Karibu rafiki kwenye makala yetu ya leo ya ushauri wa changamoto zinazotuzuia kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Kwa hali tunayopitia sasa kama dunia, ya mlipuko wa virusi vya Corona, kila mtu anapitia changamoto mbalimbali.
Na wanaokutana na changamoto nyingi zaidi ni wafanyabiashara wadogo na wa kati ambao biashara zao zilikuwa zinategemea watu kufika eneo la biashara ili kupata bidhaa na huduma zinazotolewa.
Kutokana na watu kuzuiwa au kushauriwa kutokutoka pasipo na ulazima, wateja wamepungua sana na hilo kupunguza mauzo na kuathiri biashara.
Suluhisho pekee la hali hii ni kuihamishia biashara kwenye mtandao wa intaneti, ili uweze kuwauzia watu bila ya kufika kwenye eneo lako la biashara.
Kwenye makala ya leo ya ushauri wa changamoto, tunakwenda kujifunza jinsi unavyoweza kuihamishia biashara yako mtandaoni, ukawafikia wengi na kuuza zaidi katika kipindi hiki cha changamoto na hata mabadiliko yatakayoendelea baada ya hapa.
Kabla hatujaangalia nini cha kufanya, tupate maoni ya msomaji mwenzetu anayepitia changamoto kwenye hili;
Kutokana na Corona, asilimia 95 ya wanafunzi wamesimamisha kusoma Kiswahili na karibu 100% ya booking ya wanafunzi wamesitisha na wengi waliokuwa nchini wamerudi kwao. Ingawa nimechelewa sana kuwekeza kozi online swahili kwa kutumia Zoom na Wasap.
Kama korona itaendelea, Mwisho wa mwezi tutafunga kabisa vituo baadhi ya vituo na tutabaki na ofisi tu. Mikataba yote tuliyokubaliana itasitishwa au kubadilisha na kuvunjwa
Baada ya 95% kusitisha masomo na booking, napata changamoto ya kuingia kwenye ufundishaji wa online mubashara na kuweka masomo ya Kiswahili online kwenye Youtube. Sijui nifanye sasa au nisubiri baada ya korona kwisha, hasusani kwenye yputube sijui italeta mafanikio au la. – F. K.
Rafiki, hivyo ndivyo msomaji mwenzetu anavyopitia changamoto kwenye biashara yake ya kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni, ambayo imeathirika sana kutokana na janga hili la Corona.
Tutakwenda kumshauri namna bora ya kuhamishia biashara yake mtandaoni na jinsi ambavyo wewe pia unaweza kuhamishia biashara yao mtandaoni na ukanufaika.
Ukweli kuhusu hali tunayopitia sasa.
Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tupeane ukweli wa hali tunayopitia sasa.
Najua wengi tunasubiria tukijua kwamba hali hii itapita baada ya muda mfupi na mambo yatarudi kama zamani. Ni kweli hali hii itapita, ila siyo ndani ya muda mfupi na hata baada ya kupita mambo hayatarudi kama zamani. Hivyo kujiambia kwamba unasubiri hali hii ipite na mambo yarudi kama zamani unajidanganya na kujipoteza. Unachopaswa ni kuchukua hatua mbadala ambazo zinaendana na hali tunayopitia sasa, ambazo ndiyo zitakuwa endelevu kutokana na mabadiliko ambayo yataendelea.
Mlipuko wa virusi vya Corona umekuja kama kitu cha kutuamsha na kutuonesha kama tunachofanya ni muhimu na kama tunakifanya kwa usahihi. Kama biashara imeathirika sana katika kipindi hiki cha Corona basi huenda siyo biashara sahihi au haifanyiki kwa usahihi. Hivyo kama tunataka kubaki kwenye biashara baada ya hili kupita, lazima tuzibadili biashara zetu kuwa sahihi au kuzifanya kwa usahihi na siyo kusubiri.
Na moja ya njia sahihi za kuifanya biashara yako ni kwa kutumia mtandao wa intaneti ambapo mteja anaweza kuagiza bidhaa au huduma zako akiwa nyumbani kwake na akawa na njia rahisi ya kuzipata.
SOMA; Mwongozo Wa Kufanyia Kazi Nyumbani Wakati Huu Wa Mlipuko Wa Corona.
Faida za kutumia mtandao wa intaneti.
Kutumia mtandao wa intaneti kwenye biashara kuna faida nyingi, hapa nakushirikisha chache ambazo zina manufaa sana kwa kipindi tunachopitia sasa.
- Inapunguza sana gharama za kuendesha biashara. Kwa kutumia mtandao wa intaneti unaounguza idadi wa watu unaowahitaji kusaidia kwenye biashara, unapunguza uhitaji wa eneo la kufanyia biashara na gharama nyingine ambazo biashara inaingia katika kutoa huduma zake.
- Ni rahisi kuwafikia wateja kwa kutumia mtandao, kwa sababu wengi wanatumia muda wao kwenye mtandao.
- Inaondoa ukomo wa eneo, kama unafanya biashara ya huduma, unaweza kuuza kwa mtu yeyote popote pale alipo duniani na siyo wale tu ambao wanaweza kufika kwenye biashara yako.
- Inapunguza kazi unazofanya, kwa biashara ya huduma, ukishaandaa mara moja, utauza zaidi na zaidi bila ya kuandaa tena huduma yako upya.
- Ni rahisi kutunza taarifa za wateja wako na kuweza kuwasiliana nao na kuwauzia bidhaa na huduma zaidi zitakazowafaa.
Jinsi ya kuhamishia biashara yako mtandaoni.
Karibu sasa ujifunze hatua za kuchukua ili kuweza kuhamishia biashara yako mtandaoni. Hapa tutashauri kwenye biashara ya kufundisha lugha ya Kiswahili kwa wageni, lakini unaweza kutumia kwa biashara ya aina yoyote ile.
Fuata hatua hizi katika kuhamishia biashara yako mtandaoni.
Moja; kuwa na mpango kamili wa biashara yako mtandaoni.
Kabla hujaingia kufanya biashara kwa njia ya mtandao, lazima kwanza uwe na mpango kamili.
Na mpango huo unapaswa kuhusisha maeneo matatu;
Eneo la kwanza ni jinsi bidhaa au huduma unayotoa itawafikia wateja wako. Hapa kwa biashara ya kufundisha Kiswahili kwa mtandao, unahitaji kuwa na tovuti ambayo wateja wataweza kuingia na kujiandikisha kisha kupata madarasa ya lugha hiyo.
Eneo la pili ni kuwapata wateja, wajue kuhusu uweo wa biashara yako na washawishike kupata huduma au bidhaa unayotoa. Hapa ni masoko na kwa biashara ya kufundisha lugha, unapaswa kutumia mitandao ya kijamii kama Youtube kuwapata wateja wenye uhitaji wa kujifunza lugha, unawafikisha kwenye tovuti yako na hapo wanapata huduma zinazotolewa.
Eneo la tatu ni la malipo, hapa lazima ujue utachaji kiasi gani kwa bidhaa au huduma unayotoa na utatumia njia zipi kukusanya malipo, ambazo ni salama kwako na kwa mteja. Hili ni eneo muhimu kwa sababu hukutani na wateja hivyo lazima kuwa na njia ya kulipia ambayo ni salama kwa wote. Na pale biashara inapohusisha wateja wa mataifa ya nje, unapaswa kuchagua vizuri njia ya malipo ambayo itakuwezesha kupata fedha zako.
Weka mpango wako kwa kuzingatia maeneo hayo matatu na huo ndiyo utakaoufanyia kazi.
SOMA; Hii Ndiyo Biashara Unayoweza Kufanya Ukiwa Nyumbani Na Kuingiza Kipato Bila Kukutana Na Wateja.
Mbili; chagua njia ya kutoa bidhaa/huduma yako.
Kwa huduma ya kufundisha lugha ya kigeni, kuna njia mbili za kutoa huduma hii.
Njia ya kwanza ni kwa mafunzo ambayo ni mubashara, yaani moja kwa moja, mwanafunzi na mwalimu wote wanakuwa mtandaoni kwa wakati mmoja. Hapa unahitaji kutumia aina ya mitandao inayoruhusu hilo, mfano Zoom, Whattsapp na mingine. Njia hii inahitaji muda mwingi kuendesha madarasa na walimu wengi pia, hasa kama unafanya darasa kwa mwanafunzi mmoja mmoja au vikundi vidogo vidogo.
Njia ya pili ni kuandaa mafunzo na kuyaweka kwa mtiririko wa kujifunza kwenye tovuti inayofungua mafunzo hayo kwa mtiririko, kisha mwanafunzi anajifunza mwenyewe kwa muda wake. Hapa atafungua somo la kwanza, atajifunza, kisha akimaliza anaenda somo la pili na kuendelea. Kunaweza kuwa na njia ya wao kuuliza maswali au kujibu maswali ya kujipima uelewa wao kwenye somo husika. Njia hii ya pili ni rahisi na haihitaji muda mwingi, ukishaandaa masomo na kuyaweka mtandaoni, wanafunzi wanaweza kujiunga muda wowote na kujifunza, hata kama haupo mtandaoni kwa muda huo.
Hapa nashauri utumie njia zote mbili, uandae mtiririko wa masomo ambapo mwanafunzi anaweza kufuata mwenyewe na gharama ya kujifunza kwa njia hii isiwe kubwa sana. Hivyo utaweza kukaribisha wanafunzi wengi. Na pia uwe na madarasa mubashara ambayo yanakuwa na ratiba maalumu na muda maalumu na haya gharama yake inaweza kuwa kubwa kidogo ukilinganisha na madarasa yasiyo mubashara.
Tatu; fanya masoko ya uhakika.
Uzuri wa kupeleka biashara yako mtandaoni ni kwamba unavunja kabisa mipaka, mtu yeyote na popote alipo duniani anaweza kunufaika na biashara yako. Lakini watu ni lazima kwanza wajue biashara yako ipo na inawezaje kuwasaidia, hapa ndipo ilipo nafasi ya masoko.
Kwa biashara ya kufundisha lugha, unapaswa kuwa na channel kwenye mtandao wa youtube na mitandao mingine ya kijamii.
Kisha unapaswa kurekodi video fupi za baadhi ya masomo na kuweka kwenye mitandao hiyo, ambazo zinatoa somo kidogo na baadaye kumkaribisha mtu kujiunga na kozi kama anapenda kujifunza zaidi. Kwa njia hii, mtu yeyote popote alipo atajua kuhusu biashara na jinsi itakavyomsaidia.
Kwenye mitandao ya kijamii pia unaweka jumbe fupi fupi na mafunzo mafupi zaidi ya kuwafanya watu kujifunza na kutamani kujifunza zaidi.
Hapa kwenye masoko pia andaa bajeti ya kutangaza baadhi ya masomo yako mtandaoni, hasa yale ya mubashara. Hapa unalipa gharama kidogo na kufanya matangazo yako yawafikie wengi zaidi. Wewe tu unachagua unalenga watu wa aina gani na waliopo sehemu gani.
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuongeza Wateja Na Kukuza Biashara Yako.
Nne; weka mpango wa malipo vizuri.
Eneo muhimu sana kuzingatia ni kwenye malipo. Kwa wateja waliopo ndani ya nchi hii siyo changamoto, zipo njia mbalimbali za kulipwa kwa urahisi, mfano mitandao ya simu.
Wateja waliopo nje ya nchi kuna changamoto kidogo, kwa sababu mifumo yetu ya kifedha hairuhusu mtu kulipwa moja kwa moja kutoka nje ya nchi.
Hivyo hapa unahitaji kutumia huduma ya katikati (payment gateway), ambapo wateja watalipia kupitia huduma hiyo na kisha wewe kulipwa kutoka kwenye huduma hiyo.
Ukishakuwa na mpango mzuri wa malipo, kazi yako kubwa inabaki kuandaa masomo na kufanya masoko. Masomo na masoko ndivyo vitaamua ni kiwango gani cha fedha uingize kwa kufanya biashara yako mtandaoni.
Tano; anza na kazana kuwa bora kila siku.
Mabadiliko yoyote yale huwa yana hofu kubwa, hujui ni matokeo gani utapata na hivyo unaona bora kuendelea kufanya ulichozoea. Lakini kwa hali tuliyonayo sasa, huwezi kuendelea na ulichozoea, kwa sababu hakipo tena, hivyo unalazimika kubadilika.
Anza kwa hatua ndogo kisha kazana kuboresha kadiri mwitikio wa wateja unavyokuwa kwenye huduma yako.
Usisubiri mpaka uwe na kila kitu, anza na hatua ndogo.
Mfano unaweza kuanza kwa kuandaa darasa moja ambalo litaenda mubashara kupitia mtandao wa zoom ana whattsapp, kisha ukatengeneza video za matangazo ya darasa hilo na kuziweka mtandaoni pamoja na kulipia ili kuwafikia wengi zaidi.
Unalifanya darasa hilo kuwa la utangulizi na la bure kabisa, kisha wale wanaoshiriki unawakaribisha kwenye madarasa ya kulipia. Pia unahakikisha wote umepata mawasiliano yao ili uendelee kuwashawishi zaidi na zaidi mpaka wajiunge na madarasa yako.
Sita; soma kitabu hiki.
Kama bado hujapata na kusoma kitabu JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA MTANDAONI KWA KUTUMIA BLOG, unapaswa kufanya hivyo mara moja. Kitabu hiki kinakupa mwongozo wa jinsi ya kutengeneza blog na kuitumia kutengeneza hadhira ambayo baadaye unaigeuza kuwa wateja wako. Utajifunza mengi na hatua za kuchukua ili kutengeneza fedha mtandaoni.
Kitabu hiki ni nakala tete na kinatumwa kwa email, gharama yake ni elfu kumi, ila leo utakipata kwa bei ya zawadi, tsh elfu 7 tu. Kukipata tuma fedha kwenda namba 0717396253 kisha tuma email yako na jina la kitabu na utatumiwa.
Kuna fursa nyingi mno kwa kuhamishia biashara yako mtandaoni, kila mtu alipaswa kuwa ameshafanya hivi, lakini kwa sababu ya mazoea wengi hawakufanya. Sasa dunia inatulazimisha kufanya hivyo, usiwe mkaidi tena, kwa sababu ukaidi wako utakuondoa kabisa kwenye biashara.
Anza kuchukua hatua sasa ili kuihamishia biashara yako mtandaoni. Na kama utahitaji huduma ya ukocha katika kutekeleza hili, karibu tuwasiliane kwa namba 0717396253, tuma ujumbe kwa wasap ukisema unahitaji huduma ya ukocha wa kuhamishia biashara yako mtandaoni kisha tutajadiliana na kuona namna gani tunaweza kufanya kazi pamoja kwenye hilo.
Karibu sana.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania