If you want to improve, be content to be thought foolish and stupid. – Epictetus

Hongera rafiki kwa nafasi hii nyingine nzuri sana ya leo.
Ni fursa nzuri kwetu kwenda kuweka juhudi kubwa ili kuweza kupata matokeo bora sana.
Msingi wetu wa maisha ya mafanikio ni NIDHAMU, UADILIFU NA KUJITUMA ambapo tunakwenda kufanya makubwa leo na kila siku ya maisha yetu.
Mwongozo wetu wa maisha ya mafanikio ni TATUA, AMUA NA ONGOZA ambapo mwaka huu 2018 tutaweza kupiga hatua kubwa.

Asubuhi hii tutafakari KUBALI KUONEKANA MJINGA…
Moja ya vitu vinavyowazuia wengi kujifunza ni kutokutaka kuoneoana wajinga.
Kila mtu anapenda kuonekana anajua na hivyo hapati nafasi ya kujifunza zaidi.
Kila mtu anapenda kuonekana ana kitu cha kusema, ana maoni kwenye kila jambo.
Na mbaya zaidi, kila mtu ana cha kushauri kwenye kila kitu.

Hakuna ubaya wowote kwenye ujinga, kwa sababu hakuna anayeweza kujua kila kitu.
Ukikubali kuwa mjinga, japo kwa muda, utajifunza mengi sana.
Ukikiri kwamba hujui na kuomba watu wakujuze, utajua mengi sana.
Na baada ya hapo, hutakuwa tena mjinga kwenye eneo hilo.

Kila kitu ambacho unaona watu wanajua, wamejifunza. Hakuna aliyezaliwa anajua. Na walijifunza kwa sababu walikubali kuwa wajinga.
Hivyo kubali kuwa mjinga ili ujifunze. Na usione aibu wala kufikiria watu watakuchukuliaje, kama hujui kubali hujui na jifunze.
Usiogope kusema sijui, usiogope kusema nielekeze.

Ukawe na siku bora sana leo rafiki, siku ya kukubali hujui ili uweze kujifunza mengi zaidi.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,
http://www.kisimachamaarifa.co.tz kocha