Unapojilinganisha na wengine, kwa njia yoyote ile unakata tamaa. Kwa sababu hata uwe bora kiasi gani, hata uwe unaweza kiasi gani, kuna ambao wanaweza kuliko wewe. Hivyo unapojilinganisha, utaona kama wewe siyo kitu, na kukata tamaa ya kuendelea kuweka ubora, hasa pale ambapo unakuwa umezidiwa sana na wengine. Hivyo basi acha kabisa kujilinganisha na wengine, kwa namna yoyote ile, haitakusaidia.
Unapokuwa mnyenyekevu unajifunza. Unajifunza mambo mengi sana, kuliko pale unapokosa unyenyekevu na kujiona unajua au kuweza kila kitu. Unyenyekevu ni muhimu sana kwenye maisha yako, kwani pia utaimarisha mahusiano yako na watu wengine, na utajifunza mengi zaidi kupitia wengine na kila kinachoendelea kwenye maisha yako. hivyo basi kuwa mnyenyekevu na utajifunza mengi.
Unapokuwa mdadisi unakuwa bora zaidi kila siku zaidi ya siku za nyuma. Maana ni kupitia udadisi unapata njia bora za kufanya kitu. Kwa kuwa mdadisi utajua kwa nini unafanya kitu fulani na ni njia zipi mbadala za kufanya kitu hiko. Na hapa ndipo utakapokuwa bora zaidi na zaidi, kupitia udadisi. Hivyo basi kuwa mdadisi na utakuwa bora kila siku.
Usijilinganishe na wengine, kuwa mnyenyekevu na kuwa mdadisi, maisha yako yatakuwa bora na yenye mafanikio makubwa.
SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Lipa Sasa Au Utalipa Baadae(Kwa Riba).
TAMKO LANGU;
Nimejikumbusha ya kwamba kujilinganisha na wengine ni kujitakia kukata tamaa kwa sababu kuna watu ambao wako vizuri kuliko mimi. Na pia nimejifunza kuwa mnyenyekevu kutanisaidia sana kujifunza. Na udadisi utanifanya niwe bora kila siku. Hivyo nimeamua kuacha kujilinganisha na wengine, kuwa mnyenyekevu na kuwa mdadisi. Nina hakika maisha yangu yataendelea kuwa bora kila siku.
NENO LA LEO.
“A humble man will always receive the best that others have to offer; for he recognizes the truth”
― Jeremy Aldana
Mtu mnyenyekevu mara zote anapokea kilicho bora kutoka kwa wengine kwa sababu anaujua ukweli.
Mara zote kuwa mnyenyekevu, utajifunza mengi zaidi na maisha yako yatakuwa bora zaidi.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.