Katika safari hii ya kuboresha maisha yako na kufikia mafanikio makubwa, kuna tabia nyingi sana unahitaji kuzibadili. Hii ni kwa sababu kuna tabia ambazo ulikuwa umeshajitengenezea ambazo zinakuwa kikwazo kwako kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako.
Lakini zoezi la kubadili tabia siyo rahisi. Wanasema tunajenga tabia halafu baadaye tabia zinatujenga. Hii ina maana kwamba tabia inaanza kidogo kidogo na baadaye inakomaa kiasi kwamba huwezi tena kuivunja tabia hiyo. Leo tutajadili kinachokuzuia kubadili tabia usizopenda ili uweze kujua hatua za kuondokana na tabia yoyote mbaya.
Kila tabia ambayo unayo, iwe nzuri au mbaya, kuna kitu kizuri unakipata kwenye tabia hiyo. La sivyo usingejijengea tabia hiyo. Kuna kitu kizuri, hata kama ni kidogo sana au cha muda mfupi sana, ambacho unakipata kwa tabia hiyo. Na kitu hiki ndiyo kinakusukuma wewe kuendelea kufanya tabia.
Hivyo unapotaka kubadili tabia yoyote, jiulize kwanza ni kipi kizuri unakipata kwenye tabia hiyo. Kijue kile kinachokusukuma kuendelea na tabia hiyo. Ukishakijua jua ni nini mbadala wake. Jua kwa tabia mpya unayotaka kutengeneza, unawezaje kupata kile ambacho unapata kwa sasa. Na ukianzia hapo itakuwa rahisi sana kubadili tabia yoyote ambayo inakurudisha nyuma.
Kwa mfano, kama una tabia ya kuahirisha mambo, utakuwa unafurahia kufanya hivyo kwa sababu hutaki kusumbuka kwa sasa, hutaki kuanza kufanya kitu kikubwa ambacho kitakufanya uache kufanya vitu vingine. Hivyo unaweza kubadili tabia hii kwa kugawa kile unachotaka kufanya kwenye mafungu madogo madogo sana, yanayochukua muda mfupi sana kufanya, na ukayafanya kisha ukaendelea na mambo yako mengine. Baada ya muda utajikuta umeshakamilisha jambo ulilokuwa unaona ni kubwa.
SOMA; Kabla Hujakazana Kubadili Tabia, Badili Hiki Kwanza….
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba kinachonizuia kubadili tabia nisizozipenda ni yale mambo mazuri ninayoyapata kwenye tabia nisiyoipenda. Na sasa nimejua ya kwamba ili niweze kuondokana na tabia hizi nisizozipenda nahitaji kutafuta kizuri kwenye tabia ninayotaka kujitengenezea. Nitafanya hivi ili kuondokana na tabia zote mbaya.
NENO LA LEO.
The only proper way to eliminate bad habits is to replace them with good ones. Jerome Hines
Njia pekee na sahihi ya kuondokana na tabia mbaya ni kuzibadili kwa tabia nzuri.
Kama una tabia yoyote mbaya ambayo ungetaka kuibadili, angalia ni kipi kizuri unakipata kwenye tabia hiyo na angalia utakipataje kwenye tabia mpya unayotaka kujijengea.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.