Tunaishi kwenye jamii ambapo kufanya makosa ni jambo linalopewa mtazamo hasi. Kwamba anayefanya makosa hajui, au ni mzembe au hayupo makini. Na hivyo kila mmoja wetu anakazana kutokufanya makosa. Kitu ambacho pia hakiwezekani, kwa sababu kila mmoja wetu anafanya makosa.
Sasa kinachotokea, pale mtu anapokuwa amefanya makosa kwenye jamii hizi ambazo makosa hayapendwi ni nini? Inabidi mtu akimbie makosa yake, atafute sababu, atafute wa kumlaumu, na chochote kile ambacho kitamfanya mtu aonekane kwamba makosa siyo yake.
Wote hatujui tunachofanya, wote tuna uzembe na wote tunakosa umakini katika baadhi ya maeneo. Hivyo hatuwezi kuondokana kabisa na makosa. Na tunapojaribu kuyakimbia makosa hayo tunatengeneza matatizo makubwa zaidi kwa baadaye maana tutarudia makosa yale yale.
Leo nataka kukushirikisha hili, FANYA MAKOSA, YAMILIKI, YATATUE, NA WASHIRIKISHE WENGINE ULICHOJIFUNZA.
FANYA MAKOSA.
Kama unafanya jambo lolote kubwa kwenye maisha yako, huwezi kukwepa kufanya makosa. Hivyo ninaposema fanya makosa namaanisha fanya vitu ambavyo hujawahi kufanya hapo awali.
YAMILIKI MAKOSA YAKO.
Ukishafanya makosa usitafute sababu ya kujinasua, usitafute wa kumlaumu. Jua umefanya makosa na makosa hayo ni yako wewe mwenyewe.
TATUA MAKOSA YAKO.
Dawa ya kosa ni kulitatua, na ukishalimiliki kosa, kulitatua ni rahisi sana. Hata kama itaonekana kwa nje ni ngumu, ukishalikubali utaona njia nyingi za kulitatua.
WASHIRIKISHE WENGINE ULICHOJIFUNZA.
Watu wengi wameanzisha biashara kutokana na walichojifunza kwenye makosa waliyofanya awali. Ukishatatua makosa yako, washirikishe wengine kile ulichojifunza. Utawasaidia wengi zaidi, na huenda ukaanzisha biashara nyingine.
SOMA; Huhitaji Tena Kufanya Makosa Haya.
TAMKO LANGU;
Nimejua ya kwamba siwezi kuepuka kufanya makosa, kama nimechagua kuishi maisha ya mafanikio, ambapo nafanya mambo mapya na makubwa. na ninaposababisha matatizo, njia bora ya kuyatatua ni kwa kuanza na kuyamiliki makosa yangu mwenyewe, kuyatatua na kisha kuwashirikisha wengine kile nilichojifunza.
NENO LA LEO.
All men make mistakes, but only wise men learn from their mistakes. — Winston Churchill
Kila mtu anafanya makosa, lakini ni wale wenye busara ndio wanaojifunza kutokana na makosa yao.
Kuwa mwenye busara, jifunze kutokana na makosa yako, na ili ujifunze, kwanza yamiliki makosa yako. jua ni yako mwenyewe na yatatue.
Rafiki na Kocha Wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz
TUPO PAMOJA.