIA.

Kila mtu anaweza kukosoa, kila mtu anaweza kutoa maoni yake namna gani mambo yanaweza kwenda vizuri zaidi, lakini kila mtu kuna kitu ambacho hafanyi kwa usahihi kwenye maisha yako. Kabla hujapoteza muda wako kuhukumu au kukosoa wengine, hebu kwanza angalia maisha yako kama kila kitu unafanya kwa usahihi. Kama siyo, tumia muda huo kurekebisha maisha yako badala ya kukosoa wengine.

 1. Maisha ni magumu na maumivu ni lazima.

Maisha ni magumu, ni magumu kwa kila mtu. Maumivu ni lazima na yapo kila mahali. Mara nyingi maumivu ni matokeo ya kile ambacho mtu amefanya ka kujua au kutokujua. Watu wanapata kile wanachostahili, ni ukweli ambao ni mgumu kumeza.

Hivyo hali yoyote unayopitia kwenye maisha, kabla hujamwangalia mwingine yeyote, anza kujiangalia wewe mwenyewe kwanza. Kwa sababu huwa tunazoea vitu, tunakazana kuvipata kisha tunaviozea, na tukishavizoea vinaanguka na hapo ndipo tunashindwa kuelewa dunia inaendaje.

 1. Safisha maisha yako.

Angalia kila hali unayopitia kwenye maisha yako, hata kama ni ndogo kiasi gani, je unafanya kila unachoweza kufanya? Umeweza kutumia kila fursa inayokuzunguka? Unaweka juhudi za kutosha kwenye kazi yako? je umepatana na wale ambao mmepishana? Je unaijali familia yako? Je unayabeba majukumu yako kwa ukamilifu? Je umesema kile ulichotaka kusema kwa watu wako wa karibu? Je umeyasafisha maisha yako?

Kama jibu ni hapana kwenye swali lolote unalojiuliza kuhusu maisha yako, acha kufanya kile ambacho siyo sahihi, acha kufanya sasa. Anza kufanya kile ambacho ni muhimu, ambacho ndiyo kinastahili muda wako.

 1. Kabla hujataka kuibadili dunia, anza na hapa.

Anza na maisha yako, anza kuyanyoosha maisha yako kabla hujapanga kunyoosha maisha ya wengine. Kama huwezi kuleta amani ndani ya familia yako, kipi kinakufanya ufikiri unaweza kuleta amani kwenye nchi?

Acha kufanya yale ambayo unajua siyo sahihi kwako kufanya, anza kufanya yale ambayo unajua ni muhimu kwako kufanya. Na anza na pale ulipo, kabla hujaanza kufikiria mbali.

Hata matatizo tunayokutana nayo kama nchi na dunia kwa ujumla, ni pale watu ambao hawajaweza kusafisha nyumba zao, wanataka kuisafisha dunia, kinachozalishwa ni majanga.

SHERIA YA SABA; FANYA KILE CHENYE MAANA KWAKO, NA SIYO KILICHO RAHISI.

Kuna njia rahisi ya kupata chochote ambacho unataka kwenye maisha, lakini njia rahisi siku zote huwa zinakuja na madhara yake baadaye. Hivyo kwa chochote unachotaka kwenye maisha, tumia njia sahihi na fanya kitu chenye maana kwako, siyo kwa sababu kila mtu anafanya.

 1. Upo tayari kutoa nini?

Kwa jinsi maisha yalivyo, huwezi kupata kile unachotaka kama haupo tayari kutoa kile unachokipenda zaidi. Maisha ni kutoa kafara, kupata unachotaka lazima uingie gharama, lazima uweke nguvu na muda, lazima uachane na vile unavyopenda, na hili ndiyo wengi hawawezi.

Chochote kizuri kwenye maisha kinahitaji kazi, na kazi ndiyo kafara ya kwanza ambayo kila mtu anapaswa kutoa ili kufanikiwa. Hivyo kujaribu kutafuta njia isiyohusisha kazi, ya kupata kile unachotaka, ni kujidanganya.

 1. Upo tayari kukosa raha sasa lakini kupata furaha baadaye?

Unaweza kupata raha sasa hivi, lakini raha hiyo huwa ni kikwazo cha furaha ya baadaye. Mfano unaweza kutumia muda wako kuangalia tv, kufuatilia mitandao ya kijamii ambapo unapata raha, lakini hilo litakuzuia kufanya kazi ambayo itakuletea mafanikio baadaye.

Kuweza kupata matokeo mazuri ya baadaye, katika kupata furaha baadaye, lazima uteseke sasa, lazima ukae mbali na raha za muda mfupi ndiyo uweze kupata furaha ya baadaye.

 1. Kuna wakati mambo hayataenda vizuri.

Pamoja na kwamba ukiacha kupata raha sasa, unajiandaa kupata furaha baadaye, pamoja na kwamba ili upate unachotaka unahitaji kutoa unachopenda na kuthamini, siyo kila wakati mambo yataenda kama unavyotaka yaende.

Kuna wakati utajitesa na bado baadaye usipate unachotaka. Kuna wakati utatoa kafara lakini usipate matokeo bora. Hii ni kwa sababu dunia inaenda kama inavyoenda, na siyo kama tunavyotaka sisi.

Unapokutana na hali kama hiyo usikate tamaa, bali jua kuna mambo umeyafanya ambayo hayaendani na jinsi dunia inavyoenda.

 1. Maumivu na mateso ndiyo yanaitengeneza dunia.

Kama mafanikio yangekuwa rahisi, kila mtu angekuwa nayo na kusingekuwa na cha kuwasukuma watu kuwa bora zaidi. Ni maumivu na mateso ndiyo yanawasukuma watu kuchukua hatua, kutaka kuondokana nayo, kutaka kuwa bora zaidi na hili linapelekea watu kupiga hatua zaidi.

 1. Kinachofanyika haraka hakidumu.

Chochote utakachofanya kwa haraka, chochote ambacho ni rahisi na kimetengenezwa kwa njia ya mkato, huwa hakidumu.

Kinachodumu ni kile chenye maana, ambacho mtu ameingia maumivu na mateso kukifanyia kazi, ambacho mtu amejitoa na ametoa kafara kukipata.

SHERIA YA NANE; SEMA UKWELI, AU ANGALAU USIDANGANYE.

Watu hupenda kutumia uongo kuwahadaa wengine ili kupata chochote wanachotaka. Imefika hatua watu mpaka wanajihadaa wenyewe. Njia bora ya kuishi maisha ni kuwa mkweli, au kutokudanganya wengine au kujidanganya mwenyewe.

 1. Kwa nini watu wanasema uongo?

Watu wanasema uongo kwa sababu wanasukumwa na matakwa ya kuwa sahihi, kutaka kushinda ubishani, kutaka kuonekana kwa namna fulani mbele ya wengine. Watu hutumia lugha kutengeneza picha ambayo siyo ya kweli, ili tu kupata kile ambacho wanakitaka.

Njia hiyo ya kupata unachotaka inaweza kuleta ushindi, lakini huwa inaharibu sifa ya mtu, na hivyo baadaye kuwa vigumu kupata mtu anachotaka.

 1. Uongo unadhoofisha tabia yako.

Kinachokujenga wewe, kinachokutambulisha kwa wengine, kinachofanya wengine wakuamini na kukutegemea ni tabia yako. lakini pale unapokuwa mwongo, unapofanya vitu ambavyo siyo kweli ila tu unataka wengine waone kitu fulani, unadhoofisha tabia yako na watu wanaacha kukuamini, wanaacha kukutegemea na utakaribisha majanga zaidi kwenye maisha yako.

 1. Kutokusimamia kile unachoamini ni uongo pia.

Kama watu wanakosea, kwa eneo ambalo upo, lakini huthubutu kusema makosa yao, hata kama ni watu wa juu kwako, ni kuishi maisha ya uongo. Kama kinachofanyika siyo sahihi na wewe unajua, ila unakaa kimya, ukiamini kitapita, ni kuishi uongo na kutengeneza matatizo zaidi kwa baadaye.

Simamia kile unachoamini, hata kama kina gharama, kwa sababu kuishi kwa njia nyingine ni kuishi maisha yasiyo na maana. Watu wanaotekeleza matendo ya kikatili kwenye tawala za mabavu ni watu wema, ambao wanaogopa kusimamia ukweli, wanajua wanachofanya siyo sahihi, ila hawathubutu kukataa na hivyo kuwa sehemu ya uharibifu.

 1. Ona ukweli, sema ukweli.

Mafanikio yapo kwenye ukweli, ukombozi wa dunia upo kwenye ukweli, ukweli unawapa chakula masikini, unafanya mataifa kuwa tajiri, ukweli unatengeneza marafiki badala ya maadui, ukweli ni nuru kwenye giza. Popote ulipo, ona ukweli na sema ukweli.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; BLINK, The Power Of Thinking Without Thinking (Nguvu Ya Kufikiri Pasipo Kufikiri)

SHERIA YA TISA; CHUKULIA KWAMBA MTU UNAYEMSIKILIZA KUNA KITU ANACHOJUA WEWE HUJUI.

Kusikiliza ni kazi ngumu, inahitaji kuwa mtulivu, kuacha vitu vingine vyovyote, kitu ambacho wengi hawawezi. Njia bora ya kuwa msikilizaji ni kuchukulia kwamba kila unayemsikiliza kuna kitu muhimu anajua ambacho wewe hujui. Na ukweli ni kwamba, kuna cha kujifunza kwa kila mtu.

 1. Kusikiliza ni kazi.

Kusikiliza siyo kukaa kimya pale mtu anapoongea, bali ni kujiweka kwenye viatu vyake, kuelewa kile anachosema, kuona lugha ya matendo anayotumia, na kumfanya mtu ajisikie huru kujieleza mbele yako.

Ukiweza kusikiliza vizuri, watu watakuwa tayari kukuambia kila unachotaka kujua. Hii ni kwa sababu watu wengi hawajawahi kupata nafasi ya kusikilizwa, unapotoa nafasi hiyo, wanaitumia vizuri.

 1. Kufikiria ni kugumu zaidi.

Watu wapo tayari kufanya chochote, lakini kuepuka kitu kimoja, kufikiri, hasa kufikiri kwa kina. Hata wale wanaokaa chini na kusema wanafikiria, au kusema wana mawazo, wanachofanya siyo kufikiria, bali wanachofanya ni kuhukumu au kujikosoa wao wenyewe.

Kufikiria ni kujisikiliza wewe mwenyewe, ni nafsi mbili ndani yako, moja inaongea na nyingine inasikiliza, unaweza kuelewa kwa nini kufikiria ni kugumu. Kwa sababu kuwa na nafsi mbili ndani yako, ambazo zinapingana, ni kitu ambacho wengi hawawezi kuvumilia na hivyo kuacha kabisa kufikiri.

 1. Hekima inatoka kwa wengine.

Jisikilize wewe mwenyewe na wasikilize wengine pia. Hekima haitoki kwenye kile unachojua tayari, bali inatoka kwenye yale unayojifunza kwa wengine. Jua kwamba kwa kila mtu kuna kitu unachoweza kujifunza, na sikiliza kwa makini, maana kila mtu kuna kitu anajua ambacho wewe hujui.

SHERIA YA KUMI; KUWA MAKINI KWENYE KAULI ZAKO.

Sema kile unachotaka kusema, sema kwa njia ambayo unaeleweka. Usitoe maelezo ambayo hayaeleweki au yanapingana. Ukiwa makini kwenye kauli zako, utajiepusha na matatizo mengi.

 1. Hatuioni dunia kama ilivyo, bali tunaona kile tunachotaka kuona.

Dunia ni kubwa, dunia ni ngumu, tukitaka kujua na kuona kila kitu, tutashindwa kuendesha maisha yetu. Hivyo tunachagua kuona kile ambacho tunataka kuona, ambacho tuna matumizi nacho kwa wakati huo. Ni mpaka pale mambo yanapokwenda tofauti na tunavyofikiria ndipo tunaona yale ambayo tulikuwa hatuyaoni, ambayo yapo mbele yetu wakati wote.

 1. Mambo yanapoharibika, yanayopuuzwa ndiyo huonekana.

Pale kila kitu kinakwenda kama kinavyotegemewa kwenda, mapungufu madogo madogo huwa hayaonekani, yapo mengi yanayopuuzwa ambayo hayaonekani. Ni mpaka mambo yanapoharibika, pale matokeo yanapokuwa tofauti na mategemeo, ndipo mapungufu yanaonekana, yale yaliyokuwa yanapuuzwa yanaonekana wazi.

 1. Kama kitu hakipo sahihi, kirekebishe kabla mambo hayajaharibika.

Wakati mzuri wa kubadili mambo yaliyoharibika ni kabla hayajaharibika, na unaweza kufanya hivyo kwa kuchukua hatua kwenye mambo madogo ambayo hayana madhara na yanaweza kupuuzwa, lakini baadaye yanatengeneza madhara makubwa.

Usifiche chochote kwa sababu ni kidogo, kwa sababu chochote kidogo kinakua, na kikishakua inakuwa vigumu kukifanyia kazi bila kuacha madhara.

 1. Sema kila unachomaanisha.

Ili kupata kile unachotaka, sema kile unachomaanisha, fanya kama unavyosema ili kujua nini kinatokea, angalia kila unachofanya, ona makosa unayofanya, rekebisha makosa yako na songa mbele. Hivi ndivyo unavyoweza kutengeneza maana kwenye maisha yako.

SHERIA YA KUMI NA MOJA; USIWASUMBUE WATOTO WAKIWA WANACHEZA MICHEZO INAYOONEKANA NI HATARI.

Zama hizi, watoto wamekuwa wanalindwa sana, michezo mingi imekuwa inazuiwa kwa sababu ya hatari zake. Lakini licha ya kuondoa hatari hizo, bado watoto wamekuwa wakitafuta njia hatari za kucheza. Ili kuwakuza watoto ambao wanajiamini na kuyaelewa maisha, wanahitaji kujihusisha na mambo hatari, hayo yatawafundisha sana.

 1. Vijana wa zama hizi wanateseka.

Katika zama hizi, vijana wanateseka sana. Wanajikuta kwenye wakati mgumu na kutokujitambua kwa sababu wamepata malezi ambayo yalikuwa yanawalinda kuliko kuwafanya kuwa imara. Wanalelewa kwenye mazingira yanayowaepusha na hatari na kinachotokea ni kutokujifunza mpaka wanapokutana na hatari halisi kwenye maisha.

 1. Mfumo dume hautengenezwi na wanaume.

Kumekuwa na dhana kwamba, mfumo dume ni mbinu ya wanaume kuwatawala na kuwanyanyasa wanawake. Ipo dhana pia kwamba wanaume ni katili na wasiojali wanawake. Lakini hii yote ni kutafuta majibu rahisi kwenye maswali magumu.

Ukiangalia historia ya mwanadamu, utaona kwamba majukumu ya wanawake na wanaume yaligawanywa kulingana na uhitaji wa jamii. Jamii ilihitaji wanawake kuwa karibu na watoto kwa ajili ya malezi, na hivyo kuwa na mwanaume ambaye anaweza kulisha familia.

Kwa sasa mambo yamebadilika, ambapo mwanamke hahitaji tena kumtegemea mwanaume kwa kila kitu, na hapo ndipo lawama za kila kilicho kibaya kwenda kwa wanaume. Wakati mfumo unaopingwa sasa, ulikuwa na manufaa kipindi ambacho maisha yalikuwa magumu kwa wanadamu.

 1. Jamii inawategemea wanaume kuwa imara.

Licha ya zama kubadilika, bado wanaume kwenye jamii wanapimwa kwa uimara, iwe ni kwa utajiri walionao, miili yao, akili na mengine yanayopimika kwa nje. Tafiti zinaonesha kwamba hata wanawake ambao wanaweza kuendesha maisha yao bila kutegemea wanaume, bado wanahitaji kuwa na wanaume ambao wanaweza kuwategemea.

Wanaume wanakuwa imara kwa kupitia mazingira hatari, ambayo yanaanza kujengwa tangu utotoni kupitia michezo wanayoshiriki.

SHERIA YA KUMI NA MBILI; MBEMBELEZE PAKA UKIKUTANA NAYE.

Kuna vitu vidogo vidogo kwenye maisha ambavyo huwa hatuvipi mkazo, lakini kwa kuvifanya vinakuwa na maana kubwa sana kwetu. Angalia ni vitu gani vidogo vidogo umekuwa unavichukulia poa na anza kuvifanya kwa umakini.

 1. Tabia kuu mbili za watu.

Watu wana tabia kuu mbili, kwanza watu ni viumbe wa kijamii kwa sababu wanawapenda na kuwajali watu ambao wapo ndani ya kundi moja. Pili watu siyo viumbe wa kijamii kwa sababu hawawajali wale ambao hawapo nao kundi moja.

Upendeleo ni tabia ya kawaida ya binadamu, watu huanza kuwajali wale ambao wapo nao kundi moja kabla ya kuwajali walio kwenye kundi tofauti.

 1. Msingi mkuu wa dini na falsafa zote.

Msingi mkuu wa dini na falsafa zote ni huu; MAISHA NI MATESO. Katika kuendesha maisha yetu tunakutana na changamoto mbalimbali, ambazo bila ya kuwa na njia sahihi ya kuzivuka, zinatuangusha.

 1. Udhaifu wetu ndiyo umuhimu wetu.

Fikiria kuwa mtu ambaye hafi, yupo kila mahali na anaweza kufanya kila kitu, kiumbe huyu anakuwa anakosa kitu kimoja, ukomo. Kitu chochote ambacho hakina ukomo, hakina madhaifu ni kitu kisichokuwa na matumizi.

Umuhimu wetu sisi binadamu unatokana na ukomo na madhaifu yetu. Tunajua tutakufa ndiyo maana tunaishi vizuri, tunajua hatuwezi kila kitu ndiyo maana tunakuwa bora kwenye vitu vichache, tunajua maisha ni magumu na hivyo tunakuwa imara zaidi.

 1. Maisha lazima yaendelee.

Je unaugua ugonjwa ambao hauna tiba? Je unamuuguza mtu wa karibu ambaye ana ugonjwa usio na tiba? Je una kitu kinachokuzuia usiishi vile unavyotaka? Jua kitu kimoja, haijalishi unapitia nini, maisha lazima yaendelee. Tenga muda wa kufikiria na kufanyia kazi zile changamoto unazoendelea nazo kwenye maisha yako, kisha endelea na maisha yako mengine, fanya yale mengine muhimu.

 1. Angalia vitu vidogo vyenye maana.

Pamoja na ugumu wa maisha, pamoja na changamoto nyingi unazoweza kuwa unapitia kwenye maisha yako, kuna vitu vingi vizuri vinavyokuzunguka, ambavyo ukiviangalia utaona namna ambavyo maisha yana maana kubwa. Unaweza kutenga dakika kumi za muda wako kufanya chochote unachopenda kufanya, hata kama hakina matokeo makubwa kwako, labda kuangalia vichekesho, au kuangalia wanyama ambao wanafanya yale ambayo ni muhimu kwao.

Maisha ni magumu, hivyo usikazane kuzidisha ugumu wake, angalia vitu vidogo vidogo ambavyo vitakupa maana zaidi ya maisha kwa ujumla.

Hizo ndiyo sheria 12 za maisha, ambazo ukizifuata kwa kina, utajiepusha na matatizo mengi kwenye maisha yako. japokuwa watu hatupendi sheria, hasa tunapolazimishwa kuzifuata, hizi ni sheria 12 ambazo unaweza kuchagua kuzifuata wewe mwenyewe. Ukaangalia jinsi unavyoweza kuzitumia kwenye maisha yako ili uweze kufanya yale muhimu na yenye maana kwako.

Pata kitabu hichi na kisome, zijue sheria hizi, kwenye kitabu Dk Jordan ametoa mifano na hadithi nyingi sana kufafanua sheria hizi. Ni kitabu ambacho kila aliye makini na maisha anapaswa kukisoma.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz

Usomaji