Kumpata mtu sahihi ni changamoto ambayo watu wengi sana wamekuwa wakikutana nayo.

Inawezekana kuwa unatafuta mtu sahihi wa kufanya naye kazi, au biashara.

Au pia unatafuta mtu sahihi wa kuishi naye kama mwenza wa maisha.

Huwa tunaweka sifa na vigezo mbalimbali na kisha kuanza kutafuta ni nani sahihi anayeweza kuendana na sifa na vigezo vyetu. Wakati mwingine tunapata ila mara nyingi tunakosa.

Na hata pale tunapopata, haichukui muda tunakuja kugundua mtu yule hakuwa sahihi kwetu.

Ni mara ngapi watu wanaanza mahusiano ya uchumba na kila mmoja anaamini mwenzake ni mtu sahihi kabisa kwake, wanakubaliana kwa hiari yao wenyewe kwamba wataishi pamoja, wanafanya harusi kwa furaha kubwa.

Lakini miezi au miaka michache baadaye ya kuishi pamoja, mambo yanabadilika na kila mmoja anaona mwenzake hakuwa mtu sahihi kwake. Maisha yanakuwa magumu na ya hovyo na wakati mwingine wanaishia kutengana.

Hali ni hii pia kwenye biashara, au kazi. Mtu anapata kazi na kusema hii ndio kazi ya ndoto yangu, kazi sahihi kwangu. Lakini baada ya muda anagundua sivyo alivyodhani.

Je haya yote yanatokana na nini?

Hii inasababishwa na kukosea tangu mwanzo kabisa, wakati w akutafuta mtu au kitu sahihi kwako. Ni vigumu sana kupata mtu sahihi kwako. Lakini kuna njia rahisi sana ya wewe kupata mtu sahihi kwako, bila ya kutafuta kwa nguvu. Na njia hii ndiyo tunajifunza hapa leo.

Njia bora na ya uhakika ya kupata mtu sahihi kwako iwe ni kwa mahusiano, kazi au biashara ni kwa wewe kuanza kuwa mtu sahihi. Kuwa mtu sahihi na utavutia watu sahihi. Kama wewe utaigiza utakutana na mwigizaji mwenzako na kama ujuavyo maigizo huwa hayadumu muda mrefu.

Usipoteze muda wako kutafuta mtu sahihi, anza wewe kwa kuwa mtu sahihi na utapata mtu sahihi kama unavyomtaka. Dunia huwa haidanganyi, vitu vinavyofanana vinavutana pamoja. Kuwa mtu sahihi na utapata mtu sahihi.

SOMA; FALSAFA MPYA YA MAISHA; Mtu Pekee Unayeweza Kumpa Furaha Kwenye Maisha Ni Huyu Hapa.

TAMKO LANGU;

Nimejifunza ya kwamba kuweka nguvu zangu nyingi kumtafuta mtu sahihi ni kupoteza muda wangu. Badala yake ninahitaji kuwa mtu sahihi na nitavutia watu sahihi kuja kwangu. Kuanzia sasa nitawekeza nguvu zangu kuwa mtu sahihi, na kwa mimi kuwa sahihi nitawavutia wale sahihi kuja kwangu.

NENO LA LEO.

“To find the right person, you must first BE the right person.”

― Merrill Markoe

Kumpata mtu sahihi, ni lazima kwanza wewe uwe mtu sahihi.

Usipoteze muda wako kutafuta mtu sahihi, anza wewe kuwa mtu sahihi na utawavuta watu sahihi kwako.

Rafiki na Kocha Wako,

Makirita Amani,

makirita@kisimachamaarifa.co.tz

TUPO PAMOJA.