Hongera rafiki yangu kwa siku hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni nafasi ya kipekee kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa, ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU na KUJITUMA, ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Asubuhi ya leo tutafakari kuhusu ACHA SABABU…
Kwenye maisha yako una uwezo wa kuchagua kuzalisha vitu viwili pekee;
- Kuzalisha matokeo.
- Kuzalisha sababu.
Ni hayo mawili tu watu wamekuwa wamezalisha tangu miaka na miaka, na ndiyo yamekuwa yanawatenganisha wanaofanikiwa na wanaoshindwa.
Wale ambao wanaochagua kuzalisha matokeo, wanaweka juhudi, wanapambana mpaka wanatoa kitu ambacho walitaka kutoa na kina msaada kwa wengine. Hapo katikati atashindwa, atakutana na changamoto na mambo yanaweza kuwa magumu lakini anapambana mpaka apate matokeo.
Wale wanaochagua kuzalisha sababu huwa hawajisumbui. Wanapanga kufanya, wanapoanza kufanya na kukutana na changamoto na vikwazo, hukimbilia kuangalia sababu ipi ambayo itakuwa siyo ya kijinga sana, na wanajipa hiyo. Wakikosa sababu isiyo ya kijinga, basi watatumia hata sababu ya kijinga, ili tu wajiridhishe nafsi zao kwamba tatizo siyo lao.
Ndiyo maana kila siku utawaona watu wanalaumu serikali, mazingira, hali ya uchumi, wazazi, wenza, watoto, ndugu na hata majirani kama kikwazo kwao kufika kule wanakotaka kufika.
Ukichukua sababu moja ambayo mtu anaisema, ukaichambua kwa undani, utaona wazi kabisa ya kwamba ni sababu isiyo ya msingi. Lakini watu wanazitumia na wanaridhishwa nazo.
Rafiki, chagua kuzalisha matokeo, achana na kuzalisha sababu. Tunaposoma historia, hatukutani na waliozalisha sababu, bali tunakutana na waliozalisha matokeo. Nina hakika kabisa wakati Mwl Nyerere na wenzake wanafuatilia kupata uhuru, wapo wengine nao walikuwa wakifanya hivyo, huenda kabla yao au wakati wao. Lakini hao wengine walikuwa na sababu, kwamba wakoloni hawawezi kukubali, kwamba hali siyo nzuri, kwamba mambo ni mazuri tu. Leo historia haiwakumbuki hao waliokuwa na sababu, bali walioleta matokeo.
Wakati wowote unapofanya jambo na ukaona sababu zinaanza kukunyemelea, achana nazo mara moja na weka juhudi mpaka upate matokeo unayotaka kupata.
Nenda kazalishe matokeo leo, tupa sababu mbali kabisa.
Nakutakia siku njema sana ya leo, uende ukafanye makubwa na kuweza kupata matokeo bora.
Rafiki yako,
Kocha Makirita Amani,
MAFANIKIO NI HAKI YAKO YA KUZALIWA.