Maisha yetu sisi wanadamu ni kitu kigumu sana kukielewa vizuri. Kwa kiingereza unaweza kusema ni complex.
Na ugumu huu wa kuyaelewa maisha ndio unayafanya kuwa bora zaidi.
Kila mmoja wetu ana upweke fulani ndani yake, na kila anapokuwa kwenye upweje huu, huzuni kubwa huwa inamwingia.
Haijalishi maisha yako ni bora au mabaya kiasi gani, wote tuna upweke huu na huzuni hii pia. Na mara zote huzuni huingia pale unapopata nafasi ya kuwa mpweke.
Ili kuepuka huzuni hii huwa tunakimbia sana upweke, kwa kuhakikisha tumezungukwa na watu, marafiki, ndugu na kadhalika. Na wakati mwingine mtu anaondoa ukweke huu kwa kuhakikisha kuna mtu anayempenda kweli na atakuwepo pale kwa jambo lolote lile.
Lakini upweke huu na huzuni sio vitu vibaya, na hivyo hatutakiwi kuvikimbia. Badala yake tunahitaji kuvikaribisha kwa kipindi fulani. Unapoikaribisha huzuni unapata nafasi nzuri ya kuweza kushukuru kwa yale mambo mazuri yanayoendelea kwenye maisha yako, na kwa kushukuru kwa haya mazuri basi unayapata zaidi na zaidi.
Changamoto kubwa ya dunia ya sasa ni kwamba kuna kitu kinaitwa simu, hasa simu janja(smartphone) hizi zimekuja kuharibu kabisa ile nafasi yetu ya kuwa na ukweke na kuikaribisha huzuni.
Kwa sababu kwa sasa hata kama hakuna anayekuzunguka huwezi kuwa mpweke tena. Muda wowote unaweza kuingia kwenye mitandao ya kijamii na ukaanza kuangalia maisha ya watu yanakwendaje. Au ukatuma ujumbe kwa watu wengi na watakaojibu mkaanza kupiga soga na mengine mengi.
Hizi simu zimekuwa sehemu ya sisi kukimbia upweke wetu na hili limetugharimu sana kuweza kuyafurahia maisha yetu. Hii ni kwa saba u kadiri unavyokosa muda wa peke yako wa kutafakari maisha yako, ndivyo inavyokuwia vigumu kuyathamini na kuona kuna vitu vingi vya kushukuru. Badala yake unakuwa tayari kulalamika kwa kila kitu.
Pata muda wa kuwa mpweke, kila siku, hata kama ni kwa dakika chache. Kwenye muda huo hakuna simu wala hakuna mtu mwingine, ni wewe tu. Kwa njia hii utapata nafasi ya kujijua vizuri na kuweza kushukuru kwa maisha yako ambayo ni bora sana kuliko unavyofikiri sasa.
Ni kupitia huzuni na upweke ndio tunaipata furaha ya kweli kwenye maisha yetu. Lakini kwa sababu wengi tunavikimbia vitu hivyo viwili, tunajinyima nafasi ya kufikia furaha ya kweli.
SOMA; KUJIAMINI; Umuhimu Wa Tabia Ya Kujiamini.
TAMKO LANGU;
Najua maisha yangu yana upweke na huzuni, lakini nimekuwa na kimbia vitu hivi viwili kila siku. Nimejifunza ya kwamba vitu hivi viwili sio vibaya kwenye maisha yangu, bali ni vizuri sana kama nitaweza kuvitumia vizuri. Kuanzia sasa nitatenga muda wa kuwa mpweke kila siku na kuikaribisha huzuni. Kwa njia hii nitapata nafasi ya kutafakari maisha yangu na kushukuru kwa maisha niliyonayo.
NENO LA LEO.
Every human walks around with a certain kind of sadness. They may not wear it on their sleeves, but it’s there if you look deep.
Taraji P. Henson
Kila binadamu anatembea na huzuni fulani kwenye amisha yake. Inaweza isionekane kwenye miili yao, lakini huzuni ipo ndani yao, kama ukiangalia kwa undani.
Upweke na huzuni ni sehemu ya maisha yetu, tusivikimbie, badala yake tuvitumie kufikia furaha ya kweli.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.