Karibu rafiki kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto mbalimbali ambazo ni kikwazo kwa mafanikio yetu. Changamoto huwa haziishi, kila unapovuka changamoto moja unakutana na nyingine. Hivyo kuwa bora na kuweza kukabiliana na changamoto yoyote ni hitaji muhimu kwa mafanikio yako.
Leo tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kuongeza wateja kwenye biashara yao na ukaweza kuikuza zaidi. Biashara nyingi hazikui kwa sababu hazitengenezi wateja wapya hivyo zinabaki pale pale. Lakini pia wafanyabiashara wengi hawana mpango wa ukuaji, hivyo biashara zao zinashindwa kupiga hatua.
Kabla hatujajifunza hatua za kuchukua ili kuongeza wateja na kukuza biashara yako, tupate maoni ya msomaji mwenzetu aliyetuandikia kuhusu hili;
Habari kaka pole na kazi mimi fundi wa milango na madirisha ya aluminum nina miaka 3 lakini changamoto moto yangu biashara haikui niko palepale. Nataka kufungua ofisi nyingine lakini mtaji unakua shida na wateja hawaji kwangu sijui nifanye nini nifanikiwe. Naomba msaada wako kaka Aman. – Hamad A. S.
Changamoto aliyonayo Hamad ni changamoto inayowakumba wafanyabiashara wengi wa chini na kati. Wengi wanakuwa kwenye biashara kwa miaka mingi, lakini biashara zao hazikui. Wanakuwa kama wamenasa kwenye mtego ambao hawawezi kujinasua.
Mtu unakuwa umeanzisha biashara kwa lengo la kupata uhuru wa muda na kipato, lakini biashara hiyo inaishia kuwa gereza kwako, inakuhitaji muda wote huku kipato unachoingiza kupitia biashara hiyo kikiwa hakitoshelezi.
Hapa tunakwenda kujifunza hatua tano za kuchukua ili kupata wateja zaidi na kuikuza biashara yako.
Moja; kuwa na mpango wa ukuaji.
Ukuaji kwenye biashara hautokei kama bahati, bali ni matokeo ya mipango iliyowekwa na kufanyiwa kazi. Hapa ndipo wafanyabiashara wengi wanapokwama, kwa sababu wanafikiri wakishaanzisha biashara basi yenyewe itakua.
Lazima uwe na mpango wa ukuaji, kwamba umeanza na mtaji kiasi fulani basi baada ya muda fulani mtaji huo umefika wapi. Kwamba umeanza na eneo moja baada ya muda fulani unakuwa na matawi kwenye maeneo mengine.
Hapa unapaswa kukaa chini na kuandika kabisa mpango wako, kwa kujipa muda ambapo utakuwa umefikia ulichopanga. Haijalishi umepanga nini, na wala haijalishi kama utafikia au la, kitendo tu cha kuwa na mpango ambao kila siku unajikumbusha, kinakupa msukumo tosha wa kuiwezesha biashara yako kukua zaidi.
Hatua ya kuchukua; kaa chini leo na utengeneze mpango wa ukuaji wa biashara yako, pata taswira ya miaka 2, 5 mpaka 10 ijayo utakuwa umefika wapi kisha weka hatua unazopaswa kuchukua ili kufika huko. Jikumbushe mipango yako ya ukuaji kila siku na jitathmini kama upo kwenye njia sahihi au la.
SOMA; Hatua Kumi Za Kumnasa Mteja Kwenye Biashara Yako Na Kuwa Naye Kwa Muda Mrefu.
Mbili; fanya kazi iliyo bora sana.
Wateja watanunua kwako au kufanya kazi na wewe, siyo kwa sababu unauza, au kwa sababu wanakuonea huruma, bali kwa sababu wananufaika zaidi kununua kwako kuliko wakinunua kwa wengine. Hili ni jambo muhimu sana unalopaswa kulielewa kuhusu saikolojia ya binadamu, sisi binadamu ni wabinafsi.
Hivyo angalia ni jinsi gani unaweza kutimiza ubinafsi wa wateja wako, kwa kuhakikisha wanapata kile ambacho hawawezi kukipata sehemu nyingine yoyote.
Fanya kazi iliyo bora sana, jitofautishe kabisa na wengine wanaofanya biashara kama yako, hakikisha kuna kitu ambacho mteja anakipata kwako na hawezi kukipata sehemu nyingine yoyote. Na kama unaijua biashara yako vizuri, basi kuna vingi unavyoweza kuvifanya na wateja wako wakanufaika sana.
Hatua ya kuchukua; jiulize ni kitu gani wateja wanaweza kupata kwako lakini hawawezi kupata kwa wengine, kama huna kitu cha aina hii, haupo makini na biashara yako. Tafuta kitu cha aina hiyo, anza kukitoa kwa wateja wako na utawavutia wengi.
Tatu; wafuate wateja kule walipo.
Zile fikra kwamba nitafungua biashara eneo ambalo kuna wateja wengi wanapita na wakiiona biashara watakuja wenyewe zimeshapitwa na wakati. Watu wako ‘bize’ mno zama hizi, kila mtu ametingwa vya kutosha kiasi kwamba anaweza kupita mbele ya biashara yako kila siku na asijue unauza nini.
Lazima uwe na mpango wa kuwafuata wateja wako kule waliko, na kuhakikisha wanajua kuhusu biashara yako, kuhusu huduma unazozitoa na jinsi zinavyoweza kuwanufaisha. Hapa pia ndipo unawajulisha kuhusu kile wanachoweza kupata kwako lakini hawawezi kupata kwingine kokote.
Biashara yoyote isiyokuwa na mpango wa kuwafikia wateja kule walipo (masoko) haiwezi kukua kwenye zama hizi. Kwa sababu hizi ni zama za kelele, zama ambazo ushindani ni mkali na wateja hawana muda. Hivyo kuwa na njia ya kuwafikia ni muhimu sana.
Tengeneza mpango wako wa masoko, nenda nyumba kwa nyumba, ofisi kwa ofisi na maeneo mengine yenye wateja wako, kuwa na maelezo mafupi kuhusu biashara yako na yenye ushawishi, kisha ongea na wateja wengi zaidi.
Pia tumia njia mbalimbali za kutangaza biashara yako, mitandao ya kijamii, ni moja ya njia rahisi unazoweza kutumia, ila tumia kwa namna bora ambapo utawafikia watu sahihi na kuweza kuwashawishi kufanya nao kazi.
Hatua ya kuchukua; tengeneza mpango wako wa masoko, kwa kujua wateja unaowalenga, wanapatikana wapi na kisha kuwafuata kule wanakopatikana.
Nne; jitofautishe na biashara yako kifedha.
Changamoto kubwa inayozikabili biashara nyingi ndogo ni wamiliki wa biashara hizo kutokujua mpaka kati yao na biashara zao. Kwa sababu biashara ni yake, basi anafikiri na fedha za biashara ni zake. Hivyo mtu anaweza kuondoa fedha kwenye biashara na kuitumia kwa matumizi yake binafsi.
Kwa utaratibu huu, biashara haiwezi kukua hata ufanyeje. Ni sawa na mtoto kuzaliwa halafu mama yake hamnyonyeshi maziwa, ataishia kupata utapiamlo.
Unapaswa kujitofautisha wewe na biashara yako kifedha, usiondoe fedha kwenye biashara kwa matumizi yako binafsi. Ukishaweka mtaji kwenye biashara usiutoe, hata kama kuna nini kimetokea.
Kitu pekee unachoweza kutoa kwenye biashara yako ni sehemu ya faida unayopata. Hivyo hata kama una shida gani, ichukulie biashara kama mali ya mtu mwingine na angalia njia nyingine za kukabiliana na changamoto zako.
Pia kuwa na akaunti maalumu kwa ajili ya biashara yako, ambapo ndipo fedha zote za biashara zinaingia. Iache fedha izunguke kwenye biashara na wewe tumia faida pekee.
Kama maisha yako yanategemea biashara yako na faida haitoshelezi, kazana kukuza faida na siyo kula mtaji. Uliona wapi mkulima anakula mbegu kwa sababu ana njaa, hapo ni kutengeneza njaa zaidi baadaye.
Hatua za kuchukua; jua kiwango cha mtaji ulichoweka kwenye biashara yako na usikiguse, kokotoa faida unayopata na hapo unaweza kuchukua sehemu ya faida hiyo kwa matumizi yako. kama faida haitoshelezi, weka kazi, usiguse mtaji. Na faida usitumie yote, sehemu ya faida inapaswa kurudi kwenye biashara kukuza mtaji.
Tano; kuwa na mtazamo wa muda mrefu.
Biashara nyingi ndogo huwa hazikui kwa sababu mtazamo wa wamiliki wa biashara hizi ni mdogo. Wengi wanaangalia matokeo ya muda mfupi na siyo muda mrefu. Mtu anaangalia anapata nini leo na siyo biashara itakuwa wapi miaka 10 ijayo.
Kwenye hatua ya kwanza tumejifunza umuhimu wa kuwa na mpango wa ukuaji, hapa tunajifunza unapaswa kuwa na mtazamo wa muda mrefu. Kila unachofanya kwenye biashara, jiulize miaka 10 ijayo biashara hiyo itakuwa wapi.
Kwa kuangalia hivi, utaacha kuhangaika na vitu vyenye faida ya muda mfupi lakini madhara ya muda mrefu. Utaweza kupanga na kuchukua hatua sahihi, kwa sababu unayo picha kubwa ya miaka mingi ijayo.
Biashara yoyote unayoifanya, angalia miaka 10, 20 mpaka 50 ijayo, ione ikiwa biashara kubwa sana hivyo kila hatua unayochukua sasa, unaipima kwa picha hiyo kubwa ya baadaye.
Hatua ya kuchukua; kwa kila unachofanya kwenye biashara yako, jiulize kinaipeleka wapi biashara yako miaka 10 ijayo, kama kinaipeleka kubaya, usikifanye.
Fanyia kazi hatua hizi tano na utaweza kuikuza biashara yako, kwa kuwa na wateja wengi zaidi na kudhibiti mzunguko wa fedha huku ukifanyia kazi mpango wa ukuaji.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania