Kila mtu anayeingia kwenye ujasiriamali na biashara, moja ya malengo yake ni kukua kupitia biashara hiyo. Wajasiriamali wengi huanza kidogo wakitegemea kwamba kwa kufanya juhidi na maarifa watakua na kufikia nafasi kubwa sana.
Kwa Bahati mbaya sana hiki sio kinachotokea kwa wajasiriamali wengi. Wajasiriamali wengi wanaishia kuendesha biashara ambazo zinadumaa au kufa kabisa baada ya muda fulani. Biashara nyingi zinazoanzishwa hazichukui muda mrefu kabla ya kudumaa na kufa kabisa. Kuna mambo mengi sana yanayosababisha hali hii ya biashara kufa.
Ili kuepuka wewe mjasiriamali kufikia hali hii au kama umeshaingia kukuwezesha kuondoka kwenye kifo cha biashara yako, leo utajifunza mbinu sita muhimu za kuiwezesha biashara yako kukua.
Mbinu ya kwanza; ajiri watu sahihi.
Hakuna sehemu muhimu kwenye ukuaji wa biashara yako kama watu unaowaajiri. Maana watu unaowaajiri wanaweza kukuza au kuua biashara yako. Hakikisha unafanya vizuri zoezi la kuajiri na kuwaajiri watu ambao wanapenda kweli kufanya kazi unayowaajiri wafanye. Kama mtu anapenda anachokifanya anakuwa na hamasa kubwa na pia anakuwa mbunifu. Ila kama utaajiri mtu ambaye hapendi anachofanya, atakuwa mtu wa kusukumwa ili atomize majikumu yake kitu ambacho kitakurudisha wewe nyuma.
Mbinu ya pili; Punguza hatari.
Kuwa kwenye biashara ni hatari kwa sababu jambo lolote linaweza kutokea na ukapata hasara kubwa sana. Hakuna anayeweza kudhibiti kila kitu kwenye biashara yake, hivyo kila mjasiriamali yupo kwenye aina fulani ya hatari. Ili uweze kukuza biashara yako zaidi hakikisha unapunguza mazingira haya ya hatari. Kwa kuwa huwezi kuondokana nayo kabisa, jaribu kupunguza kila linalowezekana. Kwa mfano kuepuka kupoteza biashara yako yote inapotokea hali ya hatari unaweza kuikatia biashara yako bima. Kwa hali hii utakuwa na uhakika wa kuweza kusimama tena hata mambo yakienda vibaya.
Mbinu ya tatu; Kuwa tayari kubadilika.
Tunaishi kwenye zama ambazo mambo yanabadilika kwa kasi sana. Kitu ambacho kina faida leo, mwaka kesho kinaweza kisiwepo kwenye biashara kabisa. Ili uweze kukuza biashara yako kuwa mdadisi wa mambo yanavyokwenda na pale unapoona inabidi fanya mabadiliko. Watu wengi hawapendi mabadiliko, lakini inapotokea kwamba mabadiliko ni lazima hakuna anayeweza kupinga. Kama ukipingana na mabadiliko utaishia kuachwa nyuma. Ona dalili za mabadiliko mapema na kuwa tayari kubadilika.
Mbinu ya nne; Jiridhishe na huduma kwa wateja.
Wateja ambao wameshapata huduma au bidhaa kwenye biashara yako, wanaweza kuwa chanzo cha kujenga biashara yako au kuiua. Kama wateja wanapata huduma nzuri ni dhahiri kwamba watawaambia na wenzao nao watakuja kwenye biashara yako. Kama wateja watapata huduma mbovu watawaambia wengi zaidi na hivyo utakosa wateja wengi. Kwenye dunia ya sasa ambayo taarifa zinasambaa kwa sekunde, mteja mmoja ambaye hajaridhishwa anaweza kusambaza habari kwa wateja elfu moja. Jiridhishe kwamba wateja wako wanapata huduma bora nah ii itakuwezesha kukua zaidi.
Mbinu ya tano; Wekeza faida kwenye biashara yako.
Katika makala yaliyopita hapa kwenye KISIMA CHA MAARIFA, tulijadili umuhimu wa kuwekeza faida kwenye biashara yako. Hii ni mbinu muhimu sana ya biashara yako kuweza kukua zaidi. Hakikisha unawekeza sio chini ya asilimia 20 ya faida unayopata kwenye biashara yako. Kama utategemea biashara ikupatie faida ambayo unaitumia yote unajiandaa kuanguka na biashara yako.
Mbinu ya sita; Mara zote fikiria mbele.
Kwanza kabisa huwezi kukuza biashara yako kama huangalii mbele, kama huna picha kubwa ya kesho. Kama unafanya biashara kwa kuangalia leo tu itakuwa rahisi kwako kutumia faida yote unayopata na hata kushindwa kufanya maamuzi muhimu kwa ajili ya ukuaji wa biashara yako. Mara zote angalia miaka mingi ijayo biashara yako itakuwa wapi. Kabla hujafanya maamuzi yoyote makubwa jiulize je maamuzi haya yataisaidiaje biashara hii miaka mitano au kumi ijayo. Kwa kujiuliza hivi utafanya maamuzi sahihi yatakayokuwezesha kukua.
Ukuaji wa biashara yako sio kitu ambacho kinatokea kwa haraka kama wengi wanavyofikiri. Ni kitu ambacho kinahitaji muda. Tumia mbinu hizi sita na kuwa na uvumilivu kwenye biashara yako, utafikia mafanikio makubwa.
Nakutakia kila la kheri kwenye mafanikio ya biashara yako.
TUPO PAMOJA.