Rafiki yangu mpendwa,

Kosa la kwanza na kubwa kabisa tunalifanya kwenye maisha yetu ni kujidanganya sisi wenyewe. Sisi binadamu huwa hatupendi kuukabili ukweli ulivyo, kwa sababu ukweli unauma na haubembelezi. Hivyo kwa kuwa hatuwezi kuukabili ukweli, basi tunajidanganya.

Moja ya maeneo ambayo tumekuwa tunajidanganya sana ni maamuzi tunayofanya kwenye maisha yetu. Huwa tunajiambia tumefanya maamuzi sahihi na kwa kufikiri, lakini ukweli ni sehemu kubwa ya maamuzi tunayofanya siyo sahihi, na kinachopelekea yasiwe sahihi ni kwa sababu tunayafanya kwa hisia na siyo kufikiri.

Sisi binadamu ni viumbe wa kihisia na siyo wa kufikiri kama tunavyofikiri. Msingi wetu wa kwanza katika kufanya maamuzi yoyote yale unaanza na hisia. Labda kuna kitu tunatamani kuwa nacho na hivyo tunasukumwa kuchukua hatua ili kukipata. Au kuna kitu ambacho kinatuumiza na hivyo tunachukua hatua ili kukiondoa.

Hisia hizi mbili, tamaa na maumivu ndiyo zinaendesha asilimia 99 ya maamuzi ambayo tunayafanya kila siku. Na mbaya zaidi, huwa tunafanya kwanza maamuzi kwa hisia, kisha baadaye tunajihalalishia kwa kufikiri, kitu ambacho kinafanya tuzidi kujidanganya na kushindwa kufanya maamuzi sahihi.

rational-nonrational-irrational

Hali hii ya kufanya maamuzi kwa hisia badala ya kufikiri tumeirithi kutoka kwa watangulizi wetu ambao waliishi miaka mingi iliyopita na katika mazingira mabovu sana. Fikiria binadamu ambaye aliishi karne ya tano, ambapo alikuwa akiishi porini na wanyama, kama alikuwa porini na kusikia kishindo asichokielewa, njia pekee ya kupona ilikuwa ni kuchukua hatua haraka, na siyo kuanza kujiuliza kishindo hicho ni cha nini. Katika maisha hayo magumu na mazingira yasiyo salama, kufanya maamuzi kwa hisia kulikuwa na manufaa kwa mwanadamu.

Lakini kwa zama tunazoishi sasa, zama za sayansi na teknolojia, zama za maarifa, tunaishi kwenye mazingira salama mno, lakini bado tunafanya maamuzi yetu kwa hisia.

Kwa kufanya maamuzi kwa hisia kwenye zama hizi, ni hasara kubwa sana kwetu, wale watu wanaoweza kubonyeza hisia sahihi kwetu, wananufaika sana kupitia sisi. Mfano mzuri ni wafanyabiashara, wanajua bila ya kuibua tamaa au maumivu ndani yako hutanunua wanachouza. Hivyo wanatumia kauli ambazo zitaibua hisia ndani yako, kauli kama; ‘nafasi au bidhaa zimebaki chache, wahi kabla hujakosa’, au ‘kila mtu anatumia kitu hiki, usikubali kupitwa’, zote zinaibua hisia ndani yetu na kutusukuma tuchukue hatua, hata kama kitu hatukihitaji kweli.

Mwandishi Robert Green ambaye ametumia muda wake mwingi kujifunza asili na tabia zetu sisi binadamu, ametushirikisha kwa kina sheria kumi na nane za asili ya binadamu kwenye kitabu chake cha LAWS OF HUMAN NATURE. Katika kitabu hiki, sheria ya kwanza ametuonesha jinsi ambavyo hatufanyi maamuzi kwa kina, jinsi tunavyosukumwa na hisia na akatupa hatua tatu za kutuwezesha kutawala hisia zetu na kuweza kufanya maamuzi kwa usahihi.

Hapa nakwenda kukushirikisha hatua tatu zitakazokuwezesha kutawala hisia zako na kufikiri kwa usahihi ili kuepuka kufanya maamuzi mabovu.

HATUA YA KWANZA; TANBUA UPENDENDELEO ULIONAO.

Kikwazo cha kwanza kwenye kufikiri kwa usahihi na kufanya maamuzi sahihi ni upendeleo ambao tunao. Kila mmoja wetu kuna vitu anapendelea zaidi ya vingine. Na tunapokuwa na upendeleo, huwa tunajihalalishia kile tunachofanya hata kama siyo sahihi.

Hivyo hatua ya kwanza ya kufikiri kwa usahihi ni kutambua upendeleo unaotumia kwenye maamuzi na kuacha kutumia upendeleo huo.

SOMA; UCHAMBUZI WA KITABU; 12 RULES FOR LIFE (Sheria 12 Za Maisha, Mbadala Wa Machafuko).

Kuna aina mbalimbali za upendeleo ambazo tumekuwa tunazitumia kwenye kufanya maamuzi yetu. Upendeleo huo ni kama;

 1. Upendeleo wa uthibitisho, hapa unatafuta taarifa au ushauri ambao unathibitisha kile unachotaka wewe. Mara nyingi huwa tunakuwa na kitu tunachotaka kufanya, lakini hatuna uhakika, hivyo tunatafuta taarifa au ushauri unaothibitisha kwamba kitu hicho ni sahihi. Na kwa zama hizi za taarifa, hutakosa taarifa inayokubaliana na unachotaka kufanya, hata kama siyo sahihi.
 2. Upendeleo wa kuamini, hapa unakubaliana na kitu kwa sababu tu unaamini hivyo. Imani yako inakufanya uone kwamba kitu hicho ni sahihi. Tunachopaswa kuelewa ni kwamba kama unaanza na kuamini, kila kinachoendana na imani yako kitakuwa sahihi.
 3. Upendeleo wa mwonekano, huwa tunadanganywa na mwonekano wa nje, pale ambapo mtu au kitu kinaonekana kizuri kwa nje, tunaamini ni sahihi. Tunapaswa kujua kwamba hakuna kitu kinachodanganya kama mwonekano wa nje, na kama tunataka kuupata ukweli basi tuchimbe ndani zaidi.
 4. Upendeleo wa kundi, kama kile ambacho tunataka kufanya kuna wengine wanafanya, huwa tunaamini ni sahihi, hata kama siyo. Waswahili wanasema kifo cha wengi ni harusi, au penye wengi hapaharibiki jambo, lakini siyo sahihi. Mara nyingi kinachofanywa na wengi huwa siyo sahihi.
 5. Upendeleo wa kulaumu, wakati mwingine tunafanya maamuzi kwa ajili ya kuwalaumu wengine. Tunajiona kama wanyonge ambao hatuna kitu cha kufanya kwa kuwa wengine wametuzuia au kutukwamisha kwenye kile ambacho tunataka kufanya. Tunapaswa kujua kwamba hakuna tunayeweza kumlaumu kuhusu maisha yetu ila sisi wenyewe.
 6. Upendeleo wa ubora, inapofika kwenye kufanya maamuzi, huwa tunaamini sisi ni bora kuliko wengine, tunajiambia sisi ni wasafi kuliko wengine na ni tofauti na wengine. Hivyo tunaamini kwa ubora wetu na usafi wetu, hatuwezi kufanya makosa ambayo wengine wanafanya, na hilo linapelekea kurudia makosa ambayo wengine wamekuwa wanafanya. Lazima tujue udhaifu wetu uko wapi na kuukabili ili tuweze kufanya maamuzi bora.

HATUA YA PILI; JIHADHARI NA VITU VINAVYOIBUA HISIA NDANI YAKO.

Tunapofanya maamuzi kwa hisia, huwa haitokei tu tukawa tumefanya maamuzi hayo, bali kumekuwa na vichocheo ambavyo vinaibua hisia ndani yetu na kupelekea sisi kufanya maamuzi kwa hisia hizo.

Ili kuondokana na hali hii ya kufanya maamuzi kwa hisia na kuweza kufikiri kwa kina, tunapaswa kujua vitu vinavyoibua hisia ndani yetu ili tuweze kujihadhari navyo.

Vifuatavyo ni baadhi ya vitu ambavyo vimekuwa vinaibua hisia ndani yetu, ambavyo tunapaswa kujihadhari navyo;

 1. Kumbukumbu za utotoni. Utoto ni wakati mgumu sana kwa kila binadamu, ni wakati ambao unataka kupata kila kitu lakini kutokana na mazingira au wazazi uliokuwa nao, kuna vitu ambavyo ulivikosa wakati wa utoto. Huwa unaenda maisha yako yote ukitamani sana kupata vitu hivyo. Na katika utu uzima, akitokea mtu au hali ya kukupa kile ulichokosa utotoni, utamwamini na kukubaliana naye. Mfano watu ambao hawakupata mapenzi mazuri ya wazazi utotoni, huwa inakuwa rahisi kwao kuingia kwenye mahusiano ambayo mwenza wao atampa mapenzi kama ya baba au mama, aliyokosa utotoni.
 2. Kupata au kupoteza ghafla. Pale ambapo mtu unapata matokeo mazuri kwa ghafla, au unapoteza kwa ghafla, akili zetu zinaacha kufikiri kwa usahihi, na hapa ndipo tunapokuwa kwenye hatari ya kufanya maamuzi mabovu ambayo yanatugharimu zaidi. Mfano mzuri ni wacheza kamari, akiweka fedha na akapata fedha zaidi, anaamini anajua, hivyo anaendelea kucheza mpaka inafika hatua anapoteza fedha nyingi alizopata. Na anapoliwa fedha alizoweka, anaendelea kucheza, atakuwa tayari kuuza hata nguo alizovaa ili tu aendelee kucheza akiamini ataokoa fedha alizoliwa. Kwenye maisha hali ni hivyo pia, mtu akifanikiwa kwa ghafla anajiona ameshajua kila kitu, anaanza kufanya maamuzi kwenye maeneo ambayo hana uzoefu nayo na anashindwa vibaya. Kadhalika mtu akipoteza ghafla, wengi hukata tamaa na kuona hakuna haja ya kujaribu tena. Tunapaswa kuepuka kufanya maamuzi makubwa mara baada ya kupata au kupoteza kwa ghafla.
 3. Shinikizo linalokua. Mara nyingi tunapokuwa na shinikizo fulani ambalo linakua, huwa tunashindwa kufikiri kwa kina na kufanya maamuzi. Ndiyo maana wale ambao wanataka tufanye maamuzi ya haraka yatakayowanufaisha wanatuweka kwenye shinikizo fulani, labda ni muda unaisha, au kitu kinaisha na hivyo tunaona tunapoteza. Epuka sana kuwa kwenye shinikizo lolote lile kama unataka kufanya maamuzi sahihi.
 4. Watu wanaochochea hisia. Kuna watu ambao ni mafundi katika kuchochea hisia za wengine. Hawa ni watu ambao ukikaa nao baada ya muda unajikuta ukiwa na hisia kali sana, zinaweza kuwa hisia za furaha, au hisia za chuku kulinga na mapenzi yako kwa mtu huyo au kwa namba usivyompenda. Unapaswa kuwa makini na watu hawa, kwa sababu watakupelekea kufanya maamuzi mabovu. Na wengine wanaibua hisia ndani yako kwa makusudi ili ukosee na wao wanufaike.
 5. Msukumo wa kundi. Hii ni hali ya juu ya upendeleo wa kundi ambao tumejifunza hapo juu. Kwa kuwa ndani ya kundi, unashawishika kufanya kile ambacho waliopo ndani ya kundi hilo wanafanya, hata kama ukiwa peke yako usingeweza kufanya. Hivi ndivyo watu wanajikuta wakifanya fujo kwa kuwa ndani ya kundi, lakini peke yao wasingeweza. Pia kuwa ndani ya kundi kumekuwa kunaibua hisia ambazo ukiwa nazo mwenyewe huwezi kuwa nazo. Hivyo epuka sana makundi ambayo yanaibua hisia ndani yako ili ufanye maamuzi fulani yanayokugharimu.

HATUA YA TATU; MIKAKATI YA KUELEKEA KWENYE KUFIKIRI KWA USAHIHI.

Tunaweza kuwagawa wanadamu katika makundi mawili;

Kundi la kwanza ni wale ambao wanaongozwa na hisia katika kufanya maamuzi yao, hawa ni wengi sana na ndiyo wanaojikuta kwenye matatizo makubwa kwao na kwa wengine. Matatizo yote ambayo tunayaona hapa duniani, yamesababishwa na wale ambao wanafanya maamuzi kwa kutumia hisia.

Kundi la pili ni wale ambao wanaongozwa na fikra katika kufanya maamuzi, hawa ni wachache na ndiyo wanaoleta suluhisho la matatizo yanayotengenezwa na wanaoongozwa na hisia.

Wale wanaoongozwa kwa fikra, kuna wakati wanajikuta wakiingiwa na hisia, lakini wanajitambua na kuzizuia zisiwe na madhara kwao. Lakini wale wanaoongozwa kwa hisia, hata wakipata fikra, huwa wanatumia hisia kwanza halafu fikra baadaye.

Ili uweze kufanya maamuzi sahihi, uweze kuwa na maisha bora na yenye mafanikio, unapaswa kuwa mtu unayeongozwa na fikra, ambaye unafanya maamuzi kwa kufikiri kwa akili yako na kuepuka hisia zako kuingilia maamuzi hayo.

SOMA; Makosa 28 Ya Kisaikolojia Unayofanya Na Yanayopelekea Wewe Kufanya Maamuzi Mabovu Yanayokugharimu.

Ifuatayo ni mikakati itakayokuwezesha kuwa mtu wa kufanya maamuzi kwa fikra na siyo hisia;

 1. Jijue wewe mwenyewe kiundani. Hii ni kauli ambayo inatumika sana lakini wengi wamekuwa hawaielewi. Hatua ya kwanza ya kuelekea kuwa mtu wa kufikiri, ni kujijua wewe mwenyewe kiundani. Kujua maeneo yapi una uimara na nguvu na maeneo yapi una udhaifu. Watu wengi wamekuwa wanaendesha maisha yao kama wageni kwenye miili yao. Wewe usiwe hivyo, jijue wewe mwenyewe kwa undani na utaweza kuepuka matatizo mengi ambayo umekuwa unayatengeneza kwa kutokujijua.
 2. Chunguza msingi wa hisia zako. Hakuna mtu ambaye anaweza kuondokana na hisia kabisa. Hata wale wanaofanya maamuzi kwa fikra siyo kwamba wamezika kabisa hisia zao, ila wameweza kuzidhibiti. Hatua ya kwanza ya wewe kudhibiti hisia zako ni kuzielewa vizuri, kwa kuzichunguza mpaka kwenye mizizi yake. Angalia ni vitu gani vimekuwa vinaibua hisia ndani yako. Kila wakati unapokuwa kwenye hisia kali, jiulize nini kimekufikisha hapo. Kwa njia hii utajua vichocheo vya hisia kwako na kuviepuka wakati wa kufanya maamuzi.
 3. Ongeza muda wa kuchukua hatua. Kama unachukua hatua punde baada ya kitu kutokea au kupata wazo, jua hapo unasukumwa na hisia na siyo fikra. Ili uweze kufanya maamuzi kwa kufikiri kwa usahihi, lazima ujipe muda kwanza. Usikimbilie kuchukua hatua pale unapoona, kuambiwa au kufikiria jambo. Jipe muda wa kuendelea kulitafakari na kadiri muda unavyokwenda ndivyo hisia zinapoa na fikra zako zinarudi kwa usahihi. Hata kwenye mambo madogo kama kupishana kauli, usikimbilie kumjibu mtu aliyekuudhi, badala yake tulia na tafakari hilo jambo kwa kina, kwa njia hii utajiepusha na matatizo mengi sana. Fikiria matatizo yote ambayo umewahi kukutana nayo kwenye maisha yako na utaona umekuwa unakimbilia kufanya maamuzi kwa haraka. Jipe muda, na utaepuka matatizo mengi. Hata kwenye kununua vitu, hata kama mtu anakuambia ndiyo kitu cha mwisho, wewe jipe muda na utaona jinsi ambavyo hukuwa unahitaji kitu hicho.
 4. Wakubali watu kama walivyo. Huwa tunajidanganya sana inapokuja kwenye watu, huwa tunataka watu wawe kama tunavyotaka sisi, na wakiwa tofauti tunakazana kuwabadilisha. Hakuna mtu anayependa kubadilika, na mtu akigundua kwamba anataka kubadilishwa basi anakuwa mgumu zaidi kubadilika. Endesha maisha yako kwa kuwakubali watu kama walivyo, kwa kuangalia upande wao mzuri ambao utaweza kuendana na wewe. Usijidanganye kwamba utaweza kumbadilisha mtu, haya ni makosa watu wamekuwa wanafanya wanapoingia kwenye mahusiano au wanapoajiri au kuajiriwa. Chagua mtu ambaye unaweza kwenda naye kama alivyo, na kama mtu inabidi abadilishwe ndiyo uweze kwenda naye, ni vyema ukaachana naye mapema, maana atakuletea matatizo.
 5. Tafuta mlinganyo sahihi kati ya fikra na hisia. Fikra na hisia ni vitu ambavyo vinafanya kazi kwa pamoja, ni kama farasi na mwendeshaji wa farasi. Hisia ndiyo farasi, zina nguvu kubwa lakini zenyewe haziwezi kwenda popote. Fikra ndiyo mwendesha farasi, zina udhibiti mkubwa, lakini bila ushirikiano wa hisia haziwezi kufanya chochote. Hivyo lengo siyo kuondokana na hisia kabisa, bali lengo ni kufanya maamuzi kwa fikra, halafu ukiwa umeshafikia maamuzi yako, unaziachia hisia katika utekelezaji. Kwa sababu hakuna unachoweza kufanya kama huna hisia, iwe ni za tamaa au upendo, au za chuki au maumivu. Watu wanasukumwa kufanya kazi zaidi pale wanapotaka kupata kitu fulani au kueuka maumivu fulani. Hivyo tengeneza mlinganyo sahihi wa hisia na fikra kwako, fikra zitawale wakati wa maamuzi, na hisia zihusike wakati wa utekelezaji.
 6. Penda kufikiri. Kinachofanya wengi wakwame kwenye kufikiri ni kuona ni kazi ngumu na hivyo kuiepuka. Watu watafanya kila kitu lakini siyo kukaa chini na kufikiri. Ndiyo maana wengi wanapojikuta njia panda wasijue nini cha kufanya, huwa wanaangalia wengine wanafanya nini. Na hapo wanafanya maamuzi ya hisia. Kuwa mtu ambaye unapenda kufikiri, na mara kwa mara tenga muda wa kufanya hivyo. Jilazimishe kufikiri baadhi ya vitu kabla hujaangalia wengine wanafanya nini. Akili zetu ni kama misuli, misuli inajengwa kwa mazoezi na akili zetu zinajengwa kwa kufikiri. Kadiri unavyofikiri zaidi ndivyo unavyokomaza akili yako na kuwa mtu wa kufikiri kuliko wa kutumia hisia.

Rafiki, hizi ndizo hatua tatu ambazo Robert Green ametushirikisha, za kutuwezesha kutawala hisia zetu na kufikiri kwa usahihi ili kuepuka kufanya makosa kwenye maamuzi yetu. Tumia njia hizi ili uwe mtu wa kufikiri badala ya kuwa mtu wa hisia.

Kama utapenda kujifunza zaidi kuhusu asili ya binadamu na sheria zinazoendesha asili hii, ili uweze kujielewa wewe mwenyewe na kuwaelewa wengine pia, nakukaribisha kwenye channel ya TANO ZA JUMA. Juma hili la 15 nitakushirikisha uchambuzi wa kina wa kitabu LAWS OF HUMAN NATURE, ambacho kina sheria 18 za asili ya binadamu. Hiki ni kitabu ambacho kila binadamu aliye makini na maisha yake anapaswa kukisoma.

Kama bado hujajiunga na chennel ya tano za juma fanya hivyo sasa ili usikose sheria hizi zitakazokusaidia sana kwenye maisha yako. Tuma ujumbe sasa kwa kutumia app ya TELEGRAM MESSENGER kwenda namba 0717396253, ujumbe uwe na maneno TANO ZA JUMA. Karibu sana tuwe pamoja na kujifunza zaidi kupitia vitabu.

Makala Hii Imeandikwa Na Dr. Makirita Amani Ambaye Ni Daktari Wa Binadamu, Kocha Wa Mafanikio, Mwandishi Na Mjasiriamali. Kupata Huduma Za Ukocha Tembelea; www.amkamtanzania.com/kocha

Kupokea makala moja kwa moja kwenye email yako fungua hapa na ujaze fomu; https://amkamtanzania.com/jiunge

vitabu softcopy