Bila ya changamoto, maisha yanakosa maana. Hebu fikiria kama kila kitu kingekuwa kinaenda kama unavyotaka, nini kingekusukuma kuwa bora zaidi kwenye maisha? Hakuna, ungeishia kulewa na kufanya mambo ya hovyo.
Hivyo changamoto ni kitu muhimu kwenye kila aina ya maisha na wanaofanikiwa siyo wanaozikimbia changamoto, bali wale wanaozikabili na kuzitatua.
Ni kwa sababu hiyo, mimi rafiki yako nimekuwa nakujengea uwezo wa kukabiliana na kila aina ya changamoto kwenye maisha. Kila wiki nakuandalia makala ya ushauri wa changamoto, ambayo inajibu ushauri ambao msomaji mwenzetu ameomba kwa njia iliyo mwisho wa makala hii.
Kwenye makala hii, tunakwenda kupata ushauri wa nyenzo saba unazoweza kuzitumia kufikia utajiri na mafanikio makubwa kwenye maisha yako kwa muda mfupi na bila kutumia nguvu kubwa.
Zingatia, ninaposema muda mfupi simaanishi njia ya mkato, bali muda ambao kwa hali ya kawaida peke yako huwezi, na ninaposema bila kutumia nguvu kubwa simaanishi hufanyi kazi kabisa, ila unapata matokeo makubwa ukilinganisha na kazi uliyoweka.
Kabla hatujaingia kwenye nyenzo hizo saba, tupate maoni ya msomaji mwenzetu ambaye ameandika kuomba ushauri juu ya hili;
Nilikuwa napenda utolee ufafanuzi wa kina jinsi ya kutengeneza utajiri kwa kutumia fedha za watu, muda wa watu na maarifa ya watu ukizingatia kwa dunia ya sasa naona watu wengi wanatajirika kwa muda mfupi kwa kutumia mfumo huo (leverage) – Ramadhani O. S.
Kama tunavyosoma hapa, msomaji mwenzetu ameomba nitolee ufafanuzi wa kina wa jinsi ya kutengeneza utajiri kwa kutumia rasilimali za watu wengine, yaani fedha, muda na maarifa. Hivyo hapa tutakwenda kujifunza aina saba za nyenzo tunazoweza kutumia kufikia utajiri na mafanikio makubwa.
Nyenzo ni muhimu.
“Give me a lever long enough and a fulcrum on which to place it, and I shall move the world.” – Archimedes
Nipe nyenzo yenye urefu wa kutosha na egemeo la kuiweka na nitaweza kuisogeza dunia ni kauli iliyowahi kutolewa na mwanahisabati na mwanafalsafa Archimedes. Ukiichukulia juu juu kauli hiyo huwezi kuelewa nguvu yake, lakini anachomaanisha ni kwamba japokuwa dunia ni nzito na hakuna anayeweza kuisogeza, mtu yeyote akipewa nyenzo ambayo ni ndefu na akiwa na egemeo basi anaweza kuisogeza dunia kwa urahisi.
Kama ulikimbia hesabu na sayansi ya shule za msingi basi hapa nitakukumbusha kidogo kuhusu nyenzo. Kwa lugha rahisi, nyenzo ni mfumo unaowezesha jitihada kidogo kunyanyua mzigo mkubwa. Hivyo wenzo una vitu vitatu, MZIGO, JITIHADA na EGEMEO.
Kwenye kitabu cha The One Minute Millionaire: The Enlightened Way to Wealth kilichoandikwa na Mark Victor Hansen na Robert G. Allen, waandishi wameshirikisha kwamba huwezi kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yako kama utafanya kila kitu peke yako.
Wanatuambia kwamba unahitaji kutumia nyenzo, ambazo zinawezesha jitihada zako kidogo kusukuma mzigo mzito. Mzigo mzito kwako ni ndoto yako ya utajiri na mafanikio makubwa, egemeo ndiyo wewe ambaye unataka kufikia mzigo huo na jitihada na ni zile juhudi unazoweka. Sasa kadiri wenzo unayokuwa mrefu, ndivyo juhudi zako kidogo zinavyoleta matokeo makubwa.
Zifuatazo ni nyenzo saba unazoweza kutumia kufikia utajiri na mafanikio makubwa.
- OPM (Other People’s Money) – Pesa Za Watu Wengine.
Umewahi kusikia kauli inayosema unahitaji pesa ili kupata pesa?
Kama lengo lako ni kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yako, basi jua huwezi kuufikia kwa kutegemea pesa zako mwenyewe. Hata kama utaanza biashara kwa akiba zako, kuna wakati utahitaji kukuza biashara hiyo na fedha itakuwa kikwazo kwako. Hapo ndipo unapopaswa kutumia pesa za watu wengine kama nyenzo ya wewe kufanikiwa.
Katika kutumia pesa za watu wengine, kuna njia mbalimbali.
Njia ya kwanza na iliyozoeleka ni kuchukua mkopo. Unapochukua mkopo kwenye taasisi za kifedha na kwenda kuuzalisha, unatumia nyenzo. Unatumia pesa za watu wengine, kuzalisha faida zaidi, unarejesha fedha hizo na biashara yako inakuwa kubwa.
Njia ya pili ni ushirika na wengine. Unaweza kuwa na wazo la kufanya kitu, lakini peke yako huna fedha za kutosha. Hapa unaweza kutafuta watu wengine na ukashirikiana nao katika kutekeleza wazo hilo.
Njia ya tatu ni kutafuta wawekezaji. Hapa unawapa watu nafasi ya kuwekeza fedha zao kwenye kile unachofanya, wao wanakuwa sehemu ya wamiliki na unapopata faida na wao wanapata faida pia.
Hatua ya kuchukua; kwa lengo lako la utajiri na mafanikio makubwa ulilonalo, jua ni njia ipi utaitumia kupata fedha za wengine na wakati sahihi wa kufanya hivyo. Kuwa makini usikimbilie kuchukua fedha za wengine kabla hujatengeneza mfumo mzuri kwa fedha zako mwenyewe na ukaweza kupata faida ya uhakika.
SOMA; Nafasi Nyingine Ya Kusikiliza Kipindi Cha Redio Cha Elimu Ya Msingi Ya Fedha.
- OPT (Other People’s Time) – Muda Wa Watu Wengine.
Una masaa 24 pekee kwa siku, hata uwe nani, huwezi kuongeza hata dakika moja kwenye siku yako. Hivyo kama unategemea kutumia muda wako pekee kwenye kufikia utajiri na mafanikio, tayari una kikwazo, maana muda una ukomo.
Kuondokana na ukomo huo, unaweza kutumia nyenzo ya muda wa watu wengine. Hapa unatumia muda wa watu wengine katika kukamilisha majukumu muhimu kwako, badala ya kutegemea muda wako mwenyewe.
Kwenye kutumia muda wa watu wengine, unawapa majukumu wale ambao ni wataalamu au wazoefu wa vitu fulani badala ya kuhangaika navyo mwenyewe.
Mfano badala ya kuandaa hesabu zako mwenyewe, unampa mhasibu akuandalie. Badala ya kutengeneza mikataba yako mwenyewe, unampa mwanasheria akuandalie. Hii inakuokolea wewe muda wa kujifunza vitu hivyo mpaka ujue na muda wa kufanya kazi hizo, kitu kinachokupa muda mwingi wa kufanya yale muhimu na yenye manufaa makubwa.
Hatua ya kuchukua; orodhesha majukumu yote unayokazana kuyafanya sasa, ambayo hayaendani na lile lengo lako kuu unalotaka kufikia au eneo unalotaka kubobea. Kisha tafuta watu watakaokupa muda wao kufanyia kazi maeneo hayo na wewe kuwalipa kwa kiwango kidogo ili muda huo uutumie kwa manufaa zaidi.
- OPW (Other People’s Work) – Kazi Za Watu Wengine.
Hii ni sehemu nyingine ya nyenzo, ambayo inaendana na muda, ila hapa unategemea kazi za watu wengine. Ukitaka ufanye wewe mwenyewe majukumu yako yote ya kazi hutaweza, muda una ukomo na nguvu zako hazidumu milele.
Kuondoka na kikwazo hicho unapaswa kutumia nyenzo ya kazi za watu wengine.
Kama unafanya kazi mwenyewe kwa masaa kumi kwa siku, unaishia kuwa na masaa kumi ya kazi kwa siku. Lakini ukiajiri watu 10 wa kukufanyia kazi na kila mmoja akafanya kazi masaa 10 kwa siku, unakuwa na masaa 100 ya kazi kwa siku. Hebu ona hapo, kutoka masaa 10 mpaka 100, ni nyenzo kubwa hiyo.
Hatua za kuchukua; kwenye shughuli zako, iwe ni biashara au kujiajiri, weka mfumo ambao utawezesha watu wengine kukusaidia majukumu na kuleta matokeo makubwa kuliko kufanya wewe peke yako.
SOMA; USHAURI; Mfumo Bora Wa Kuajiri Utakaokuwezesha Kupata Wafanyakazi Bora Na Waaminifu.
- OPE (Other People’s Experiences) – Uzoefu Wa Watu Wengine.
Mafanikio yanahitaji uzoefu mkubwa kwenye lile eneo ulilochagua. Unaweza kupata uzoefu huo kwa kujaribu na kukosea, kitu ambacho kitakuchukua muda mrefu na ambao huna.
Kuondokana na ukomo huo, unaweza kutumia nyenzo ya uzoefu wa watu wengine. Hapa unawaangalia wale ambao wamefika kule ambapo unataka kufika, kisha kujifunza kwa uzoefu wao. Kitu ambacho wao walitumia miaka 10 kujifunza kwa kujaribu na kushindwa, wewe unaweza kujifunza na ukawa umeokoa miaka 10.
Njia za kutumia uzoefu wa wengine ni kuwa na Menta, Kocha au kujifunza kupitia vitabu na mafunzo ya watu wengine. Menta anakuwa mtu ambaye ameshafika kule unakotaka kufika na anakuwa tayari kukushika mkono. Kocha ni mtu ambaye ana uzoefu kwenye eneo husika na kuwa tayari kukusimamia kwenye eneo hilo.
Hatua za kuchukua; hakikisha unakuwa na menta na kocha katika safari yako ya mafanikio. Watu hao watakusaidia kupata uzoefu ambao huna kwa sasa. Pia jifunze kuhusu wengine waliofanikiwa kwenye eneo unalofanyia kazi kupitia vitabu na mafunzo mbalimbali.
- OPI (Other People’s Ideas) – Mawazo Ya Watu Wengine.
Kuna mawazo mengi mazuri ambayo yameshafanyika kwenye maeneo mengine ila pale ulipo sasa mawazo hayo bado hayajatumika. Badala ya kung’ang’ana mpaka upate wazo lako la kipekee, unaweza kutumia mawazo ambayo yameshafanya kazi kwenye eneo jingine na kuyaboresha kwenye eneo ulilopo.
Hiyo ndiyo nyenzo ya mawazo ya watu wengine, kuangalia kile ambacho wengine wanafanya na kuona unawezaje kuyafanya kwa ubora zaidi kwa pale ulipo wewe.
Hatua za kuchukua; badala ya kusubiri mpaka upate mawazo mazuri, angalia mawazo mengine ambayo yamefanikiwa sana, kisha ona ni jinsi gani unaweza kutumia mawazo hayo kwenye kile unachofanya. Mtandao wa intaneti umerahisisha sana hili angalia mifumo ambayo imefanya kazi kwa mafanikio kwenye maeneo mengine na iboreshe ilete matokeo mazuri kwenye kile unachofanya.
- Scalable Production & Distribution – Uzalishaji Na Usambazaji Usio Na Ukomo.
Kama unatoa huduma ambayo inahitaji uwepo wako wa moja kwa moja, unajiwekea ukomo, kwa sababu huwezi kuwa kila mahali kwa wakati mmoja.
Ili kuondoa kikwazo hicho, unapaswa kuwa na uzalishaji na usambazaji usio na ukomo.
Mfano badala ya kushauri mtu mmoja mmoja, andika kitabu kinachobeba ushauri muhimu unaotoa. Kwa zama hizi za mtandao, hakuna ukomo wa kuzalisha na kusambaza kitabu hicho. Unaweza kukiweka kwa nakala tete na ukakiuza kwa muda mrefu na kikafika kila eneo duniani.
Hatua ya kuchukua; kwa bidhaa au huduma unayotoa, ondoa ukomo uliopo kwenye uzalishaji na usambazaji, hakikisha inaweza kuzalishwa na kusambazwa kwa wingi kadiri inavyohitajika.
SOMA; USHAURI; Jinsi Ya Kuihamishia Biashara Yako Mtandaoni, Kuwafikia Wengi Na Kuingiza Kipato Zaidi.
- Scalable Customer Base – Wateja Wasio Na Ukomo.
Kama biashara unayoifanya inalenga watu waliopo kwenye eneo fulani pekee, unakuwa na ukomo, maana watu hao wakiisha umemaliza wateja. Pia kama wateja wanahitaji kuja eneo moja unakuwa na ukomo. Mfano kama una mgahawa wenye nafasi 50 za kukaa wateja, wakishakaa wateja 50 huwezi kuhudumia tena wateja wengine, ni mpaka hao waondoke.
Kuondokana na ukomo huo, unapaswa kutumia nyenzo ya wateja wasio na ukomo, unaifanya biashara yako kwa namna ambayo unaweza kuhudumia wateja wengi kadiri wanavyohitaji bila ya kuwepo kwa kikwazo chochote.
Mtandao wa intaneti umerahisisha sana hili, tengeneza biashara ambayo inaweza kufanyika kwa mtandao wa intaneti na utaondoa ukomo wa wateja.
Hatua za kuchukua; kwa bidhaa au huduma unayotoa, ondoa ukomo wa wateja, ifanye iweze kupatikana kwa yeyote na popote alipo. Hata kama kwa sasa unalenga walio eneo husika, anza kutengeneza njia ambazo walio mbali wanaweza kuipata pia kisha tumia mtandao wa intaneti kukamilisha hilo.
Rafiki, hapa umejifunza nyenzo saba unazoweza kutumia ili kufikia utajiri na mafanikio makubwa, kwenye kila nyenzo umejifunza hatua za kuchukua, fanyia kazi hatua hizo na utaweza kufikia ndoto yako kubwa.
Nakutakia utekelezaji mwema wa yale ambayo umejifunza,
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani
TOA CHANGAMOTO YAKO USHAURIWE
Kama una changamoto ambayo inakuzuia kufikia malengo yako unaweza kuitoa kwa kubonyeza maandishi haya na kujaza fomu. Changamoto yako inaweza kuwa moja ya makala zijazo kila siku ya jumatatu.
Kupata vitabu na uchambuzi wa kina wa vitabu jiunge na channel ya SOMA VITABU TANZANIA kwa kufungua kiungo hiki; www.t.me/somavitabutanzania
