Lakini siyo mpango.
Hamasa ni nzuri sana, inaweza kukuondoa kwenye hali ya kukata tamaa na ukarudi kwenye mapambano ya kukamilisha ndoto zako.
Lakini hamasa siyo mpango, licha ya kuwa na hamasa, unahitaji kuwa na mpango mzuri, mpango bora ambayo utakufikisha kule unakotaka kufika.
Wengi husahau hili na kuangalia hamasa pekee. Na kwa kuwa mara nyingi hamasa huwa haidumu muda mrefu, basi watu hurudi kwenye kutafuta hamasa kila mara, na hili linawaondoa kwenye kutekeleza kile walichohamasika kufanya.
Hamasa ni muhimu, lakini kile utakachokwenda kufanya na hamasa hiyo ndiyo muhimu zaidi. Usiseme tu nimehamasika sana, bali sema nimeweza kufanya hiki kwa hamasa niliyopata.
Sijali ujumbe huu umekuhamasisha kiasi gani, ninachojali ni unakwenda kufanya nini baada ya kusoma ujumbe huu. Je unakwenda kuanza kile ulichokuwa unasita kuanza muda mrefu? Je unakwenda kumalizia kitu ambacho ulikuwa umeacha kufanya? Unafanya nini na hamasa ndiyo kilicho muhimu zaidi.
Itumie hamasa kuwa bora sana kwenye kile ambacho tayari umeshakuwa au unataka kuwa. Hamasa ilete matunda yanayoonekana na siyo maneno matupu.
TAMKO LANGU;
Nimejifunza ya kwamba hamasa ni nzuri sana, lakini siyo mpango. Ni vizuri nikawa na hamasa, ila muhimu zaidi ni nimefanya nini kwa hamasa niliyokuwa nayo. Kile ninachofanikisha kufanya ni muhimu zaidi. Mwisho wa siku unahitaji kutuonesha ni kipi ulichofanya, na siyo kutuhadithia ni hamasa kiasi gani umekuwa nayo.
NENO LA LEO.
“If every day at work feels like a Friday, then you are doing what you were meant to do.” ― Alan W. Kennedy
Kama kila siku kwenye kazi yako unajisikia ni kama siku ya Ijumaa, basi unafanya kazi ambayo ndiyo muhimu sana kwako.
Unahitaji msukumo kutoka ndani, na mipango mizuri ili kuweza kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako. hamasa peke yale haitoshi, tunataka kuona umefanya nini na hamasa uliyonayo.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.