Moja ya vitu muhimu kwenye kufikia mafanikio makubwa ni maono. Kama hujui unapokwenda, njia yoyote itakufikisha popote na kwa kuwa hujui unapokwenda, hutajua hata kama umefika.
Hivyo lazima maono yawepo, na maono siyo kitu cha kubadili kila mara kama mtu unavyojisikia, badala yake ni kitu ambacho unachagua na kukifanyia kazi hasa.
Hata pale mambo yanapokuwa magumu na kuona kama haiwezekani tena, hupaswi kubadili maono au malengo. Badala yake unapaswa kubadili njia za kukufikisha pale.
Unaangalia yale unayofanya, hatua unazochukua na matokeo unayopata, kisha unakazana kufanya kwa ubora zaidi ili kufikia maono yako.

Ukikimbilia kubadili maono au malengo yako, utaendelea kubadili hivyo kila mara. Kwa sababu kuna wakati utaona kama unachofanya ni kigumu na hakiwezekani, na wakati huo ukaona wanachofanya wengine ndiyo kizuri na kinachofaa. Ukiacha na kwenda kwenye kile unachoona ni rahisi, utafika wakati wa changamoto na utaona siyo kizuri tena kama ulivyofikiri.
SOMA; UKURASA WA 897; Hamasa Inapatikana Hapa….
Muhimu ni kuchagua na kutengeneza maono yako kwa umakini, yawakilishe yale ambayo ni muhimu sana kwenye maisha yako, zile alama unazotaka kuacha hapa duniani. Kisha fanya hiyo kuwa ramani ya maisha yako, kuwa msingi wako kwenye kila maamuzi unayofanya.
Unapokutana na ugumu au changamoto, hubadili maono, bali unabadili zile hatua unazochukua.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
Kwa kupata vitabu vya biashara na mafanikio tembelea www.kisimachamaarifa.co.tz/vitabu
Kupata blog ya kitaalamu unayoweza kuitumia kutengeneza kipato tembelea www.mtaalamu.net/patablog