DARASA LA JUMAPILI.

MADA; JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Habari wanamafanikio?

Jumapili hii kwenye muda wetu wa darasa, kuanzia saa 12 jioni mpaka saa 2 usiku, tutakuwa na darasa la JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Hili ni darasa muhimu kwa zama tunazoishi kwa sababu kutokana na wingi wa maarifa na taarifa, inakuwa vigumu mno kufanya maamuzi sahihi.

Katika darasa hili tutajifunza yafuatayo;

  1. Mafuriko ya maarifa na taarifa.
  2. Maana ya kufikiri kwa kina.
  3. Aina za kufikiri.
  4. Hatua za kufuata ili kufikiri kwa kina.
  5. Hatari za kuepuka wakati wa kufikiri kwa kina.
  6. Mfumo wa kufikia maamuzi sahihi wakati wa changamoto.

 

Karibuni sana wote kwenye darasa hili muhimu la kufikiri ili tuweze kufanya maamuzi sahihi.

Kumbuka mwaka huu mwongozo wetu ni TATUA, AMUA NA ONGOZA, kufikiri kwa kina ni muhimu kwenye kutatua matatizo, kufanya maamuzi na hata kuwaongoza wengine.

Rafiki na Kocha,

Dr. Makirita Amani,

www.kisimachamaarifa.co.tz/kocha

 

 

DARASA LA JUMAPILI.

MADA; JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

Karibuni sana kwenye darasa letu la leo kuhusu JINSI YA KUFIKIRI KWA KINA NA KUFANYA MAAMUZI SAHIHI.

UTANGULIZI; KWA NINI DARASA LA KUFIKIRI KWA KINA?

Kufikiri ni kitu rahisi kusema lakini kigumu sana kufanya.

Mwanafalsafa mmoja amewahi kusema kwamba watu wapo tayari kitafuta kila sababu lakini siyo kukaa chini na kufikiri.

Ni vigumu kufikiri kutokana na nidhamu ambayo mtu unahitaji kuwa nayo katika kufikiri na kuweza kufikia maamuzi sahihi.

Pia jamii zinazotuzunguka hazitutaki tufikiri, hivyo wengi wamekuwa wakifanya mambo kwa sababu ndivyo wamezoea yanafanyika, walizaliwa wakakuta watu wanafanya hivyo na wao wanaendelea kufanya hivyo.

Lakini kukaa chini na kufikiri, kunampa mtu uwanja mpaka wa kufanya kwa ubora zaidi.

Kitu kingine muhimu sana ni kwamba, tupo kwenye zama za maarifa na taarifa, na hivyo wale wanaofikiri kwa kina, ndiyo wanaoweza kufanya maamuzi sahihi na kuchukua haraka.

Sababu ya mwisho sana ya kila mtu kushiriki darasa hili ni namna ambavyo mambo yanakwenda sasa.

Kila mtu ana maoni na kuna mambo mengi ya kufanya, mtu kuweza kujua afanye kipi ni changamoto.

Hivyo kuwa na msingi sahihi wa kufikiri na kufikia maamuzi kutakusaidia sana kuepukana na changamoto mbalimbali.

Karibuni sana darasani.

 

 

KIPENGELE CHA KWANZA; MAFURIKO YA MAARIFA NA TAARIFA.

Kuna usemi kwamba kufa kwa kiu baharini ni ujinga, lakini hili ndilo ambalo linatokea kila siku kwenye zama hizi tunazoishi.

Kinachotokea ni kwamba, watu wanazungukwa na taarifa na maarifa mengi kiasi kwamba yanawazuia kujua ni hatua zipi wachukue.

Kadiri mtu anavyokumbana na maamuzi mengi, ndivyo ufanyaji wa maamuzi kwake unakuwa mgumu.

Zama tunazoishi sasa, ni zama ambazo kuna taarifa na maarifa mengi kuliko wakati wowote ule.

Leo hii, mtoto wa miaka 15 anazungukwa na maarifa na taarifa nyingi kuliko raisi wa marekani alivyoweza kuwa na maarifa na taarifa hizi kwenye karne ya 19 na hata ya 20.

Tungetegemea kwamba kwa maarifa na taarifa hizi, uwezo wa watu kufikiri na kufanya maamuzi kuwa mzuri, lakini mambo yamekuwa kinyume, badala ya uwezo wa kufikiri kuongezeka, umepungua.

Wengi sasa hawawezi tena kufanya maamuzi yao wenyewe, badala yake wanaangalia wengi wanafanya nini na wao kufanya.

Hali hii imewaingiza watu kwenye changamoto nyingi mno

  • watu wamesomea vitu ambavyo baadaye wamegundua haviwafai.
  • watu wameingia kwenye kazi ambazo baadaye wamekuja kuzijutia.
  • watu wameanzisha biashara ambazo zimekuja kuwashinda.
  • watu wameingia kwenye mahusiano ambayo yamewaumiza.
  • watu wamejiingiza kwenye fursa ambazo zimeishia kuwapa hasara kubwa.

Yote haya yangeweza kuzuilika kama mtu angechukua nafasi ya kufikiri kwa kina kabla ya kufanya maamuzi.

Kama watu wangeweka kelele za wengi pembeni, kama wangeweka husia kando, na kufikiri kwa kina, ukweli ungekuja mbele yao na kuwasaidia wasianguke.

 

 

KIPENGELE CHA PILI; MAANA YA KUFIKIRI KWA KINA.

Kwenye darasa letu hili la kufikiri kwa kina, na kwa madhumuni ya sisi kuweza kuchukua hatua, kufikiri kwa kina kutakuwa na tofauti na inavyochukuliwa na wengine.

Kwetu sisi, kufikiri kwa kina ni kuuona ukweli na uhalisia jinsi ulivyo, bila ya kufuata mkumbo au hisia. Kuona kitu kama kilivyo na kuweza kuchukua hatua sahihi.

Kuna maadui wakuu watatu wa kufikiri.

Adui wa kwanza ni mazoea (status quo).

Kwenye mazoea mtu unafanya kitu bila hata ya kufikiri kwa sababu ndivyo ulivyozoea kufanya.

Hii inakuwa hatari sana kwa sababu kwa jinsi mambo yanavyobadilika, yale yaliyofanya kazi nyuma hayawezi kufanya kazi sasa.

Adui wa pili ni mkumbo.

Nadhani kila mtu anajua hizi kauli..

Wengi wape…

Kifo cha wengi harusi…

Penye wengi hapaharibili neno…

Lakini uhalisia ni kwamba, wengi hawapaswi kupewa kwa wingi wao, na kifo cha wengi bado ni kifo. Na mara kwa mara penye wengi panaharibika mengi.

Adui wa tatu ni hisia.

Mara zote, hisia zikiwa juu, fikra zinakwenda chini.

Hisia na fikra haziwezi kwenda pamoja, kila mara hizia zinapokiwa juu, akili inatekwa na haiwezi kufikiri kwa kina.

Ndiyo maana kila ambaye amewahi kufanya maamuzi akiwa na hasira, huwa anakuja kujutia maamuzi hayo.

Kadhalika wanaofanya maamuzi wakiwa na furaha sana, wanakuja kugundua waliahidi vitu ambavyo ni vigumu kutekeleza.

Ni kupitia maadui hawa watu wanashindwa kufikiri kwa kina, na pia watu wanatumia maadui hao kuwalaghai watu wafanye maamuzi bila ya kufikiri kwa kina.

Mfano mtu anapokuambia angalia watu wengi wanafanya hilo, wote hao hawawezi kuwa wanakosea.

 

 

KIPENGELE CHA TATU; AINA ZA KUFIKIRI.

Kitaaluma zipo aina nyingi za kufikiri, na zinatofautiana kulingana na lengo ambalo mtu analo.

Lakini aina zote zinapelekea kufikia maamuzi ambayo yanamwezesha mtu kuchukua hatua fulani.

Zifuatazo ni aina maarufu zaidi za kufikiri.

  1. kufikiri kibunifu (creative thinking) hii inahusisha fikra ambazo zinakuja na kitu kipya, kitu ambacho hakijazoeleka au kujulikana. Mara nyinyine hii inaitwa kufikiri nje ya box
  2. kufikiri kwa uchambuzi (analytical thinking) hii inahusisha kuchukua dhama na kuigawa kwenye vipengele vyake, kuchambua kila kinachohusika ndani ya kitu.
  3. kufikiri kwa kina (critical thinking) hii inahusisha kuchambua na kufanya tathmini ili kujua ukweli, uhalisia, uhalali na thamani ya kitu. Aina hii ya kufikiri pia inahusisha kuvunja na hata kujenga upya hoja, ili kuweza kujua undani wake na usahihi wake.

Pia zipo aina nyingine za kufikiri ambazo kwa madhumini ya darasa la leo hazitakuwa na umuhimu. Aina hizo ni kama abstract, concrete, convergent, divergent na hata holistic thinking.

 

 

KIPENGELE CHA NNE; HATUA ZA KUFUATA ILI KUFIKIRI KWA KINA.

Kwa kuwa sasa tumeshaelewa kuhusu kufikiri kwa kina, na tumeshajua maadui wa kufikiri kwa kina, sasa tunakwenda kujifunza hatua za kufikiri kwa kina.

Zifuatazo ni hatua muhimu kufuata ili kuweza kufikiri kwa kina na kuweza kufanya maamuzi sahihi.

  1. Anza na msingi wa awali.

Mambo mengi ambayo watu wanafanya, wamekuwa wanafanya kwa mazoea, na hata wanapotaka kubadilika au kuboresha, wanaanzia pale walipo sasa. Hivyo wanachofanya ni kuongeza kitu kidogo sana lakini wanaendelea kufanya yale yale.

Dawa ya hii ni kufikiri kwa msingi wa awali. Hapa unajiuliza kama usingekuwa unafanya unachofanya, je ungefanyaje? Kama ungekuwa ndiyo mtu wa kwanza kabisa kuanza, je ungeanzaje?

Hapa unajifanya kama hujui kabisa namna ambavyo umekuwa unafanya, na hii inaifungua akili yako kuona njia mbadala.

Ili kukusaidia kwenye hili, angalia tatizo ulilonalo, na kile unachotaka kufikia, kisha fikiria njia mpya kabisa za kutatua tatizo hilo na hata kufikia pale unapotaka.

Hii ni njia nzuri sana ya kuja na wazo bora la biashara, badala ya kuangalia wengine wanafanya nini na kuboresha, unaanza kuangalia kama wengine wangekuwa hawapo kabisa, wewe ungefanya biashara gani? Na ungeifanyaje?

  1. Tilia mashaka kila kitu na kila mtu.

Inapokuja kwenye swala la kufikiri kwa kina, usimwamini mtu yeyote kwa asilimia 100, ndiyo, namaanisha mtu yeyote, haijalishi ni nani. Mpe kila mtu nafasi ya kukosea au kuwa na ajenda binafsi.

Ukishamtilia shaka kila mtu, sasa jiulize mtu huyu ananufaikaje na kile anachotaka wewe ufanye.

Angalia mtu anaweza kuwa haoni nini, maana kila mtu huwa ana upofu wake, hasa mtu anapopenda au kuchukia kitu, anaweza kuwa na hoja nzuri lakini ikawa imeharibiwa na kile anachopenda au kutokupenda.

Nb; usiwaambie watu kwamba huwaamini au una mashaka nao, hii ni mbinu yako ya kukuwezesha kudadisi zaidi.

  1. Angalia ajenda binafsi ambayo ipo nyuma ya mtu au kitu.

Pale mtu anapokuwa anakuambia kitu, angalia ni ajengda gani binafsi ipo nyuma ya mtu au kitu hicho. Mtu ananufaikaje kwa wewe kuchukua hatua, au anaumiaje kama wewe hutachukua hatua.

  1. Fikiria kinyume kabisa.

Kwa chochote unachoambiwa au kuona, jiulize kama ingekuwa kinyume chake, je ingekuwaje?

Kama watu wanakuambia kitu fulani huwa hakiwezekani, jiulize je kama kingewezekana, kingekuwaje? Hii inakusaidia kuondokana na mazoea na hata kuona kile ambacho wengi hawaoni.

  1. Tambua propaganda.

Taarifa na maarifa mengi ni propaganda, taarifa zinazotolewa kama za kawaida, lakini chini yake zina malengo tofauti kabisa ya kuwafanya watu wachukue au kutokuchukua hatua fulani.

  1. Angalia kama mtu anafanya anachosema.

Njia nyingine muhimu ya kuweza kuona kwa kina kile ambacho mtu anakuambia, hi kuangalia kama yeye anafanya au anaweza kufanya. Pia kuangalia kama mtu anahusika na yupo tayari kubeba madhara yanayotokana na kile anachosema. Hii ni muhimu sana kwenye ushauri wowote unaopokea kutoka kwa wengine.

 

 

KIPENGELE CHA NNE; HATARI ZA KUEPUKA WAKATI WA KUFIKIRI KWA KINA.

Tumeona maadui watatu wa kufikiri kwa kina.

Lakini zipo hatari nyingine za kuepuka pale unapofikiri kwa kina.

  1. Epuka kujumuisha.

Kamwe usijumuishe watu au vitu. Kwa mfano kwa sababu mwanamke mmoja au wawili wamekusaliti haipo sahihi kusema wanawake wote ndivyo walivyo. Kadhalika kwa vitu vingine kama sehemu, rangi, dini na hata makabila.

Ni kweli baadhi ya watu au vitu vina tabia zinazoendana, lakini kila kitu kinastahili kupewa nafasi yake.

Kujumuisha vitu kunakuzuia kufikiri kwa kina.

  1. Epuka kuwa na machaguo machache.

Katika kufikiri ili kufikia maamuzi, hakikisha unakuwa na machaguo mengi.

Ukiwa na chaguo moja huna chaguo, hiyo sasa ni lazima.

Ukiwa na machaguo mawili unakuwa njia panda, ufanye hili au lile.

Ukiwa na machaguo matatu, angalau sasa una nafasi ya kufanya uchaguzi.

  1. Epuka kuwa na machaguo mengi.

Machaguo yakiwa mengi sana, yanafanya kufikiri na hata kufikia maamuzi kuwa kugumu zaidi.

Kunachosha na mtu kuamua kuchukua chochote aunkutokuchukua chochote kabisa.

  1. Epuka hisia kali kama tulivyoona kwenye maadui wa kufikiri, subiri husia zitulie ndiyo ufanye maamuzi.
  2. Weka pembeni chuki au hukumu yoyote uliyonayo.

Unaweza kuwa unachukia vitu kwa sababu zako binafsi, sasa chuki hizo zinaweza kukuzuia kuona ukweli jinsi ulivyo.

Unapokiwa unafikiri na kufanya mamauzi, weka chuki na hukumu zako pembeni.

 

 

KIPENGELE CHA SITA; MFUMO WA KUFIKIA MAAMUZI SAHIHI WAKATI WA CHANGAMOTO.

Wakati wa changamoto ni wakati mgumu kufanya maamuzi kwa sababu  changamoto zinaonekana kama hatari kwenye maisha yetu.

Hivyo akili zetu huacha kufikiri na huwa tunafanya maamuzi yanayotokea mbele yetu kwa haraka.

Ili kuweza kufanya maamuzi mazuri kwenye wakati wa changamoto, unahitaji kuwa na maarifa na taarifa ambazo zinakiwa zimekujenga vizuri kifikra.

Kwa njia hii, yale ambayo umekuwa unajifunza na kufikiri wakati ambao siyo wa changamoto, yanakiwezesha kufikiri kwa usahihi.

Kila maarifa na taarifa unayopata yanaijenga akili yako kwa namna fulani. Hivyo kadiri unavyokuwa umejikusanyia taarifa na maarifa mengi kabla ya changamoto, ndivyo inavyokiwa rahisi kuyaleta pamoja wakati wa changamoto.

Wakati wa changamoto, hasa ambazo bi dharura, siyo wakati wa kuanza kutafuta maarifa na taarifa. Bali ni wakati wa kuyatumia.

Kuna kitu kinaitwa GUT INSTINCT yaani silika fulani inayokuwa ndani yako, ambayo inakufanya uamini kitu ni sahihi hata kama huna uhakika nacho au huna sababu ya kuelezea.

Sasa silika hii hujengwa na maarifa na taarifa unazozipata kila siku. Unakiwa na mfano hapa na mfano kule, unakuwa umejifunza kitu fulani kuhusu jambi fulani, mwisho unaweza kutumia yote hayo kufanya maamuzi sahihi.

HITIMISHO, MAONI NA MASWALI NA MAJIBU.

Hilo ndiyo darasa letu la leo kuhusu kufikiri kwa kina ili kiweza kufanya maamuzi sahihi.

Karibuni sana kwa mjadala, kwa maswali, nyingeza, mifano na chochote cha kutuwezesha kujifunza zaidi.

Karibuni sana.

SWALI; Sebastian Kalugulu: Kuna wakati unafikiri vyema na kujipa changamoto lakini unakuta miongozo inakupa maamuzi.

Mfano mahakimu na majaji. Machaguo waliyonayo ni Sheria tu. Hapo inabidi upingane na maamuzi yako.

JIBU; Ni kweli,

Kuna baadhi ya maeneo yana protocol za kufuata, ambazo nyingi hutokama na mazoea au tafiti ambazo zimedhibitisha ndiyo njia sahihi.

Lakini siyo mara zote zinakuwa sahihi.

Ila kwa maamuzi na matumizi binafsi, ni vyema mtu kujitengenezea protocol yako mwenyewe na kuiboresha kila mara.

SWALI; Sadick Kilasi: Je hizi aina za kufikiri zinatumika kutokana na aina fulani ya jambo unalofikiri?

JIBU; Ndiyo, inategemea na kile unachofikiri na lengo ni nini. Yaani matokeo ya mwisho unalenga nini. Kuelewa kitu, kujua ukweli wa kitu na kadhalika.

SWALI; Francis Kaijage: Asante saana coach kwa darasa hili zuri,,, binafsi nimefanikiwa kujua ni nini kufikiri kwa kina,, ila nataka kufahamu vema kufikiri kwa kina ndio kufanya tahajudi katika aina hizo za kufikiri.

JIBU; Tahajudi siyo aina ya kufikiri.

Tahajudi siyo hata kufikiri.

Tahajudi ni njia ya kuituliza akili, kuiondoa kwenye kufikiri, ili iweze kutulia na kuweza kufikiri vizuri zaidi baadaye.

SWALI; Godlove Ulomi: Maswali yangu kwako kocha.

Ni wakati gani wa kufikiri kwa kina kabla au n wakati wa kufanya jambo X.

Je ni sahihi kutumia nyanja zote za kufikri kwa kina kwenye jambo moja.

JIBU; 1. Wakati sahihi wa kufikiri kwa kina ni kabla, ili kiweza kufanya maamuzi sahihi.

Lakini pia kama umeingia kwenye maamuzi na kugundua hukufikiri kwa kina, una nafasi ya kufikiri kwa kina na kuweza kujua hatua zipi unaweza kuchukua.

  1. Ndiyo, unahitaji kutumia nyanja zote, hasa pale ambapo unachofikiri siyo dharura.

SWALI; Huvira Peterson: Asante kocha kwa darasa zuri, Umenikumbusha wakati wa uhai wa marehemu mume wangu! Kukiwa na topic alikuwa akisema hebu tufikiri vizuri halafu baada ya muda mrefu kupita ndio anaanzisha tena. Sasa issue ya muda inakuwaje maana kuna kusahau pia?

JIBU; Asante Huvira kwa mfano huu.

Kujipa muda kwenye kufikiri ni mbinu ya kutumia akili na uzoefu wako kuja na majibu sahihi.

Wazungu wanaita SLEEPING ON IT, yaani unakaa na wazo kichwani, bila ya kufanya maamuzi, la labda ukiwa umetulia kabisa, labda unalala au umeamka au unaoga, ghafla unapata mawazo yanayokuwezesha kufikia maamuzi.

Kwa mfano neno EUREKA limekuwa likitumiwa kama mchangao wa kujua kitu, ambapo inasemekana mwanasayansi Archimedes alikua anafikiria sana kuhusu kujua ujazo wa vitu visivyo na umbo. Sasa akawa anaingia kwenye bafu ya sink kuoga, akaona maji yanaongezeka kina kwa yeye kuingia, ndipo akagundua kile kina kilichoongezeka ndiyo ujazo ulioingia. Inasemekana alitoka uchi akikimbia na kusema eureka, eureka, na baadaye ilimwezesha kuja na ARCHIMEDES PRINCIPLE, ambayo ni sheria muhimu sana kwenye sayansi.

SWALI; Moses Mahenge: Ahsante sana kocha kwa darasa zuri,

Stress au msongo wa mawazo ni kufikiri sana ila mtu huyo anakuwa amekosa majibu au ni kitu kingine?

JIBU; Msongo unakuja pale mtu anapokuwa na mambo mengi anayofikiri, ambayo hafikii tamati au maamuzi, halafu pia anakuwa na hofu. Machaguo mengi pia na mtu machaguo yanaleta msongo.

MAONI; Sebastian Kalugulu: Ila nimeona ktk changamoto Za ugomvi hasa wa mapenzi unyumba na familia hilisomo linafiti vizuri sana.

Pia makazini tunapotoa maamuzi kuhusu jambo flani hatua hizi ni mihimu zaidi. Kwa watu wenye kampuni Za biashara na wanaoongoza NGO haya maarifa yana faida chanya sana asante sana kocha.

JIBU; Ni kweli Sebastian,

Tena kwenye kutatua changamoto kama za ugomvi ni muhimu sana kwenda na misingi hii, kwa sababu kwenye ugomvi kujua ukweli huwa inakuwa vigumu

SWALI; Beatus Elias Rwitana: Haya mambo mazito, somo zuri sana, ila maamuzi kama ya mahusiano, wakati mwingine kazi kwelikweli.

JIBU; Na wengi huumia sana hapo,

Kwa sababu fikra huwa hazipewi nafasi.

Lakini pia mtu una nafasi ya kudhibitisha hisia kwa fikra.

Kwa mfano kwenye sales kuna principle hii; people buy for emaotional reasons, then justfy with logic.

Ikiwa na maana kwamba, kinachowasukuma watu kununua vitu ni hisia, halafu wakishanunua wanajidhibitishia kwa fikra.

Nadhani umewahi kutoka nyumbani ukiwa huna mpango wa kununua kitu, halafu unakutana na muuzaji wa kitu, anakushawishi mpaka unanunua, halafu baada ya kununua ndiyo unaanza kujiambia lakininhata hivyo nisingeweza kupata kwingine kwa bei hiyo, au kuna siku jitakihitahi na kadhalika, hayo yanakuwa yamekuja baada na siyo kabla, kwa sababu kabla iligubikwa na hisia.

MAONI; EL SHAD BASHIRU: Asante Sana coacher!! Hakika jina KISIMA CHA MAARIFA linasadifu yaliyomo ndani,, Hakika tunajichotea Na wewe unatenda sehemu yako,, iliyobaki ni sisi, either kuchukua hatua Au kuacha.

SWALI;  Sadick Kilasi: Maandishi ni kufikiri, mfano vitabu, kwanini vina nguvu sana? Kama vitabu vya dini?

JIBU; Maandishi yana nguvu kubwa kwa sababu msomaji anatengeneza picha kwenye akili yake mwenyewe.

Vitabu vya dini vinakuwa na nguvu zaidi kwa sababu imani na hisia pia vinahusika.

SWALI; Moses Mahenge: Kocha hili suala la kufikiri lina uhusiano gani na akili?  Unaweza kuona mzazi anamwambia mtoto “we huna akili kweli umeshindwa kufikiri hata hili!!!”

JIBU; Ndiyo kuna uhusiano wa kufikiri na akili au ule uharaka wa kuelewa na kuchambua mambo.

Kwa sababu haya yote yanafanyika kwenye ubongo, ambapo wepesi wa kuelewa na kuchambua mambo, unasaidia mtu kufanya maamuzi bora na kwa haraka zaidi.

SWALI; Sebastian Kalugulu: Hivi kocha kwa nini Hisia ina nguvu sana kuliko Uhalisia? Na hasa pale mazingira yanapokuwa yanafanana Basi hasira huwa kubwa na busara huzidiwa. Ni swala la maumbile vichocheo (hormones) au ni tabia?

Mtu unamwambia sio kweli lakini anakuja na evidence statements unashindwa hata kuvumilia..

Hiki ndicho Beatus anasema kazi kwelikweli. Kwa wanajua kuunganisha matukio na kuongea sana hisia kwao ni 90% kuliko uhalisia.

JIBU; Hii ni dhana ambayo ipo kabisa,

Na kwenye neuroscience wanaiita AMYGDALA HIJACK, Hisia zinakuwa kali na akili inakuwa haifanyi kazi kabisa.

Ni dhana ndefu kidogo, mtu unaweza kujifunza kwenye kitabu cha Daniel Goleman kinachoitwa EMOTIONAL INTELLIGENCE, ameeleza dhana hii kwa kina.

SWALI; Geofrey Kiwia: Swali Langu ni hivi kuna wakati mzuri Wa kufikiri kwa kina zaidi.

JIBU; Wakati akili haijachoka.

MAONI; Elizabeth George chasusa: Ni kweli kwenye suala la kufikiri hasa maneno tunayotoa na kuwaambia watoto wetu yanaweza kuwaathiri kwa kiwango kikubwa zaidi ya tunavyofikiri, naenda kutoa kwa suala ambalo nilimuambia mwanangu kama wiki zimepita, lakini jambo hili japo nilimwambia kwa utani lakini nimekuja kujutia Leo ukizingatia ni mtoto wa miaka mitano, tulikuwa tunakula samaki na Mimi nikawa naacha kula vichwa na yeye akawa anakula, akaniuliza mama mbona huli vichwa Mimi kwa utani nikamwambia ukila kichwa cha samaki hayo macho anavyokuangalia ujue hata tumboni anaenda kukutazama hivyo hivyo, tukacheka nikaendelea na siku zikapita, Leo tunakula tena samaki naona na yeye anatoa vichwa na havili kabisa nikamuuliza mbona unaacha vichwa akanijibu kuwa wewe ulisema nikila vichwa samaki ataenda kuniangalia tumboni kwa hiyo Mimi naogopa samaki asije akaenda kuniangalia tumbo langu, kwa kweli nilicheka lakini nilipata funzo kubwa sana, hivyo ikabidi nimwambie ukweli kuwa vichwa samaki vina michanga ndio maana mie huwa sipendi kula, ndio akapata imani akaanza kula, kwa hiyo tuwe makini na kufikiri maneno tunayosema kabla ya kuwaambia watoto wetu

JIBU; Kama usingmemfafanulia angeweza kukua akiamini hivyo hivyo.

Kwenye moja ya mafundisho yake Zig Zigler alikuwa anapenda kutumia sana mfano huu.

Anasema kuna bwana mmoja aliona mke wake, sasa kila akileta samaki mke wake kabla ya kumipka anamkata mkia. Akaona hilo linaendelea kila mara ikabidi siku moja amuulize, akamjibu ni kwa sababu mama yangu alikuwa anafanya hivyo. Basi wakasema tumpigie simu mama, mama alipoulizwa kwa nini alipokuwa anapika samaki anamkata kwanza mkia? Akasema yeye alikuwa anaona mama yake anafanya hivyo.

Kwa bahati nzuri mama wa mama, yaani bibi alikuwa bado hai, basi wakasema wampigie simu ili kupata suluhisho, alipopigiwa bibi akasema mimi nilikiwa namkata samaki mkia kwa sababu kikaangio changu kilikuwa kidogo hivyo haenei vizuri.

Mazoea yalikuwa yameenda kwa vizazi viwili bila ya kujua sababu halisi na kwamba kwao haikiwepo tena.

SWALI; Mahule Peter: Je Kocha Tafiti mbalimbali zinasemaje kuhusu hii GUT INSTICT? Je ni vema kuifuata pale unapokutana nayo au inakuwaje hapo? Yaani kuifuata hata kama huna uhakika au kusimama?

JIBU; Tafiti zinaonesha kwa wale wenye uelewa mpana wa mambo, GUT INSTINCT zao mara nyingi huwa sahihi, lakini wasio na uelewa mpana, huwa ni majanga.

MAONI; Goodluck Moshi: Kipengele cha NNE kimenipa jambo la kunisaidia sana hasa la kumpa nafasi ya kila mtu kukosea, na hata la kuwaza pande mbili za kuwa mtu atafaidika na nini kwa kutekeleza anachokuambia au atapata hasara gani kwa kutotekeleza.

MAONI; Goodluck Moshi: Ni muhimu pia kutengeneza protocol utakayokuwa unaitumia kufanya maamuzi , nimeona hili katika Project Management Institute ya Marekani wanao muongozo ambao unawaguide project managers duniani wanapokuwa katika dilemma , hichi alichosema kocha ni muhimu sana pia kuimplement katika maisha yetu ya kila siku.