When you arise in the morning, think of what a precious privilege it is to be alive – to breathe, to think, to enjoy, to love. – Marcus Aurelius

Hongera rafiki yangu kwa nafasi hii nzuri na ya kipekee sana ya leo.
Ni siku nyingine mpya, siku ambayo tuna nafasi ya kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana na kupiga hatua ya kuelekea kwenye mafanikio.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari SHUKURU KWA UPENDELEO HUU WA LEO….
Unapoamka asubuhi nzuri kama hii ya leo,
Ni rahisi sana kufikiri vitu ambavyo umekosa kwenye maisha yako,
Ni rahisi sana kufikiri mambo ambayo ulipanga kufanya jana ila ukaahirisha na kusema utafanya leo.
Ni rahisi sana kufikiria ratiba kali ya siku ya leo iliyopo mbele yako,
Ni rahisi sana kufikiria watu wanaokusumbua na kufanya maisha yako, kazi yako na hata biashara yako kuwa ngumu.
Ni rahisi sana kuona namna gani maisha yanazidi kuwa magumu na hali kuwa ngumu.

Na yote hayo ambayo ni rahisi kufanya, yana mchango SIFURI kwenye hatua unazoweza kupiga ili kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi.
Yanakufanya ukate tamaa na kuona mambo hayawezekani.
Lakini kama ukiangalia upande mwingine wa maisha yako, utaona ni kwa namna gani siku hii ya leo ni bahati na upendeleo kwako.

Kuweza kuamka leo ukiwa hai, ukiwa unapumua, ni upendeleo wa kipekee, siyo wote wameamka wanapumua leo.
Kuweza kuamka ukiwa na nguvu za kuweza kuchukua hatua mbalimbali kwenye maisha yako ni nafasi ambayo siyo kila mtu ameanza nayo leo.
Kuamka ukijua wapo watu wanaokupenda kama ulivyo, na unawapenda kama walivyo, ni upendeleo mkubwa sana kwako.

Badala ya kupoteza nguvu na muda wako kwenye yale ambayo hayapo sawa, na hilo kupelekea wewe kuona maisha ni magumu nanhayafai, hebu ianze siku hii kwa kufikiri na kutafakari yale ambayo yako sawa, yako vizuri na yanakuwezesha wewe kupiga hatua zaidi.

Siri kubwa kwetu binadamu ni kwamba, akili yetu inaturuhusu kuona kile tunachofikiri. Hivyo kama tutafikiri kwenye ubaya na uhaba, tutakachoona ni ubaya na uhaba kila mahali.
Lakini kama tutafikiri kwenye uzuri na wingi, kila kinachotuzunguka na tunachofanya kitakuwa kizuri na kwa wingi.
Yote yanaanzia kwenye fikra zetu.

Ukawe na siku bora leo rafiki yangu, siku ya kuziweka sawa fikra zako, ili kuweza kuona uzuri na utele wa maisha yako na ya wengine pia.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha