KITABU; Philosophy for life and other dangerous situations : ancient philosophy for modern problems / Jules Evans
UKurasa 94 – 103.

Falsafa ya Epicurean inaweka msisitizo wa kuishi maisha ya raha muda wote na kuepuka aina yoyote ya maumivu.
Kitu ambacho kwa haraka kinaweza kuonekana ni kizuri, kwa sababu nani ambaye hapendi maisha ya raha?
Lakini dhana hii ina madhara kwa sababu kadiri mtu anavgojiuliza iwapo ana furaha au la, ndivyo anavyozidi kukosa furaha
Yaani kama kila wakati unajiuliza iwapo maisha yako ni ya raha, kwa sehemu kubwa yatakuwa siyo ya raha.

Lakini pia kuna zaidi kwenye maisha kuliko tu kuangalia kama mtu una raha au la.
Kwa mfano mambo mengi ambayo tunapaswa kufanya kwenye maisha, hayana raha ya moja kwa moja. Bali yana maana kwenye maisha yetu.
Kwa mfano mtu anapokwenda kupigana vita, siyo kwamba ana raha kufanya hivyo, bali mara nyingi kitendo hicho kina maana kubwa kwake, kujitoa kuilinda nchi yake na watu wake.

Kumekuwa na jitihada za nchi kupima viwango vya furaha kwa watu wake. Lakino vipimo hivi vimekuwa havina uhalisia. Kwani matokeo yamekuwa yanabaki kuwa sawa, licha ya kuwepo kwa changamoto tofauti tofauti katika nyakati za kupima.
Hivyo furaha ya mtu inaanzia zaidi ndani yake, na ni vigumu sana kuipima kwa nje.
Kama hilo lingewezekana, basi mataifa mbalimbali yangeweza kuwafanya watu wake kuwa na raha muda wote.

Tukazane kufanya yale yenye maana kwenye maisha yetu, na furaha itakuwa sehemu ya mchakato. Lakini kama tutakaa tukijiuliza kama tuna furaha au la, hatuwezi kuwa nayo.

Kocha Makirita Amani,
http://www.amkamtanzania.com/kurasa