Kama unapunguza bei kwa sababu gharama zako za uzalishaji au za kuendesha biashara zimepungua na unajali wateja wako wapate kilicho bora, hongera sana.
Lakini kama unapunguza bei kwa sababu unataka wateja wengi zaidi waje kwako badala ya kwenda kwa washindani wako kibiashara, nina habari mbaya kwako, huo ni uvivu wa kibiashara.
Kupunguza bei kama njia ya kushindana kwenye biashara ni uvivu wa kibiashara, uvivu wa kufikiri na kutokuwa tayari kuweka thamani kubwa zaidi ili mteja aweze kulipia zaidi.
Na uvivu huo wa kibiashara utakugharimu sana, maana unapopunguza bei, unapunguza kiasi cha faida unayopata, ukipunguza faida unashindwa kutoa huduma bora na hivyo unajikuta ukitoa huduma mbovu zaidi.
Pia unapopunguza bei kama sehemu ya kuvutia wateja, unachofanya ni kuvutia wateja wasioajili chochote ila bei. Hawa ni wateja wasumbufu sana, ambao watayafanya maisha yako kibiashara yawe magumu sana.
Kwa sababu hata baada ya kupunguza bei, wataamini unawauzia kwa bei ya juu, na ikitokea mwingine anauza kwa bei ya chini kuliko wewe, wateja hao watakuhama na kwenda wanakoweza kupata bei rahisi zaidi.
SOMA; BIASHARA LEO; Viashiria Kwamba Umeshaingia Kwenye Ushindani Utakaokupoteza Kibiashara.
Kama unataka kudumu kwenye biashara, kama unataka biashara yenye mafanikio makubwa, basi usikimbilie kupunguza bei, badala yake kazana kuongeza thamani. Weka muda wako, juhudi zako na ubunifu wako katika kutoa thamani kubwa, thamani ambayo inamfanya mteja atatue matatizo yake, thamani ambayo mteja hawezi kuipata sehemu nyingine yoyote.
Ukiwa na thamani ya aina hii, utawavutia wateja sahihi, wateja wanaojali kile wanachopata na siyo bei. Ukiwahudumia vizuri wateja hawa wanakuwa siyo wasumbufu, utaenda nao kwa muda mrefu na watakuletea wateja wengi zaidi.
Kama umejitoa kuingia kwenye biashara, basi pia jitoe kuweka kazi ya kutosha, ili kutoa thamani kubwa kwa wateja wako. Usikimbilie kupunguza bei, itakugharimu sana kibiashara na hata kimaisha.
Kila la Kheri Rafiki Yangu.
Rafiki na Kocha wako,
Dr. Makirita Amani,