Mpendwa rafiki yangu,

Katika jamii yetu ni wazi kwamba wazazi wengi hawana utamaduni wa kuwafundisha watoto mambo ya fedha. Kwanza wengi wanasema usimruhusu mtoto mdogo kushika fedha, na inapotokea kama mtoto anahoji kuhusu fedha hatumpatii jibu sahihi.

Changamoto ya wazazi wengi ni kukosa msingi wa elimu ya fedha. Kama mzazi hajui unafikiri atawezaje kumfundisha mtoto wake? Ili watoto wetu wawe bora tunapaswa kwanza sisi wazazi tuwe bora. Bila kufanya hivyo tutaendelea kuwa na kizazi ambacho hakina elimu ya msingi wa fedha.

Elimu ya fedha ni muhimu sana kwa watoto, kama wazazi tunatakiwa kuwaelimisha watoto na kuwapa mtazamo chanya juu ya fedha. Ila wazazi wengi wanaiongelea fedha vibaya ndiyo maana hata mtoto anapokuwa anajua fedha siyo kitu kizuri, utasikia wengi wakiwaambia watoto wao kuwa fedha ni shetani. Hii inawajengea imani watoto kuwa kumbe kuwa na fedha nyingi siyo kitu kizuri kabisa.

FEDHA KWA BLOG

Imani hizi hasi za kifedha ndiyo zinamjenga mtoto na kisha kukua katika imani hiyo na baadaye inakuja kumwathiri mtoti huko ukubwani. Wengi wamelishwa imani hasi leo hii hawataki kusikia kuwa utajiri ni kitu kizuri, wengi wanawalisha watoto wao sumu kuwa utajiri ni kitu kibaya.

Wazazi wanawajaza watoto chuki ya kuwachukia matajiri, na kuwajengea imani kwamba masikini ndiyo kitu kizuri. Mwambie mtoto wako ukweli kwamba umasikini ni kitu kibaya ni laana haukusaidii kupata mahitaji yako ya kila siku hapa duniani na utajiri ni kitu kizuri unakusaidia kupata kile unachokitaka.

Leo nenda kavunje imani hii iliyojengeka katika jamii yetu, kwamba wazazi wa kiume pekee yao ndiyo wanastahili kuwa na fedha na hivyo na wazazi wa kike yaani mama hawastahili kuwa na uwezo mkubwa wa kifedha. Ukitaka kuamini hilo, hata wazazi wa kike wanapoombwa mahitaji na watoto wao utasikia wakiwaambia msubirini baba yenu aje mmwambie, mimi sina fedha.

SOMA; Hizi Ndiyo Nguzo Nne Za Malezi Bora

Kila siku mzazi wa kike anasema baba ndiyo mwenye fedha na watoto wanajijengea akili kuwa kumbe fedha anapaswa kuwa nazo baba na siyo mama. Hata wale watoto wengi wa kike hawajitumi  wala kujisumbua wanapokuwa wakubwa wanaona kwamba jukumu la kuwa na fedha au utajiri katika familia ni baba na siyo mama.

Ni dhana potofu sana, ivunje kuanzia leo, kila mtu ana haki ya kuwa tajiri, kuwa na fedha, mafanikio ni haki yako ya kuzaliwa. Mafanikio ni jinsi zote na siyo moja kama watu wengi wanavyodhani. Angalia hata katika jamii zetu, mwenye fedha sana na wanaojituma ni wanaume , hii inawafanya hata watoto kuamini kuwa wazazi wa kiume ndiyo wanawajibika katika mambo ya kifedha.

Hatua ya kuchukua leo; wazazi msijenge mazingira ya kuonsesha kuwa mzazi wa kiume ndiyo mwenye fedha na mzazi wa kike siyo wenye fedha. Jengeni utaratibu imara wa kuwaonesha kuwa wazazi wote ni sawa na kila mtu ana haki ya kuwa tajiri na kumiliki fedha nyingi. Wajengee watoto imani chanya juu ya fedha na siyo hasi.

Kwahiyo, elimu elekezi juu ya fedha ni muhimu sana. Watoto wafundishwe mambo ya fedha wakiwa wadogo ili waelewe maana ya fedha mapema na siyo ukubwani. Tuwaeleze watoto kuwa fedha ni jawabu la mambo yote, tukiwa na fedha mambo mengi yanawezekana.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana