Mambo yanabadilika kwa kasi sana, na biashara nazo hazijaachwa nyuma. Kuweza kupona kibiashara kwenye zama hizi za mabadiliko, lazima uwe mbele ya mabadiliko. Lazima uweze kubadilika kabla mabadiliko hayajafika.

Tabia za watu zinabadilika sana kwa sasa, na hii inakufanya wewe mfanyabiashara kuzielewa tabia za wateja wako, ili uweze kuwahudumia vizuri na kuwapa sababu za kuendelea kuwa wateja wa biashara yako.

customer concept shown in light bulb

Hapa kuna maswali matatu muhimu ya kujiuliza kuhusu wateja wako, ambayo yatakuwezesha kuwahudumia vizuri.

  1. Ni kitu gani unaweza kufanya haraka kwa wateja wako?

Tupo kwenye zama ambazo kama kuna kitu watu hawana, basi ni muda. Wateja hawana muda kabisa, hivyo chochote wanachotaka, wanakitaka sasa hivi. Kwa sasa ni vigumu sana mteja kukaa muda mrefu akisubiri kupata huduma, akiona muda w akusubiri ni mkubwa, anabadili mawazo na kuondoka.

Hivyo biashara yako inapaswa kuwa inayomwezesha mteja kupata kile anachohitaji, kwa haraka. Mteja asione anapokuja kwenye biashara yako anapoteza muda.

Pia bidhaa na huduma unazotoa, zimsaidie mteja kuokoa muda, kupata muda zaidi wa kufanya yale ambayo anaona ni muhimu kwake. Bidhaa au huduma yako isiwe kitu kinachopoteza muda wa mteja.

  1. Ni jukumu lipi unaweza kumpunguzia mteja?

Angalia kila biashara ya sasa, mteja anaahidiwa kupelekewa kile alichonunua popote alipo. Hii ni kwa sababu mteja tayari ana mambo mengi ya kufanya, hivyo anaweza kukosa muda wa kuacha yote na kuja kwenye biashara yako.

Hivyo biashara yako inapaswa kuwa na mfumo huu, ambapo inampunguzia mteja majukumu anayopaswa kufanya. Weka urahisi wa mteja kupata bidhaa au huduma pale alipo.

Iwapo biashara yako itakuwa inaongeza majukumu kwa mteja, utakuwa unawafukuza au huwapi hamasa ya kuja kwako.

SOMA; BIASHARA LEO; Mteja Mmoja Baada Ya Mwingine…

  1. Ni namna gani unamsaidia mteja wako kushinda?

Kila mtu anapenda ushindi. Kitu kinachowafanya watu wanunue ni imani kwamba kile wanachonunua kitafanya maisha yao kuwa bora zaidi. Kitafanya waepukane na changamoto au vikwazo wanavyokutana navyo sasa.

Hivyo jua kwa hakika ni maeneo gani unawawezesha wateja wako kushinda, na fanya kazi nzuri kuhakikisha wateja wako wanashinda kweli.

Maswali haya matatu, unapoyapatia majibu mazuri ndiyo yanayokuletea wateja kwenye biashara yako, na kuwafanya wateja wawe waaminifu kwenye biashara yako. Maswali haya ndiyo yataiwezesha biashara yako kujulikana na kukua zaidi. Kwa sababu yanamwezesha mteja kupata kile anachokitaka, kwa njia bora kwake na kwa haraka.

Jiulize na jipe majibu ya maswali hayo kila siku.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Makirita Amani,

Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu

Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog