Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.


Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu WEWE NI KILE UNACHOJUA….
Uko hapo ulipo sasa,
Ukifanya kile unachofanya sasa,
Kwa sababu ya kile unachojua.

Maarifa uliyopata siku za nyuma ndiyo yamekujenga namna ulivyo sasa.
Ndiyo yamekujengea imani ulizonazo sasa
Na ndiyo yamepelekea ufanye yale unayofanya sasa.

Hivyo matokeo yoyote unayopata sasa, siyo kwa kubahatisha, bali ni wewe umeyatengeneza.
Hiyo ina maana kwamba, kama hapo ulipo sasa hapakutoshi, kama matokeo unayopata sasa hayakuridhishi, unayo nafasi ya kuchukua.
Na hatua ya kwanza ni kubadili kile unachojua,
Kupata maarifa sahihi ya kukufikisha kule unakotaka.
Kama kazi zinakusumbua, ni kwa sababu ya kile unachojua kuhusu kazi, unahitaji kupata maarifa tofauti kuhusu kazi na biashara ili uweze kufanikiwa.

Na kama kila siku una changamoto kuhusu fedha, basi msingi wake ni kwenye kile unachofahamu kuhusu fedha. Kubadili unahitaji kupata maarifa tofauti na sahihi kuhusu fedha.
Popote unapotaka kufika rafiki, tofauti na hapo ulipo sasa, lazima uanze kuweka maarifa tofauti na uliyonayo sasa.
Anza kuweka maarifa sahihi na tofauti, ili uweze kufikia ndoto zako.

Nakitakia siku njema sana ya leo rafiki yangu.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.