Wafanyabiashara wengi wadogo wanaingia kwenye biashara wakiwa hawajui lolote kuhusu biashara.

Hawajawahi kufundishwa misingi ya biashara na wala hawajawahi kusoma kitabu chochote kuhusu biashara.

Wao wanachojua ni hili; biashara ni kununua na kuuza, nunua kwa bei ya chini, uza kwa bei ya juu na utapata faida.

Na wanakwenda kufanya hivyo, wananunua mali kwa bei ya chini na kuuza kwa bei ya juu, ambayo ni sawa na wengine wanavyouza.

Wanakuja kustuka kwamba hawapati faida, na kinachowaonesha hilo ni mtaji kupungua na baadaye biashara kufa kabisa.

Rafiki yangu mpendwa, biashara zingekuwa rahisi hivyo, kwamba ni kununua tu na kuuza, tusingekuwa tunaona biashara zikiwa zinakufa kila wakati. Kila biashara inayoanzishwa ingefanikiwa.

Lakini biashara zina mambo mengi, ambayo wengi hawayajui na hawayazingatii na ndiyo maana changamoto zimekuwa hazikomi.

kuza faida.jpg

Leo kwenye makala yetu ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufanikiwa, tutajifunza jinsi kupata faida na kuepuka hasara kwenye biashara yako.

Kabla hatujaingia kwenye yale ya kufanya, tupate maoni ya wasomaji wenzetu walioomba ushauri kwenye hili.

Changamoto inayonizuia kufikia malengo niliyokusudia ni hasara kwenye biashara, kila nikifanya biashara najikuta mtaji pamoja faida vyote napoteza nifanyeje? – Evance L.

Dr changamoto ya nina duka la vifaa vya umeme ninashindwa kujua  na kufahamu ni faida gani duka langu linaingiza faida kwa mwaka pia nakatika kutunza takwimu. Joseph M.

Mimi ni mjasiriamali mdogo na nikipata faida katika biashara yangu huwa natoa matumizi yote ya muhimu na inayobaki, nairudisha kwenye mtaji wangu ninahitaji kufahamu kama nafanya jambo jema au la ila nikipatwa na dharura nachukua hela katika mtaji wangu. Emmanuel M.

Kama tulivyosoma maoni ya wasomaji wenzetu hapo juu, faida ni changamoto kwenye biashara nyingi. Kuanzia kushindwa kujua faida, kupata hasara na hata kushindwa kujua matumizi sahihi ya faida inayopatikana kwenye biashara.

Kwenye makala ya leo tunakwenda kujifunza mambo matano ya kuzingatia ili kuweza kupata faida na kuepuka hasara kwenye biashara yako.

Karibu ujifunze, uchukue hatua na biashara yako iweze kupata faida na kuepuka hasara.

Moja; Zijue Namba Muhimu Za Biashara Yako.

Biashara ni mchezo wa namba, kama upo kwenye biashara na huzijui namba muhimu za biashara yako unajidanganya. Kuwa kwenye biashara na kutokujua namba za biashara yako ni sawa na kuendesha gari huku umefumba macho, tegemea ajali muda wowote.

Kuna namba nyingi za kujua na kufuatilia kwenye biashara yako, lakini kwa kila biashara, namba hizi sita ni za msingi kabisa, hivyo kila mfanyabiashara anapaswa kuzijua na kuzifuatilia kwenye biashara yake.

 1. Mtaji unaozunguka. Hii ni ile fedha ambayo ipo kwenye biashara kama mtaji. Hii ni namba muhimu kuijua na kuifuatilia ili kujua kama biashara inakua au inakufa. Utajua hilo kwenye kupanda au kushuka kwa mtaji.
 2. Manunuzi/uzalishaji. Hii ni fedha inayotumika kununua au kuzalisha bidhaa au huduma ambayo biashara inauza. Hii ni muhimu sana uijue kwa sababu ndiyo inachukua mtaji.
 3. Mauzo. Hii ni fedha inayoingia kwenye biashara kutokana na mauzo ya bidhaa au huduma ya biashara. Hii ni namba muhimu kwa sababu ndiyo chanzo kikuu cha mapato kwenye biashara yako, bila mauzo hakuna biashara.
 4. Gharama za uendeshaji. Hizi ni zile gharama ambazo biashara inaingia katika kuiendesha. Gharama kama za pango, umeme, maji, kodi, wafanyakazi na nyinginezo ambazo unalipa kwenye biashara yako zinaingia hapo. Ni muhimu sana kuzijua hizi maana ndiyo zinazokula faida ya biashara yako.
 5. Faida halisi ya biashara. Hii ni ile fedha inayopatikana baada ya kuchukua mauzo na kutoa manunuzi/uzalishaji, kisha kutoa gharama za kuendesha biashara. Hii ni namba muhimu sana, kwa sababu ndiyo inapima uhai wa biashara.
 6. Wateja. Hawa ndiyo wanaonunua kwenye biashara. Hii ni namba muhimu kufuatilia maana itakuonesha kama biashara inakua au kufa kulingana na ongezeko au kupungua kwa wateja.

Hakikisha namba hizi 6 unazijua na kuzifuatilia kwa ukaribu kwenye biashara yako kama kweli unataka kufanikiwa kwenye biashara hiyo.

SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuongeza Wateja Na Kukuza Biashara Yako.

Mbili; Tunza Vizuri Kumbukumbu Za Biashara Yako.

Umeshazijua namba muhimu, sasa hakuna muujiza kwenye kuzijua, zaidi ya wewe kutunza kumbukumbu. Na hapa nikutahadharishe tu, acha uvivu. Andika kila kinachofanyika kwenye biashara yako. Utaandika kwa namna gani hilo chagua mwenyewe, kama ni kwenye daftari, kama ni kwa programu maalumu za uendeshaji wa biashara, hapo chagua mwenyewe.

Lakini hakikisha unatunza vizuri kumbukumbu za kila kinachofanyika kwenye biashara. Umenunua andika, kiasi gani umenunua. Umeuza andika, umelipa kitu andika, umetoa fedha kwenye biashara andika. Wateja uliowahudumia andika idadi yao. Kila kinachofanywa kwenye biashara, na wewe au mwingine yeyote, kinapaswa kuandikwa kwa namna ambayo ni rahisi kurejea baadaye na kukokotoa vitu muhimu.

Tatu; Kokotoa Faida Halisi Ya Biashara.

Umetunza vizuri kumbukumbu za biashara yako, sasa sehemu muhimu kabisa ya kujua biashara yako inaendaje ni faida halisi ya biashara hiyo.

Kwanza kabisa chagua ni kipindi gani unatumia kupima, nashauri uwe unafanya kila siku kama ikiwezekana, kama haiwezekani basi hakikisha unafanya kila wiki na kila mwezi.

Kukokotoa faida halisi ya biashara chukua hatua zifuatazo;

 1. Chukua mauzo na toa manunuzi, hapa utapata faida ghafi.
 2. Chukua faida ghafi na ondoa gharama zote za kuendesha biashara katika kipindi unachopima.
 3. Kinachobaki hapo ndiyo faida halisi ya biashara yako.

Vitu muhimu vya kujua kwenye kukokotoa faida halisi.

Iwapo hakuna faida ghafi, yaani mauzo ni madogo kuliko manunuzi, basi hapo hakuna biashara, unaelekea shimoni, hivyo unapaswa kufanya mabadiliko makubwa kwenye biashara yako.

Iwapo kuna faida ghafi, lakini hakuna faida halisi, maana yake gharama za kuendesha biashara ni kubwa, hivyo unaweza kuzipunguza gharama hizo au kuongeza zaidi faida ghafi ili uweze kubaki na faida halisi.

SOMA; Tano Za Juma Kutoka Kitabu; Profit First (Jinsi Ya Kuweza Kutengeneza Faida Kwenye Biashara Yoyote Ile).

Nne; Pangilia Vizuri Matumizi Ya Faida Hiyo.

Kupata faida ni jambo moja, matumizi ya faida hiyo ni jambo jingine ambalo huwa linawatatiza wengi.

Wapo ambao huwa wanatumia faida yote kwa sababu ndiyo kilicho chao kwenye biashara hiyo.

Na wapo ambao wanarudisha faida yote kwenye biashara.

Unapaswa kupangilia vizuri faida yako kwa ajili ya ukuaji wa biashara yako.

Kwanza kabisa tenda fungu unalojilipa wewe. Hakikisha malipo yako yanatokana na faida inayopatikana kwenye biashara, hivyo jiwekee kiwango utakachojilipa kwenye biashara yako.

Pili kuwa na akiba maalumu ya dharura au mtaji mbadala ambayo unaweza kuitumia pale biashara inapokutana na changamoto au unapokutana na fursa nzuri katika wakati ambao huna fedha za ziada.

Tatu sehemu ya faida inapaswa kurudi kwenye mtaji, ili kuiwezesha biashara yako kukua zaidi. Biashara haiwezi kukua kama mtaji unabaki vile vile, unapaswa kuukuza kwa kurudisha sehemu ya faida kwenye mtaji.

Tano; Kila Siku Kazana Kuongeza Faida.

Umeshajua kwamba mtaji ndiyo namba muhimu kwenye biashara yako, hivyo kila siku chukua hatua ambazo zitaongeza faida zaidi kwenye biashara yako.

Hapa ni baadhi ya hatua unazoweza kuchukua kila siku.

 1. Kuongeza wateja wa biashara yako kwa kufanya masoko zaidi.
 2. Kuongeza mauzo ya biashara yako kupitia wateja wapya na kuuza zaidi kwa wateja ulionao sasa.
 3. Kutafuta sehemu ambayo unaweza kununua kwa bei ndogo zaidi au kuwa na njia za kuzalisha kwa gharama ndogo.
 4. Kupunguza gharama za kuendesha biashara.

Kila siku ya biashara yako angalia fursa za kuongeza zaidi faida kwenye biashara hiyo, kwa sababu ndiyo njia pekee kwa biashara hiyo kukua.

Rafiki, umejifunza jinsi ya kupata faida na kuepuka hasara kwenye biashara, sasa kazi ni kwako kuyaweka kwenye matendo haya uliyojifunza ili biashara yako iweze kufanikiwa. Kama unajiambia kuna mambo hapa ni magumu kwako kufanya, basi jua umeshachagua kutokufanikiwa kwenye biashara. Haupo kwenye biashara kufanya mambo rahisi, bali mambo sahihi. Umeshayajua yaliyo sahihi, nenda kayafanye.

Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani

TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE

Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.

Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania