Habari za wakati huu rafiki?

Karibu tena kwenye mazungumzo yetu haya muhimu sana kati yangu mimi na wewe rafiki yangu. Na kupitia mazungumzo haya ya leo naomba nikukumbushe kitu kimoja muhimu sana ambacho tumekuwa tunakiongea mara kwa mara.

Pamoja na mipango mizuri ambayo unaweka kila siku.

Pamoja na mbinu mpya unazotafuta kila siku,

Lakini bado kuna vitu muhimu havitabadilika, na kimoja wapo ni wewe kuweka juhudi.

Ni lazima uweke kazi, ni lazima uweke juhudi, ni lazima jasho likumwagike, iwe la mwili, la akili au yote kwa pamoja.

Ni lazima uwe tayari kujisukuma kufanya hata pale ambapo hujisikii kabisa, na hii itakutokea mara nyingi kwenye safari yako hii ya mafanikio.

Ni lazima uwe tayari kuendelea kuweka kazi hata kama huoni yale majibu uliyokuwa unategemea kupata, hasa siku za mwanzoni.

Na pia ni lazima uwe tayari kuendelea kuweka juhudi kubwa zaidi hata baada ya kuanguka na kushindwa.

Ukweli ni kwamba hakuna kitu kitakachotokea mpaka pale kazi itakapofanywa.

Hata upange vizuri kiasi gani, hata uongee kiasi gani, hata uwe na mbinu bora kiasi gani, ili kitu kitokee ni lazima kazi ifanywe.

Ndio maana leo hii nakukumbusha tena, japo tumekuwa tunajadili hili mara kwa mara, fanya kazi, weka juhudi, zaidi na zaidi, na usikate tamaa.

Hakuna kitu kirahisi.

Moja ya vitu vinavyowarudisha watu nyuma kwenye ufanyaji wa kazi ni kufikiri kwamba kuna kazi fulani rahisi na nyingine ngumu. Na mara nyingi ile kazi unayofanya wewe ndio unaona ngumu, wakati ile wanayofanya wengine unaona ni rahisi.

Ukweli ni kwamba hakuna kazi rahisi, kazi zote ni ngumu. Kinachotufanya tuweze kuendelea kufanya kazi pamoja na ugumu wake ni kule kupenda kufanya kitu kile, au kupenda msaada ambao watu wanaupata kupitia kila unachofanya.

Unaweza kuwa kazi yako ni kufagia ofisi, na ukajiona wewe ndio una kazi ngumu sana, na kutamani kazi ya meneja wa ofisi ile. Lakini huwezi kujua ugumu wa kazi ya meneja, unaweza kuona amekaa ofisini siku nzima lakini hujui mzigo mzito aliobeba, hujui makubwa sana yanayotegemewa kuhusu yeye ambayo hana hakika kama ataweza kuyatekeleza.

Kwa kifupi hii game sio rahisi, lakini inapokuwa ni kitu tunapenda basi tunaendelea kuweka juhudi.

Unaweza kuona labda mimi ninayeandika kazi yangu ni rahisi sana, lakini huwezi kujua ugumu wa kuandika kila siku, yaani ni kila siku, siku 365 kwa mwaka, na uandike kitu ambacho mtu akisoma anaweza kuondoka na kitu cha kufanyia kazi.

Unaweza kuona labda kiongozi fulani kazi yake ni rahisi, yeye natoa tu maelekezo na watu wanafanya. Lakini sio rahisi kama unavyofikiri. Utakuta kiongozi huyu anakutana na vikwazo vikubwa sana vinavyompa wakati mgumu na kushindwa kufanya baadhi ya maamuzi.

Kwenye ajira na kwenye biashara.

Nimekuwa nakutana na watu wengi ambao wameajiriwa na wengi utasikia wakisema kazi hii imenichosha, bora niingie kwenye biashara, nifanye mambo yangu kwa uhuru. Wengi hufikiri kama kazi ni ngumu basi wakiingia kwenye biashara mambo yatakuwa yamenyooka. Wanafikiri wakishaanza biashara basi wateja watakuwa wamejipanga kuwasubiri, au kugombania kile ambacho wanatoa.

Mawazo mazuri sana, ila nikuambie ya kwamba kwenye biashara yako utahitaji kuweka kazi mara mbili ya unayoweka sasa kwenye ajira yako. kwenye ajira ulikuwa unafanya kazi labda saa mbili asubuhi mpaka saa kumi jioni, kwenye biashara yako utaanza kufanya kazi saa kumi asubuhi mpaka saa sita ya usiku. Kwenye ajira unaweza kupata nafasi ya kufanya kazi siku tano kwa wili na likizo ya mwezi kwa mwaka. Kwenye biashara utafanya kazi siku saba za wiki na miezi yote ya mwaka, hasa mwanzoni.

Hivyo usifikiri kuna mahali ambapo ukikimbilia hutaweka kazi, kila mahali kunakutaka wewe uweke kazi, na sio kazi ya kitoto, kazi ya maana, kama unataka kufikia mafanikio makubwa.

Kaa chini na fanya kazi. Nukta.

Nimalize kwa kusema kwamba, kaa chini na ufanye kazi. Pamoja na kelele zote utakazopiga, pamoja na mbinu zote utakazotafuta, pamoja na mengine mengi utakayotamani kufanya, lakini mwisho wa siku kaa chini na ufanye kazi.

Naamini kazi yako unaijua vizuri, basi ifanye, na ifanye kwa uwezo wako wote.

Kama unafagia, basi hakikisha unafagia vizuri sana kiasi kwamba anayekaa ulipofagia aone ni tofauti kabisa na sehemu nyingine.

Kama unafundisha, fundisha vizuri sana mpaka kila anayekufuatilia unachofundisha aelewe vizuri.

Kama unaandika andika, yaani kaa chini na andika, na andika kitu ambacho kina mchango kwa mtu mwingine.

Kama unafanya biashara yoyote ifanye kwa ubora wa hali ya juu sana, hakikisha wateja wako wanapata kile ambacho kinawatatulia matatizo yao.

Kaa chini na fanya kazi. Usianze kupiga kelele kwamba kazi yako ni ngumu, hakuna mtu aliyekuambia itakuwa rahisi.

Usianze kupiga kelele kwamba kazi za wengine ni rahisi, hujajaribu kuvaa viatu vyao.

Na usianze kupiga kelele kwamba dunia haina usawa, labda pamoja na juhudi kubwa bado unashindwa, hakuna aliyekuahidi usawa.

Fanya kazi rafiki yangu, hakuna mbadala kwenye hilo.

Je utaanza kufanya kazi leo? najua ulikuwa unafanya kazi, namaanisha kufanya kwa mtazamo huu mpya tulioshirikishana hapa?

MAKALA MUHIMU ZA KUSOMA;

Umeshajiandikisha kwenye semina ya kuufanya mwaka 2016 kuwa mwaka wa kipekee zaidi kwako, mwaka wa kuleta mabadiliko kwenye kazi na maisha yako? kama bado fanya hivyo leo, nafasi zinajaa haraka. Fungua hapa kujiunga na semina hii kubwa sana kwa 2016; Karibu Kwenye Semina; 2016 NI MWAKA WANGU WA UBORA WA HALI YA JUU.

Tarehe 09/12/2015 badala ya kusherekea uhuru wa nchi yetu kwa sherehe tuliusherekea kwa kufanya usafi. Lakini kuna usafi muhimu sana kwako ambao huenda hujapata nafasi ya kuufanya. Soma hapa na ujue maeneo matano muhimu sana kwenye maisha yako ambayo unahitaji kuyafanyia usafi leo; Siku Ya Usafi Kitaifa; Usafi Muhimu Sana Kwako Kufanya Kwenye Maisha Yako Ili Kufikia Mafanikio Makubwa.

Nakutakia kila la kheri katika safari hii uliyochagua ya kuyafanya maisha yako kuwa bora kila siku.

Rafiki na Kocha wako.,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

AMKA CONSULTANTS