Watu wengi hufikiri biashara ni kwenda kununua vitu kwa bei ya jumla, kuja kuviweka kwenye eneo lako la biashara na kuuza kwa reja reja.
Unakaa eneo lako la biashara na mtaja akipita anaona upo pale unauza, anakuja, anauliza bei unamjibu, akitaka kununua unampa, kama asipotaka anaondoka.
Au wengine wanafikiri ukishakuwa na fedha, ukapata eneo zuri la kuweka biashara, ukaweka bidhaa, ukaajiri wafanyakazi basi wewe ulichobaki ni kuja kuvuna faida tu.
Kama kufanikiwa kwenye biashara ndio kungekuwa rahisi hivi basi kila mfanyabiashara angekuwa mbali sana.
Lakini tunaona wengi wanaanza biashara na zinawashinda.
Tunaona wengi wanakuwa na mitaji mikubwa, wanakodi maeneo ya biashara mazuri wanakuwa na bidhaa na wanaajiri wafanyakazi ila biashara zinashindwa kudumu.
Haya yote yanasababishwa na watu kutokujua majukumu yao kwenye biashara ni yapi.
Majukumu yako kwenye biashara siyo kuuza na kununua pekee, siyo kuajiri watu na kuja tu kufuatilia. Kazi yako wewe kama mmiliki wa biashara ni kubwa sana, na inahitaji uwe makini.
Na haya hapa ni baadhi tu ya mengi unayohitaji kufanya.
1. Unahitaji kujenga utamaduni wa biashara yako. Kila biashara ina utamaduni wake. Na utamaduni hii ni jinsi mambo yanavyofanyika, jinsi wateja wanavyohudumiwa, jinsi maamuzi muhimu yanavyofanywa, jinsi changamoto zinavyotatuliwa na mambo mengine muhimu kwenye kuendesha biashara yako.
2. Unahitaji kutengeneza hadithi ya biashara yako. Na hadithi hii unaitengeneza kupitia huduma unazotoa kwa wateja wako. Jinsi gani wanaridhishwa na biashara yako, na kitu gani kinawafanya waende kuwaambia wengine kuhusu biashara yako.
3. Unahitaji kuwa na maono makubwa ya biashara yako, na malengo ya muda mrefu unayoyafanyia kazi kila siku. Usifikirie tu kununua na kuuza kila siku, bali fikiria hapo ulipo ni daraja la kukupeleka mbali zaidi. Na jua ni wapi unapotaka kufika na utafikaje.
4. Unahitaji kuitangaza biashara yako kwa njia bora na za kisasa. Sio tu kwa kuonekana au kuweka matangazo, bali kuhakikisha unawafikia wale wote ambao wanaweza kunufaika na biashara unayofanya.
5. Unahitaji kutoa huduma bora sana kwa wateja wako. Pamoja na kutengeneza hadithi ya biashara yako, unahitaji kutoa huduma bora sana, huduma ambazo mteja atajisikia amepata kile anachotaka na kukutegemea zaidi.
Haya ni baadhi tu ya majukumu yako kama mmiliki wa biashara, ambayo hayafanani na yale uliyozoea kila siku ya kununua na kuuza.
Yafanyie kazi, usitake kuwa mfanyabiashara wa kawaida, kuwa mfanyabiashara bora na utafikia mafanikio makubwa.
Tupo Pamoja.