Mpendwa rafiki yangu,

Habari njema ni kwamba kila mtu ni kiongozi wa maisha yake. Watu wengi wanafikiri kuwa kiongozi ni mpaka kuongoza kundi kubwa la watu, hapana, hata kujiongoza wewe mwenyewe kila siku ni uongozi pia. Kama wewe ni baba basi wewe ni kiongozi wa familia yako.

Kwenye kila kikundi cha watu ili mambo yaende sawa lazima pawepo na viongozi watakaowaonesha wengine dira. Mahali ambako panakosa uongozi ni mahali ambapo hapana usimamizi na sehemu ikikosa usimamizi panakua kama chooni yaani kila mtu yuko huru kufanya kile anachojisikia kufanya.

cropped-mimi-ni-mshindi

Kila sehemu lazima kuna kuwa na sheria na utaratibu ambao unawaongoza watu, hata serikali inaendeshwa kwa katiba, wanafuata mwongozo siyo kila mtu anajiamulia vile anavyotaka yeye.

Kwa mfano, hivi ingekuwa kila mtu ni mtoa amri jeshini hali ingekuwaje? Vipi katika nchi? Familia au hata kazini kwako? Kila sehemu huwa kuna mtu mmoja wa mwisho kutoa amri ila kila mtu angekuwa anatoa amri basi dunia hii ingekuwa imechafuka vibaya sana na tusingeona kama dunia ni mahali salama pa kuishi bali kinyume chake.

Lazima tukubali kufuata taratibu elekezi ili mambo mengine yaweze kwenda, na mara nyingi hatuwezi kwenda kinyume na sheria za asili kwani ukijaribu kwenda kinyume na sheria za asili maana yake ni unataka kuibadili dunia na ni kitu ambacho hata hakiwezekani.

Kitu cha kukiepuka kwa kila kiongozi kwenye uongozi wake ni kuepuka kufanya maamuzi yoyote kwa hisia. Viongozi wengi huwa wanachemka eneo hili , wengi wanapenda kuahidi wakiwa na hisia na hapa ndipo  ugumu wa utekelezaji unapokuja katika maisha ya uongozi.

Tunatakiwa kujifunza kuwa ukiwa na hisia, iwe ni furaha, upendo, hasira kamwe usiahidi. Subiri wakati ukiwa umetulia na akili za kawaida maana hisia huwa zinawaendesha watu vibaya na kupelekea kuahidi mambo ambayo hutoweza hata kuyatekeleza.

Tano Za Juma Kutoka Kitabu The Laws Of Human Nature (Sheria Kumi Na Nane Za Asili Ya Binadamu Na Jinsi Ya Kuzitumia Kuwa Na Maisha Bora)

Mara nyingi hisia zinapokuwa juu, fikra zinakuwa chini hivyo uwezo wa kufikiri unakuwa  chini.  Na tunatakiwa kufanya maamuzi kwa kutumia akili na siyo hisia hata siku moja. Hisia zitakupelekea kuchukia hata kiti cha uongozi ulichokalia.

Mara nyingi unatakiwa kutulia kwanza, usiwe na papara hata siku moja kwenye maamuzi ya uongozi fikiri kwanza. Ukiwa kwenye utulivu utapata majibu bora sana.

Hatua ya kuchukua leo; Ili usionekane mwongo, usiahidi ukiwa na hisia maana unapoahidi na hisia itakusumbua baadaye kwenye kutekeleza kama kiongozi.

Kwahiyo, unaweza kutumia mbinu hata katika mahusiano yako, watu ambao uko nao katika mahusiano ukiwa ni mtu wa kuahidi ukiwa na hisia utajikuta una madeni mengi ya kutekeleza. Ni vema kutulia na kufanya maamuzi na kuahidi wakati huna hisia.

Makala hii imeandikwa na

Deogratius Kessy, ambaye ni mwandishi, mwalimu na mjasiriamali. Unaweza pia kujifunza mengi kutoka kwake kupitia mafundisho anayoendelea kuyatoa kupitia mtandao wake wa www.mtaalamu.net/kessydeo, vitabu na kwenye klabu yake ya MIMI NI MSHINDI.  Karibu sana.

Ukawe na siku bora sana rafiki.

Rafiki na mwalimu wako,

Mwl, Deogratius kessy

0717101505/0767101504

deokessy.dk@gmail.com // kessydeo@mtaalamu.net

Asante sana