Karibu rafiki kwenye makala ya ushauri wa changamoto mbalimbali zinazokuwa kikwazo kwetu kufikia mafanikio makubwa.

Changamoto ni sehemu ya safari yetu ya mafanikio, hivyo hatupaswi kuzikimbia, bali kuzitatua na kusonga mbele.

Kwenye makala hii tunakwenda kupata ushauri wa jinsi ya kuondokana na uraibu au uteja wa kamari na michezo ya bahati nasibu.

Wengi wamekuwa wanaanza michezo hii kama sehemu ya burudani, lakini baadaye inageuka kuwa mzigo kwao. Wanajikuta hawawezi kujizuia na kupoteza muda na fedha nyingi kwenye michezo hiyo.

kubeti.jpg

Kabla hatujaingia kwenye hatua za kuchukua, tupate maoni ya wasomaji wenzetu ambao wameomba ushauri kwenye hili;

Nimejaribu kuacha kucheza kamari kwa miaka 4 sasa nimeshindwa nimekuwa teja nikipata hela yote nachezea mpaka nimepoteza familia yangu (mke na mtoto) mpaka pesa ya kula tulikuwa tunakosa. Nimejaribu kuacha nimeshindwa. Naomba ushauri – Ombeni P. K.

Kubeti jamani huu ni mwaka wa tano nabeti tu. – Ibrahim I. K.

Unagundua umeshakuwa na uraibu au uteja wa kitu pale ambapo unashindwa kuacha kukifanya au kukitumia hata kama kinakupa hasara au kukuumiza. Katika hatua hiyo akili yako inakuwa imeshabadilishwa na kitu hicho, na kuwa tegemezi kwenye kitu hicho.

Kutokana na akili kuwa imeathiriwa, huwa siyo rahisi kuacha kitu kama ambavyo mtu ulikianza, inahitajika nguvu na juhudi za ziada kuweza kuondokana na uraibu wa aina yoyote ile.

SOMA; Kama Umewahi Kucheza Kamari Au Bahati Nasibu Nina Maneno Makali Kwako, Yasome Na Yatakusaidia.

Hapa nakwenda kushirikisha hatua za kuondoka kwenye uraibu au uteja wa kamari na michezo mingine ya kubahatisha. Njia hizi pia zinaweza kutumika kuondokana na uraibu mwingine kama wa vilevi, mitandao, mapenzi n.k.

MATUMAINI.

Tafiti zimekuwa zinaonesha kinachowasukuma watu kushiriki michezo ya kubahatisha au kamari siyo kupata ushindi, bali yale matumaini ya kupata ushindi. Mfano mtu anayenunua tiketi ya bahati nasibu kwa shilingi elfu moja akitegemea kupata milioni moja, anachokitaka hasa siyo ile milioni moja, bali yale matumaini kwamba anaweza kupata milioni moja.

Kwa kujua hili, unaweza kuondokana na uraibu wa kamari na michezo ya kubahatisha kwa kutengeneza matumaini mapya. Jitengenezee matumaini makubwa na yaweke kwenye taswira ambayo unaiona kabisa na kila mara weka taswira hiyo kwenye akili yako.

Kuwa na malengo makubwa, kuwa na maono na ndoto kubwa sana na hakikisha una picha ya maono hayo, unajiona kabisa ukiwa pale unapotaka kufika. Kisha jikumbushe picha hiyo kila siku na mara kwa mara kwenye siku yako.

Matumaini hayo makubwa yataondoa ile kiu ya wewe kushiriki michezo ya kubahatisha au kamari ili kupata matumaini hayo.

FEDHA.

Huwezi kucheza kamari au michezo ya kubahatisha kama huna fedha. Hivyo hatua muhimu kuchukua ni kutengana na fedha zako. Usikubali ukae na fedha ambayo utaweza kuitoa kirahisi kushiriki michezo hiyo.

Fedha zako za akiba ziweke kwenye gereza, kuwa na akaunti maalumu ambayo unaweza kuweka fedha lakini huwezi kutoa. Pia fedha za ziada unazozipata ambazo hukuwa unategemea, ziwekeze mara moja kabla hujakaa nazo muda mrefu.

Epuka sana kukaa na fedha kwenye akaunti yako ambayo ni rahisi kutoa. Na kwa kuwa siku hizi kamari zinachezwa hata kwa simu, epuka kukaa na fedha kwenye mitandao ya simu unayotumia.

Kama uteja umeshakuwa mkubwa kwako, chagua mtu unayemwamini kisha kaa naye chini mfanye makubaliano. Fedha zako zote atakuwa anazishika yeye, na kisha wewe anakupa kile kiasi cha fedha kinachokutosha kwa mahitaji yako tu. Labda kama kwa siku unatumia elfu 10, basi anakupa hiyo tu.

Ukiweza kutengana na fedha kwa muda, na kuepuka kuuza au kukopa ili kushiriki michezo hiyo, utashindwa kushiriki na hapo utavunja uteja.

SOMA; Hatua Tatu Za Kukuwezesha Kutawala Hisia Zako Na Kufikiri Kwa Usahihi Ili Kuepuka Kufanya Maamuzi Mabovu.

MUDA.

Unashiriki michezo ya kubahatisha na kamari kwa sababu una muda mwingi ambao huna kitu cha kufanya. Katika hali hii, muda mwingi ni adui yako.

Hivyo epuka sana kuwa na muda mtupu kwenye siku yako. Badala yake pangilia siku yako nzima na ijaze na majukumu mbalimbali kiasi kwamba huna kabisa muda ambao ni mtupu.

Kama kazi unayofanya inakupa muda mwingi, chagua kitu kingine cha kufanya kwenye muda wa ziada unaopata. Anzisha biashara ya pembeni, fufua kipaji chako, soma vitabu, jifunze vitu vipya na mengine yatakayokuweka ‘bize’.

Jiambie wazi kabisa muda mtupu ni adui kwako, hivyo uepuke sana.

MAZINGIRA.

Mazingira yana mchango mkubwa sana kwa uraibu na uteja kuendelea. Hivyo ili kuvunja tabia hiyo, lazima ubadili mazingira yako.

Ondoka kabisa kwenye mazingira ambayo yanachochea wewe kucheza kamari au michezo ya kubahatisha.

Angalia ni katika mazingira yapi unasukumwa kushiriki michezo hiyo, kisha ondoka kabisa kwenye mazingira hayo.

Kama ni michezo unayofuatilia, acha kuifuatilia. Kama ni marafiki umekuwa nao acha kuwa nao. Kama ni matangazo unayaona yanayokuhamasisha, yaepuke.

Kaa mbali na mazingira yoyote yanayokuhamasisha kushiriki kwenye michezo ambayo inakupa uteja na uraibu.

MSONGO.

Mara nyingi unakimbilia kufanya kitu ambacho una uraibu nacho pale unapokuwa na msongo wa mawazo. Kufanya kitu hicho inakufanya ujisikie vizuri na hivyo kuondokana na msongo.

Unapaswa kutumia njia nyingine za kuondokana na msongo, ambazo hazikuingizi kwenye uraibu.

Njia kama kufanya tahajudi ina manufaa mazuri katika kuondokana na msongo. Pia kufufua vipaji vyako na kuvifanyia kazi inakuwa njia nzuri ya kuondokana na msongo.

SOMA; Hivi Ndivyo ‘Nguvu Ya Buku’ Inavyoweza Kukufikisha Kwenye Ubobezi Wa Hali Ya Juu Na Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako.

KIKUNDI.

Kama hali yako ya uraibu imekuwa kubwa na peke yako umeshindwa kuondokana nayo, basi jiunge na kikundi cha kusaidiana ambacho kitakuwezesha kuondoka kwenye uraibu huo.

Uzuri wa vikundi hivi ni kwamba mnakuwa watu ambao wote mnataka kuondoka kwenye uraibu na hivyo kusaidiana katika hatua za kuondoka kwenye uraibu huo. Mnakutana mara kwa mara kujadiliana na kufuatiliana katika hatua za kuondokana na msongo huo.

Katika vikundi vya aina hii mnakuwa na washauri au wanasaikolojia ambao wanawasaidia kwa karibu kuondokana na uraibu ambao mtu anakuwa ameingia.

Kama umefika hatua ya kuona kile unachofanya hakina tena manufaa kwako lakini ukijaribu kukiacha unashindwa, jua umeshakuwa mteja wa kitu hicho. Chukua hatua hizi tulizojifunza hapa na kua na msimamo katika kuzifanyia kazi bila kujiruhusu kutetereka na utaweza kushinda uteja huo na kujenga maisha yako upya.

Mara zote pambana kulinda akili yako isiharibiwe kwa kuwa tegemezi kwenye kitu chochote kile. Tumia muda wako kujifunza vitu vipya na kusoma vitabu. Jifunze kufikiri kwa kina kabla ya kufa ya maamuzi yoyote yake. Na epuka kabisa njia zozote za mkato za kupata unachotaka au kuondoka kwenye msongo, chochote kinachokupa raha ya muda mfupi basi jua kitakupa maumivu ya muda mrefu.

Hivyo kwenye maisha yako, jifunze kuchelewesha raha, badala ya kukimbia maumivu ya muda mfupi na kupata raha ya muda mfupi, kubali maumivu ya muda mfupi ambayo yatakupa raha ya muda mrefu.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania