To the wise, life is a problem; to the fool, a solution. – Marcus Aurelius

Hongera sana mwanamafanikio kwa siku hii nzuri na ya kipekee.
Ni nafasi bora kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.

Asubuhi ya leo tutafakari MAANA YA MAISHA KWA MWEREVU NA MPUMBAVU….

Kwa mwerevu, maisha ni tatizo na hivyo mara zote hukazana kupata suluhisho la tatizo hilo.
Mwerevu anajua mafanikio kwenye maisha ni zao la kutatua matatizo ya wengine.
Mwerevu anajua kwenye maisha binafsi, ukitatua tatizo moja unapiga hatua ya kukutana na matatizo zaidi.
Mwerevu halalamikii matatizo, wala kuyakimbia, badala yake anayakaribisha na kuyatatua.

Kwa mpumbavu, maisha ni suluhisho, hivyo hataki kukutana na tatizo lolote.
Mpumbavu anapokutana na tatizo, anaanza kuangalia nani amesababisha tatizo hilo, anatafuta wa kulaumu na kulalamikia kwa tatizo hilo.
Mpumbavu hufanya kila namna kuiimbia tatizo na kukataa kwamba siyo lake au hajasababisha yeye.
Mpumbavu yupo tayari kujificha kwa muda kwenye vitu kama ulevi au usumbufu wa mitandao ili tu kujisahaulisha tatizo.

Mafanikio yako kwenye maisha yanategemea na upande uliochagua, na uelewa wako wa maisha unachangia upande unaochagua.
Kuwa mwerevu, jua maisha ni mfululizo wa matatizo, ambayo yapo ndani ya uwezo wako kuyatatua na yatatue.

Ukawe na siku bora sana ya leo rafiki yangu, tatua matatizo makubwa na ya muhimu leo, usiyakimbie.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha