Habari za leo rafiki?
Karibu tena kwenye mazungumzo yetu kwa siku ya leo, ambapo tunakumbushana mambo muhimu katika safari yetu ya maisha ya mafanikio.
Leo nataka tugusie eneo muhimu sana ambalo ni kujijengea kinga ya mafanikio. Yaani kuwa na kinga ambayo itakuwezesha kufikia mafanikio bila ya kuzuiwa na chochote kwenye safari yako.
Mtoto mdogo anapozaliwa, huwa anashambuliwa na magonjwa mengi akiwa mdogo kuliko mtu mzima. Na hii ni kwa sababu kinga yake dhidi ya magonjwa mbalimbali huwa inakuwa ipo chini sana.
Lakini unajua mtoto huyu anawezaje kupata kinga dhidi ya magonjwa hayo hatarishi kwake? Ni pale anapoumwa magonjwa hayo. Yaani mtoto anapoumwa ugonjwa fulani ndiyo mwili wake unatengeneza kiga dhidi ya ugonjwa ule, hivyo wakati mwingine hatasumbuka tena kama alivyosumbuka mara ua kwanza.
Wanasayansi baada ya kujua hili, wakatafuta njia ya mtoto kupata kinga ya magonjwa hatari na ndipo wakaja na chanjo. Unajua chanjo inafanyaje kazi? Ni kama unaambukizwa kwa makusudi ule ugonjwa ambao unataka kukingwa nao, ila unapewa kwa njia ambayo siyo kali sana, halafu mwili unaona ni ugonjwa na unatengeneza kinga. Hivyo ugonjwa halisi unapokuja, unakuta tayari mwili una kinga na hivyo haumsumbui tena mtoto.
Sasa leo tunakwenda kujifunza jinsi ya kutumia dhana hii ya kinga katika kuhakikisha tunafikia mafanikio makubwa kwenye maisha yetu.
Kabla hatujaangalia jinsi ya kujijengea kinga, ni lazima kwanza tujue ipi ni hatari yetu katika kufikia mafanikio. Na hatari zipo wazi, changamoto, kukatishwa tamaa, na hata kuchoka tu wewe mwenyewe.
Hivyo ni muhimu sana kuwa na kinga kwenye mambo hayo vinginevyo utajikuta unaishia njiani.
Sasa kinga tunaipataje? Ni kama ilivyo kwenye ugonjwa, labda tuugue, au tutengeneze mazingira ya kuugua.
Kwa changamoto ni lazima uzipitie, na unapopitia changamoto na ukaweza kuzivuka bila ya kukata tamaa, unakuwa umejijengea kinga kubwa sana. Changamoto kama hiyo haiwezi kukusumbua tena baadaye. Na hata changamoto nyingine hazitakuumiza sana kwa sababu tayari umeshaweza kutatua changamoto nyingine kubwa. Hivyo unapoingia kwenye changamoto, usilalamike wala kujaribu kuikimbia, badala yake ifurahie na jua hapo ndipo unapojijengea kinga ya mafanikio.
Pia unaweza kujijengea chanjo ya changamoto ni muhimu sana kuifanya kwani huwa inawasumbua wengi. Unajua sisi binadamu ni viumbe ambao huwa tunaridhika sana, mambo yakiwa yanaenda vizuri huwa tunajisahau kabisa na kuanza kufanya kile tunachofanya kwa mazoea. Ni mpaka pale hali ya mambo inapobadilika ndiyo sasa tunaona kuna hatari na kuanza kuhangaika.
Chanjo ya changamoto ni wewe kuishi nje ya COMFORT ZONE yako, yaani kufanya mambo ambayo hujazoea kuyafanya, kufanya mambo ambayo yanakupa hofu ya kufanya. Kadiria unavyofanya hivi mara kwa mara unajiongezea uimara wa kukabiliana na hali ambazo zinaweza zisiwe nzuri sana kwako kama zikikukuta hujajiandaa. Usikubali kabisa kufanya vitu kama ulivyozoea kufanya, jaribu kufanya vitu kwa utofauti, jaribu njia ambazo hujawahi kutumia, na jaribu vitu ambavyo unahofia unaweza kushindwa, hapa unaimarisha sana kinga yako.
Kwenye kukatishwa tamaa pia unahitaji kujijenge akinga kubwa sana, kwa sababu huu ni ugonjwa unaoua mafanikio haraka sana, hasa wanaokukatisha tamaa wanapokuwa ni watu wa karibu. Jijengee kinga kwa kuendelea kufanya licha ya watu kusema huwezi au utashindwa. Endelea kuweka juhudi ukijua ya kwamba utapata matokeo bora. Wewe angalia ule upande chanya tu, na usitake kubishana nao kwa maneno, badala yake fanya na wataona wenyewe. Na kama ndiyo umeamua kujijengea kinga kwa kufanya vitu vya tofauti, wewe mwenyewe utakuwa unajua hata ukishindwa utakuwa umejifunza kitu kipya, siyo sawa na ambaye hajajaribu kabisa.
Ni muhimu sana rafiki yangu ujijengee kinga ili uweze kufikia mafanikio makubwa kwenye maisha yako. Na jua unapokuwa mchanga kwenye safari hii ndiyo utashambuliwa sana na haya magonjwa ambayo ni changamoto, kukatishwa tamaa na hata wewe mwenyewe kuchoka. Lakini kadiri unavyozidi kwenda, changamoto zinaanza kuwa kitu cha kawaida na hata wanaokukatisha tamaa wanakuwa wameshachoka, kwa sababu wanaona hurudi nyuma na wanaanza kukuona ukifaidika.
Nakusihi tena rafiki yangu, usikubali kurudi nyuma, hii ni safari bora ambayo umechagua kufanya kwenye maisha yako, itakuwa na manufaa makubwa sana kwako hapo baadaye.
Nakutakia kila la kheri kwenye safari hii bora sana kwako.
TUPO PAMOJA,
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani.
makirita@kisimachamaarifa.co.tz