Mafanikio kwenye biashara siyo kitu kigumu kama wengi wanavyofikiri. Ni kujua kanuni sahihi ya mafanikio ya biashara yako, kisha kuifanyia kazi huku ukiwa na subira na uvumilivu.

Wengi wanaoshindwa kwenye biashara wanakosa kanuni sahihi ya kufanyia kazi au wanakosa subira na uvumilivu.

Na kwa kuwa mafunzo ya biashara ni mengi, kujua kanuni siyo pagumu, ila kuwa na subira na uvumilivu ndipo wengi wanaposhindwa.

Watu wengi wanapenda mafanikio ya haraka kwenye biashara zao, hivyo wengine hujikuta wakitafuta njia za mkato ambazo zinawaingiza kwenye matatizo makubwa zaidi.

SOMA; BIASHARA LEO; Chagua Wateja Kabla Ya Kuanza Biashara.

Kuna maeneo sita unayohitaji kuwa sahihi kwenye biashara yako, ili uweze kuendesha biashara yenye mafanikio makubwa.

  1. Kuwa eneo sahihi, biashara yako lazima iwe eneo sahihi, eneo lenye watu wenye uhitaji wa kile unachouza.
  2. Kuwepo wakati sahihi, kila uhitaji wa watu una wakati maalumu, biashara yako inapaswa kuwafikia wateja kwa wakati sahihi.
  3. Kuwa na suluhisho sahihi, hivyo lazima ujue wateja wana uhitaji gani, wana shida gani, wana changamoto gani, kisha kuwa na suluhisho sahihi kwao.
  4. Kuwa na mawasiliano sahihi, wateja wako hawatajua kama upo na unaweza kuwapa wanachotaka, hivyo unahitaji kuwa na mawasiliano sahihi yatakayowawezesha wateja kujua kuhusu wewe na kuja kwako.
  5. Kuchukua hatua sahihi, ili biashara yako ipige hatua, lazima uweze kuchukua hatua sahihi kulingana na hali unayokuwa unapitia.
  6. Malipo sahihi, lazima wateja wawe tayari na wamudu kulipa malipo sahihi ambayo kwako yatakupa faida. Kama utakazana kuuza chini ili kupata wateja wengi, lakini usipate faida, biashara itakuwa ngumu sana kwako.

Muhimu kabisa kwenye mambo hayo sita unayopaswa kuwa sahihi kwenye biashara yako ni KURUDIA. Fanya kwa usahihi kisha rudia tena na tena na tena. Siyo mara zote utapata matokeo makubwa, lakini kama utaendelea kufanya, utapata matokeo bora sana.

Fanya yaliyo sahihi na rudia kuyafanya zaidi na zaidi na hayo ndiyo mafanikio kwenye biashara yako. Mara zote jifunze kwa kila hatua unayochukua, na kuwa mvumilivu hasa.

Kila la Kheri Rafiki Yangu.

Rafiki na Kocha wako,

Dr. Makirita Amani,

www.amkamtanzania.com/kocha