Mpendwa rafiki,

Zama zetu zimekuwa zina changamoto kubwa sana ya malezi ya watoto. Wazazi wanakuwa wako bize kweli na kazi na unakuta watoto wengi wanalelewa na wasaidizi. Wale wasaidizi wanakuwa hawana misingi mizuri ya kuwapa watoto hivyo wanajikuta wanawalea watoto kadiri ya tabia na misingi waliyokuwa nayo.

Mwalimu wa kwanza katika malezi ya watoto ni mzazi, hapa wazazi wamejisahau kweli, wanashindwa kuwadhibiti watoto wao na kuwapelekea malalamiko walimu wa mashuleni kuwa watoto wao wako moja, mbili , tatu. Mzazi mwingine anadiriki kusema mtoto wangu amenishinda anaenda kuwaambiwa walimu wa mtoto huyo wamsaidie. Hivi kama wewe umeshindwa kumlea mtoto wako katika maadili mazuri tokea akiwa mdogo unafikiri ni nani atayeweza kumkunja samaki ambaye tayari ameshakauka?

Wazazi wengi wanategemea sana walimu kuweza kuwasaidia kila kitu watoto wao , kama mzazi ukimtegemea mwalimu ndiyo awajibike kwenye kila kitu katika malezi ya mtoto wako hapo utakua unakosea.

Mtu pekee ambaye anatakiwa kujenga misingi imara ya mtoto wake ni mzazi. Tunasema nyumba ni msingi, sasa kama mtoto amekosa misingi mizuri kwa wazazi usitegemee mtu mwingine ataweza kumbadilisha kama msingi ulikuwa mbovu. Mtoto anapewa misingi ya hovyo nyumbani ambayo haimsaidii mtoto kuweza kupambana na mazingira yoyote, kama akiwa shule au mbali na nyumbani.

Wako wazazi ambao hawataki watoto wao wafanye kazi, kazi za nyumbani kama vile usafi wa mazingira, kupika na nyingine zinazohusiana na hizo. Kazi nyingi wanaachiwa wadada wa kazi, kwa namna hii mtoto kama hajazoea kufanya kazi nyumbani akienda shule za bweni lazima atapata shida, siyo tu shuleni bali pia hata wakija kuingia katika mahusiano ya ndoa wanakuwa hawezi kazi, kazi ambayo ingetakiwa kufanya na mke anashindwa anatafutwa msaidizi wa kazi wa kumsaidia.

SOMA; Hii Ndiyo Dhana Potofu Ya Kifedha Inayopaswa Kuvunjwa Katika Malezi Ya Watoto

Wazazi mnatakiwa kuwalea watoto katika falsafa ya kazi na kujitegemea. Usipomfundisha mtoto wako misingi ya kazi, dunia itakuja kumfundisha kwa kikatili tena bila huruma. Utamlea mtoto wako vile unavyotaka lakini dunia inakuja kumfundisha asili yake.

Hakuna mkataba ambao unaonesha kuwa wewe utaishi na mtoto wako milele, wako wazazi wanaosema kuwa mimi sitaki mtoto wangu apate shida kama mimi nilivyopata. Mfundishe mtoto kuwajibika hata kama una uwezo wa namna gani.

Dunia huwa haiangalii uwezo wa mzazi, kama wazazi mmeshindwa kuwafundisha watoto dunia itakusaidia ila kwa riba kubwa. Ni bora ukawazoesha watoto mapema kupambana na asili ya dunia kabla dunia haijawafundisha.

Kutokujua sheria siyo kibali cha wewe kusamehewa na dunia, wafundishe watoto kweli, usiwafiche, walee kama vile utakufa kesho, wafundishe misingi ambayo itawafanya wasimame hata kama wewe hauko hapa duniani.

Hatua ya kuchukua leo; mzazi pambana kuhakikisha unamfundisha mtoto asili ya dunia, mfundishe misingi ya kazi, uwajibikaji na kujitegemea. Usimlee katika namna ambayo kama wewe utaishi naye milele. Kila eneo la maisha yako mfundishe mtoto, dunia ya sasa haina huruma usipomfundisha mtoto wako watakuja kuteseka sana hapo mbeleni bila kujali walifundisha au la.

Kwahiyo, kila mmoja wetu anajua ukweli wa mambo ulivyo, muda mwingine tunajaribu kutengeneza sababu zetu ili kuukwepa ukweli kama ulivyo. Kumbuka ukweli huwa unajitetea wenyewe, jitahidi sana kuwajibika kwa watoto au mtoto wako, usiitegemee dunia ije kukusaidia kwa adhabu bali anza sasa hujachelewa.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana