Hongera rafiki yangu kwa siku hii nzuri sana ya leo.
Ni nafasi bora na ya kipekee sana kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili tuweze kupata matokeo bora sana.


Msingi wetu ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku.

Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu KIFO CHA KUJITAKIA….
Kwenye kazi na biashara, wapo watu ambao wamekuwa wanachagua njia inayowapeleka kwenye kifo, yaani kazi na biashara zao kushindwa kabisa.
Watu hawa huwa wanachagua kufanya kile ambacho kila mtu anafanya na kukifanya kama ambavyo wengine wanafanya.

Anakosa chochote cha kumtofautisha na wengine na hivyo kuwa kwenye ushindani mkali ambao unapelekea kifo cha kile anachofanya.

Chochote unachofanya kwenye maisha yako, hakikisha kipo kitu cha kukutofautisha na wengine.
Hakikisha kuna namna ambavyo uko bora zaidi ya wengine.
Hakikisha kipo kitu ambacho kinapatikana kwako ila kwa wengine hakipatikani.

Hapo ndiyo unaweza kujiweka mbali na wengine na kuweza kufanya makubwa sana.
Siyo rahisi, ndiyo maana wengi hawafanyi.
Lakini inawezekana kufanya, na matokeo yake yatakuweka sehemu bora zaidi.
Unapochagua kuwa kama wengine, unakuwa umechagua kifo cha kujitakia, kwenye kile unachofanya.

Uwe na siku bora sana ya leo.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA,
http://www.makirita.info