Mpendwa rafiki yangu,

Kazi ya malezi ni kazi sana, siyo kazi rahisi kutengeneza misingi imara kwa watoto. Watoto wanapozaliwa wanakuwa hawana kitu kichwani ubongo wao unakuwa wazi kama vile daftari jipya ambalo halijaandikwa hii ndiyo hupelekea hata mtoto kushindwa kuongea kwa sababu hakuna kitu katika akili yake lakini baada ya muda ataanza kuongea taratibu taratibu mpaka anaimarika.

Kipindi ambacho watoto wanaweza kushika vitu basi ni pale wanapokuwa wadogo. Unaweza kuwafundisha misingi mizuri kwa sababu vichwa vyao ni rahisi sana kupokea kitu kipya kwani akili yao inakuwa haina mambo mengi.

Lakini siku hizi, wazazi wanawaachia watoto wadogo kuangalia TV na kwenye tv wanaona vitu ambavyo hawastahili kuona. Mtoto mdogo akianza kuona vitu ambavyo ni kinyume na umri wake ni jambo la hatari sana linalomwathiri mtoto kiakili. Mambo anayoona huwa hayafutiki katika akili yake hivyo unashangaa mtoto anajua mambo mengi ya kidunia lakini yale ya darasani kwake hakuna kitu.

Rafiki, kitu kibaya katika malezi ya watoto ambacho wazazi wanapaswa kukiepuka ni kuwalinganisha watoto. Hakuna kitu kibaya kama hichi kwa watoto. Kwanza wazazi mnapaswa kuelewa kuwa watoto hawafanani, kwani hata wewe katika familia yako mlikuwa mnafanana? Hata mapacha waliofanana hawafanani kwa kila kitu.

Tumezoea ule utamaduni wa kuwaambia watoto nilivyokuwa mdogo mimi sikuwa kama wewe, nilikuwa nina akili sana, nilikuwa nifaulu sana. sasa jambo kama hili ni baya kwa watoto, usiwalinganishe badala yake unatakiwa kumsifia kwenye ubora wake.

Mfano mwingine ni pale mzazi anaposema yaani wewe tu ndiyo hufanyi vizuri katika masomo yako lakini kaka au dada zako wote wako katika mstari sijui wewe ukoje. Tunapoanza kuwalinganisha watoto wanaanza kujiona wao hawana thamani kabisa.

Hivyo wanakosa hata hamasa ya kujituma kwa sababu wanajiona wao hawana kitu, wengine ndiyo bora. Mzazi unatakiwa kumsifia mtoto kwenye ubora wake na siyo kumlinganisha na wengine, mbona wewe uko tofauti na mwenzako hapana. Tuko tofauti ndiyo maana hatufanani kwa kila kitu, angalia uwezo wake uko wazi na mpongeze kule anakoweza sana na utashangaa anabadilika.

SOMA;Hii Ndiyo Dhana Potofu Ya Kifedha Inayopaswa Kuvunjwa Katika Malezi Ya Watoto

Tunapowalinganisha watoto wanahisi hatuwapendi wala kuwathamin jinsi walivyo. Kila mtoto ana upekee wakehivyo tunatakiwa kuwapongeza na kuwapokea jinsi walivyo.

Hatua ya kuchukua leo; acha ile tabia ya kulinganisha watoto. Kwa mfano, nilivyokuwa mdogo sikuwa kama wewe. Wapongeze watoto kwenye ubora wao na usiwalinganishe tuko tofauti na kila mmoja ana upekee wake.

Kwahiyo, tuwapokee watoto kadiri tulivyopewa na Mungu, tusiwabague bali tuwalee vizuri kwa upendo bila kujali udhaifu waliokuwa nao. Tunapowabagua ndiyo kama tunawaongezea maumivu kwenye ule udhaifu wao.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana